Simba mitandaoni haikamatiki

HAPA nchini licha ya kwamba timu za soka zenye mashabiki wengi Ligi Kuu Bara kuwa ni Simba na Yanga, lakini bado wapo ambao wanazifuatilia nje ya uwanja klabu hizo ambazo zimejizolea wafuasi wengi katika mtandao wa kijamii wa Instagram. Mwanaspoti limefanya utafiti kujua klabu gani za Ligi Kuu zenye wafuasi wengi katika mtandao huo unaopendwa na watu wengi.

SIMBA (Mil 1.6)

Kitendo cha Simba kunyakua ubingwa mara tatu mfululizo kinaweza kuwa ndio sababu ya kukusanya kijiji katika mtandao huo. Simba ndio timu inayoongoza kwa kuwa na wafuasi wengi ikiwa nao milioni 1.6. Licha ya kuwa na idadi hiyo ya wafuasi, pia wachezaji wake hawapo nyuma kwa kuwa na vijiji kibao kwenye m mtandao huo. Miongoni mwa wachezaji wao wenye wafuasi wengi ni Shomari Kapombe (122,000), Meddie Kagere (340,000), Aishi Manula (432,000), Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (511,000).

Wengine ni Clatous Chama (258,000), Jonas Mkude (312,000), Gerson Fraga (145,000), Bernard Morrison (144,000) na Luis Miquissone (107,000).

YANGA (815,000)

Yanga ina wafuasi 812,000 katika mtandao huo wa kijamii, hivyo imepitwa na watani zao, Simba. Hii inaweza kuchangiwa na timu hiyo kukosa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo.

Licha ya mambo kuwa hivyo, lakini huko mtandaoni wana nafasi ya kuendelea kujiongezea wafuasi wapya kutokana na usajili walioufanya.

Wakati mambo yakiwa hivyo kwa Yanga, wachezaji wake wana vijiji kwenye mtandao huo miongoni mwao ni Feisal Salum ‘Fei toto’ (90,200), Metacha Mnata (53,300), Michael Sarpong (41,900), Carlinhos (79,000) na Haruna Niyonzima (29,000).

AZAM (532,000)

Tangu Azam FC ipande Ligi Kuu, imechukua ubingwa mara moja - 2014, lakini katika mtandao huo ina wafuasi 532,000. Miongoni mwa wachezaji wa Azam FC wenye wafuasi wachache huko Instagram ni pamoja na Price Dube (3,524), lakini wapo wenye vijiji vyao ambao ni pamoja na Shaaban Chilunda (65,500), Frank Domayo (37,900) na Salum Abubakari ‘Sure Boy’ (31,100).

MTIBWA SUGAR (171,000)

Mtibwa Sugar ya Morogoro imejikusanyia wafuasi 170,000 huko Instagram ambao wanaifuatilia.

Nyota wa zamani wa Yanga na Nkana FC ya Zambia, Hassan Kessy ndiye mwenye kijiji cha watu akiwa nao 58,300.

KMC (120,000)

Tangu KMC ipande daraja misimu mitatu iliopita, imepata wafuasi 120,000 huko Instagram. Kinara mwenye wafuasi wengi kwa wachezaji ni kipa Juma Kaseja aliye na kijiji chenye watu 202,000. Wanaomfuatilia ni beki wa zamani wa Yanga, Andrew Vicent (99,000) na Sadala Lipangile (47,000).

MBEYA CITY (95,800)

Tangu Mbeya City, ipande imekuwa ikijiongezea ufuasi viwanjani na mitandaoni. Katika mtandao wa Instagram ina wafuasi 95,800.

Nyota wengi wa Mbeya City kurasa zao za Instagram zina wafuasi wa kawaida mfano nahodha, Mpoki Mwakinyuke anao 653, huku Kibu Denis akiwa nao 96.

POLISI TANZANIA (35,200)

Polisi Tanzania katika mtandao wake wa kijamii imejikusanyia wafuasi 35,200.

Supastaa wa timu hiyo, Marcel Kaheza ana wafuasi 18,500, ilhali Joseph Kimwaga aliyejiunga na klabu hiyo hivi karubuni anao 46,900. Idadi hiyo ya wafuasi ni kubwa kuliko hata ya klabu yake.

TANZANIA PRISONS (33,100)

Katika mtandao huo, unaonyesha timu hiyo ina wafuasi 33,100. Mfungaji wa bao la Tanzania Prisons kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, Lambaty Charles uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, ana wafuasi 4,995, Jacob Zuma (1,419) na Jeremiah Kisubi anawafuasi 193.

KAGERA SUGAR (25,900)

Pamoja na kuwepo muda mrefu kwenye Ligi Kuu Bara, Kagera Sugar ina wafuasi 25,900 kwenye Instagram. Kinara wa mabao wa msimu uliopita wa timu hiyo, Yussuf Mhilu ana wafuasi 7,556 kwenye ukurasa wake wa Instagram.

COASTAL UNION (72,600)

Katika mtandao huo Coastal Union ina wafuasi 72,600 wanaoutembelea kuona kilichowekwa kuhusiana na soka. Hakuna mchezaji mwenye maajabu kwenye kikosi cha Coastal Union katika mtandao wa Instagram, ukiondoa Abdul Sopu ambaye wamemsajili kutoka Simba SC ana wafuasi 3,879 na Yusuph Abbas Soka anao 1,305.

NAMUNGO FC (53,600)

Tangu ipande daraja misimu mitatu iliopita, imefanikiwa kujikusanyia wafuasi 53,600 ambao wanatembelea kuona maendeleo ya timu.

Winga Shiza Kichuya ambaye amejiunga na Namungo kwa mkopo ukurasa wake wa mwanzo wa mtandao huo wa kijamii una wafuasi 145,000, lakini bahati mbaya wajanja wameuchezea hivyo imembidi kufungua mpya wenye wafuasi 5,557, ilhali Lucas Kikoti ana wafuasi 4,658.

RUVU SHOOTING (5,457)

Timu hiyo yenye maskani yake Pwani ambayo ina msemaji machachari Masau Bwire katika mtandao wake wa Instagram imejikusanyia wafuasi 5,457.

Graham Naftal ni miongoni mwa wachezaji wenye wafuasi wengi kwenye mtandao wa Instagram akiwa nao 2,310.

GWAMBINA FC (20,700)

Pamoja na timu hiyo kupanda daraja msimu huu, imejikusanyia wafuasi 20,700 kwenye mtandao wake wa Instagram ambao wanafuatilia kujua habari za Gwambina FC. Nyota wa zamani wa Mbeya City, Yanga na Lipuli ya Iringa, Paul Nonga ni miongoni mwa wachezaji wa Gwambina wenye wafuasi wengi zaidi kwenye mtandao huo akiwa nao 28,900.

IHEFU SC (20,800)

Ihefu SC haiko nyuma mitandaoni licha ya kupanda daraja msimu huu, kwani imeweza kujikusanyia wafuasi 20,800 kwenye mtandao wao Instagram.

Cyprian Kipenye ni miongoni mwa wachezaji wa Ihefu ambaye ukurasa wake wa Instagram unasomwa na wafuasi 1,456. Mchezaji huyo ni kinda wa Simba anayeichezea timu hiyo kwa mkopo wa msimu mzima.

DODOMA JIJI (16,500)

Timu hii ni miongoni mwa zilizopanda daraja msimu huu, na mpaka sasa imefanikiwa kujikusanyia watu 16,500 kwenye mtandao wa Instagram. Kwa Dodoma Jiji miongoni mwa wachezaji wao wenye wafuasi wengi kwenye mtandao huo ni Salmin Hoza anayeichezea kwa mkopo akitokea Azam akiwa nao 6,780 na Peter Mapunda ana wafuasi 1,225.

BIASHARA UNITED (24,100)

Haijalishi ipo mkoani, lakini kuna watu ambao wanawafuatilia kwenye mtandao wao wa kijamii Instagram kujua kinachoendelea ndani ya timu hiyo. Mpaka sasa Biashara ina wafuasi 24,100.

Katika kikosi hicho mdogo wake na Abdi Banda, Omary ni miongoni mwa wachezaji wa Biashara wenye wafuasi wengi kwenye mtandao wa Instagram anakiwa nao 16,200.

MWADUI FC (708)

Pamoja na kuonekana inakosa ushindani wa kuwa katika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Mwadui FC ina wafuasi 708 katika mtandao wao huo wa kijamii.

Miongoni mwa nyota wanaounda kikosi cha Mwadui ni pamoja na Joram Mgeveke mwenye wafuasi 1,384 wakiwa ni wengi zaidi kuliko ilionao klabu yake.

JKT TANZANIA

JKT Tanzania ndio klabu pekee ya Ligi Kuu Bara ambayo haina ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Licha ya klabu hiyo kutokuwa na ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii, Jabir Aziz ambaye ni mchezaji wao anao wafuasi 13,000.