Simba kuzindua logo, jezi mpya

Thursday August 13 2020

 

By THOBIAS SEBASTIAN, ELIYA SOLOMON

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara Simba SC kesho Agosti 14, 2020 watazindua Wiki ya Simba ambayo msimu huu itatambulika kama 'Champions week, another level'.

Ofisa habari wa Simba, Haji Manara alisema kuna mambo mengi ambayo watayafanya msimu huu kwani walikuwa na msimu bora kwa kuchukua makombe manne.

Manara katika uzinduzi huo na wataanza na mambo matatu ambayo mchana wataanza na kuzindua nembo mpya ya timu.

"Baada ya muda mchache kuonesha nembo mpya ya klabu ambayo tulianza mchakato baada ya mabadiliko tutazindua jezi mpya za msimu wa 2020-21, ambazo tulipanga kuzizindua siku ya fainali ya kombe la Shirikisho (ASFC)," alisema.

"Tutamaliza na tukio la siku kwa kutambulisha wachezaji wetu wapya ambao tumewasajili msimu kwani hatukuwa kimya katika zoezi la kusajili kulingana na mahitaji ya kikosi chetu," alisema.

"Siku ya Jumamosi Agosti 15 Wanasimba wote tutakuwa na tukio la kwenda kufanya usafi katika eneo la daraja la Salenda pembezoni mwa ufukwe wa bahari tukiwa sambamba na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Hazani Zungu.

Advertisement

"Jumapili Agosti 16 tutakuwa na tukio la kuomba dua kwa marehemu na wakongwe wote wa Simba waliotangulia mbele ya haki na tukio hili litafanyika pale makao makuu ya klabu yetu saa 6 mchana na tunaomba Wanasimba wote wajitokeze kwani baada ya tukio hili kutakuwa na chakula.

"Jumatatu na Jumanne zitakuwa siku maalumu kwa Wanasimba wote kuunga juhudi za serikali kwenda kujitokeza katika vivutio vya nchi hii kwa kufanya utalii wa ndani na tutaomba kama itawapendeza wenye mamlaka kutupa punguzo," alisema Manara.

"Jumanne hiyo hiyo tutakuwa na mkutano ambao tutatangaza viingilio, timu ambayo tutacheza nayo, mechi itaanza muda gani na masuala mengine ya msingi ambayo yatakuhusu jambo hili," aliongezea Manara.

Manara alisema kwa kishirikina na wadhamini wao SportPesa watakwenda katika timu za mitaani ili kugawa vifaa vya michezo ikiwemo jezi.

"Siku za Jumatano, Alhamisi na Ijumaa itakuwa siku maalumu kwa Wanasimba nchi nzima huko walipo kwenda kuchangia damu katika vituo mbalimbali ambavyo watakuwa wamejipanga," alisema.

"Mbali ya ubora wa kikosi cha Simba, benchi la ufundi na Uongozi mambo kama haya ya huruma kurudisha kwa jamii ndio yamechangia kutupa mafanikio msimu huu," alisema.

"Alhamisi tukiwa na wachezaji wetu wote tutakwenda katika shule ya Uhuru ambapo kuna wanafunzi wenye matatizo mbalimbali na klabu itatoa vitu mbalimbali ambavyo itakuwa imejaliwa navyo.

"Jumamosi Agosti 22 ndio kilele chenyewe cha wiki ya Simba na mara ya kwanza tutatumia viwanja viwili kwa maana Taifa ambao tutatumia kucheza mechi na Uhuru ambao tutafunga luninga ili mashabiki kuona ambavyo vinaendelea huku tukiwa na sapraize nyingi.

"Jumapili ndio itakuwa hitimisho kwa kufanya sherehe tukiwa pamoja na wageni waalikwa pamoja na msafara mzima wa timu ambayo tutacheza nayo mechi Jumamosi" alisema Manara.

Meneja wa Mahusiano wa SportPesa, Sabrina Msuya ambao ndio wadhamini wa wiki ya Simba aliwapongeza Simba kwa mapinduzi makubwa ambayo wanaonesha katika soka.

Sabrina alisema katika wiki hii ya Simba yatakuwa na promosheni kwa washindi kupata tiketi ya mechi pamoja na kugawa jezi.

"Jumanne tutaungana na Simba kugawa vifaa vya michezo katika timu za mtaani," alisema Sabrina.

Advertisement