Simba kwa Nkana ni vita ya kisasi, ila kwa Songo heshima

Muktasari:

  • Simba kwa sasa imejiwekea lengo ya kurudia rekodi yake ya 2003 ilipofuzu kwa mara ya kwanza kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Dar es Salaam. Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba baada ya kuichakaza Mbabane Swallows na kusonga mbele kwa Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 8-1, sasa inasubiri mshindi kati ya Nkana ya Zambia dhidi ya UD Songo ya Msumbiji itakayochezwa leo.

Katika mchezo wa jana Simba, ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 ugenini kwa magoli yaliyofungwa na Cletus Chama mawili, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere kila moja akifunga bao mmoja.

Ushindi huo unaifanya Simba kuwa karibu zaidi kucheza dhidi ya Nkana ambayo inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na faida ya mabao mawili ya ugenini baada ya kuichapa UD Songo 2-1 katika mechi ya awali jiji Maputo.

Mashabiki wengi wa Simba wangependa kuona timu yao inacheza dhidi ya Nkana FC inayochezewa na beki wao wa zamani Ramadhani Kessy.

Simba imeanzishwa 1936, wakati Nkana ilianzishwa 1935, ila klabu hizo mbili zote zinafanana kwa kuvaa jezi nyekundu.

Simba wanaitaka Nkana wakiwa na lengo la kulipa kisasi cha mwaka 2002 walipokutana kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa 2002, katika mchezo wa kwanza uliofanyika mjini Kitwe Nkana ilishinda 4-0, lakini katika mechi ya marudiano iliyofanyika Dar es Salaam, Simba ilishinda 3-0 lakini Nkana ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.

Mbali ya mchezo huo, rekodi inaonyesha tangu mwaka 1974, Simba imeshinda mechi tatu kati ya tano ilizocheza dhidi ya klabu za Zambia katika mashindano mbalimbali ya Afrika.

Mwaka 1974, Simba ilitoa Green Buffaloes ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-1 katika Kombe la mabingwa Afrika. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Zambia, Simba ilishinda 2-1 dhidi Buffaloes na marudiano ikishinda 1-0.

Mwaka 1976, Green Buffaloes ya Zambia ililipa kisasi kwa kuiondoa Simba kwa jumla ya mabao 4-2, katika mchezo wa kwanza ugenini Simba ilichapwa 3-2 na marudiano ilifungwa 1-0.

Simba ilirudi tena Zambia mwaka 1995, ilifanikiwa kuitoa Power Dynamos kwa penalti 3-4 baada ya mechi mbili ya nyumbani na ugenini kulazimisha sare 1-1 hivyo matokeo ya jumla kuwa 2-2 ndipo penalti zilipotumika kumpata mshindi.

Mwaka 2004, Simba ilitolewa mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Zanaco FC ya Zambia baada ya kufungwa kwa jumla ya mabao 3-2. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam Simba ilishinda 1-0, lakini mechi ya marudiano Zanaco ilishinda 3-1 na kusonga mbele.

Safari ya Msumbiji iwapo UD Songo itawatoa Nkana FC, basi hiyo itakuwa ni mara ya tatu kwa Simba kwenda jijini Maputo ikiwa na rekodi ya kutolewa mara moja na klabu za Msumbiji.

Katika mashindano ya mwaka 2005, Simba ilifanikiwa kusonga mbele baada ya kuichapa Ferroviario Nampula kwa jumla ya mabao 3-2. Simba ilitumia vizuri uwanja wake wa nyumbani kwa kushinda 2-1 Dar es Salaam, kabla ya kulazimisha sare 1-1 jijini Maputo.

Miaka miwili baadaye katika Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ilikubali kipigo cha jumla cha mabao 5-3 kutoka kwa Textil do Pungue na kuaga mashindano.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Maputo, Simba ilifanikiwa kulazimisha sare 1-1, kabla ya kukubali kipigo cha mabao 4-2 katika mchezo marudiano uliofanyika Dar es Salaam.

MATOKEO JUMLA YA SIMBA 1974-2007

1974: Green Buffaloes (Zambia) 1-3 Simba

1976: Green Buffaloes (Zambia) 4-2 Simba SC        

1979: Simba 5-4 Mufulira Wanderers (Simba)

1995: Power Dynamos (Zambia) 2–2 (3–4 p) Simba        

2002: Nkana FC (Zambia) 4–3 Simba

2004: Simba 2–3 Zanaco (Zambia)

2005: Simba 3–2 Ferroviario Nampula (Msumbiji)

2007 Textil do Pungue (Msumbiji) 5 - 3 Simba