Simba kusuka ama kunyoa leo

Tuesday February 12 2019

 

HAKUNA kitu kingine ambacho Simba inatakiwa kufanya leo Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ila kupata ushindi dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba inavaana na Waarabu wakitoka kupoteza mchezo wao wa kwanza uliopigwa wiki iliyopita nchini Misri.

Simba ilikung’utwa mabao 5-0 ikiwa ni siku chache tu tangu wakumbane na kipigo kama hicho kutoka kwa wapinzani wao wengine wa kundi hilo, AS Vita ya DR Congo.

Vipigo hivyo ni kama vimewakatisha tamaa mashabiki wa klabu hiyo na wadau wengine wanaofuatilia soka nchini, wakiona kama nafasi ya Simba kutinga robo fainali imeyeyuka tofauti na matumaini waliyokuwa nayo awali baada ya kutinga makundi.

Licha ya Simba kupoteza michezo miwili mfululizo tena kwa idadi kubwa ya mabao, bado haina maana kama ndio imeshapoteza dira kwenye mbio zao za kufuzu kupitia kundi hilo.

Simba ina nafasi ya kusonga mbele kama itazitumia vyema mechi zake tatu zilizosalia zikiwamo mbili za nyumbani ikiwamo ya leo dhidi ya Al Ahly wanaorudiana nao kabla ya kuikaribisha AS Vita katikati ya Machi mwaka huu.

Mchezo pekee wa ugenini kwa Simba ni dhidi ya JS Saoura ya Algeria utakaoochezwa Machi 9 na baada ya hapo ndipo itarejea nyumbani kuwasubiri Wakongo.

Ni kweli kwa kuangalia msimamo na matokeo ambayo Simba imeyapata katika mechi zake tatu za awali katika michuano hiyo, iinaweza kukukatisha tamaa kwa sababu huoni itapenya vipi dhidi ya wapinzani wao waliopo juu yao, yaani vinara Al Ahly na AS Vita ambao msimu uliopita kila moja ilifika fainali za michuano ya CAF, Wamisiri wakicheza Ligi ya Mabingwa na Wakongo katika Kombe la Shirikisho japo zote zilichemsha kubeba mataji mbele ya Esperance ya Tunisia na Raja Casablanca ya Morocco.

Hata hivyo Mwanaspoti bado linaamini Simba haipaswi kushuka uwanjani leo kinyonge dhidi ya Al Ahly hata kama imetoka kupokea kichapo kizito kwa Wamisri hao.

Wachezaji, lazima watambue kuwa matokeo mazuri sio tu yatarejesha furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo na watanzania wengine wanaofuatilia soka, lakini pia itairejesha timu yao kwenye nafasi ya kuandikisha rekodi itakayokuja kudumu kwa muda mrefu na kuwapa heshima wao.

Hakuna timu ya Tanzania iliyowahi kuvuka na kucheza robo fainali au hatua nyingine za juu za michuano ya CAF tangu mifumo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kubadilishwa kwani mara zote klabu hizo wawakilishi zimekuwa zikishia makundi tena kwa aibu.

Kwa hali na rekodi hiyo ni lazima nyota wa Simba wawakabili Wamisri kama mbogo aliyejeruhiwa kwa nia ya kuhakikisha katika mchezo huo wanapata ushindi ili kufufua matumaini yao ya kusonga mbele.

Itakuwa ni aibu kwao kama watakubali Al Ahly wawafunge tena nyumbani baada ya kuwadhalilisha katika mechi ya kwanza ugenini.

Simba na mashabiki wake watambue kuwa hata kama timu yao haitasonga mbele kutoka kwenye kundi lao, lakini tayari wamepambana na kutimiza wajibu wao kwa kuivusha kwenye makundi ikiwa ni baada ya miaka mingi kupita tangu ilipocheza mara ya mwisho 2003.

Muhimu ni mashabiki kuachana kufanya kama walivyowafanyia nyota wao kwenye michuano ya SportPesa kwa kuwazoea na kuwaghasi kutokana na kuchukizwa na matokeo waliyopata kwenye michuano hiyo ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Wakenya.

Tunaamini Simba ina kikosi kizuri, ila makosa madogo yamekuwa yakiigharimu katika mechi zao zilizopita hasa kwenye safu yao ya ulinzi, kitu ambacho Mwanaspoti inaamini Kocha Patrick Aussems na vijana wake watarekebisha mapema kabla ya mchezo huo wa leo Jumanne.

Jambo la muhimu kwa wachezaji wa Simba ni kujituma na kuhakikisha inajitoa kwenye mechi zilizosalia ili kufikia makosa ya nyuma ya kuipa heshima Simba mbele ya wapinzani wao ambao rekodi zao kwa michuano ya Afrika ni za kuvutia, lakini isiwe kigezo cha kuwagwaya.

Kama Simba waliweza kuwafumua JS Saoura kwa mabao 3-0 nyumbani katika mchezo wa kwanza, ni vipi ishindwe kupata matiokeo mazuri dhidi ya wageni watakaokuja kucheza nao hapa nchini, hasa ikizingatiwa rekodi zinaonyesha Wekundu hao huwa hawafungiki kirahisi nyumbani.

Hivyo wito wetu ni kwa mashabiki wa soka wajitokeze kwa wingi uwanjani kuiunga mkono Simba ili kupa nguvu na kupata matokeo mazuri hatimaye ijiweke kwenye nafasi ya kufuzu hatua uinayofuata itakayoitajirisha klabu na kuipa heshima kubwa Tanzania kama itaweza kuvuka hatua inayofuata.

Advertisement