Simba kusheherekea ubingwa leo

Muktasari:

Simba imetwaa Ubingwa wa Ligi hiyo kwa mara ya kwanza ikiwapokonya waliokuwa mabingwa watetezi JKT Queens na sasa vita imehamia kwa timu tano zinazowania nafasi mbili za juu na kukwepa kushuka Daraja.

WAKATI Ligi Kuu ya Wanawake ikitarajia kufikia tamati leo Jumatano Agosti 13, 2020, timu tano zitakuwa katika vita mbili kali za kuwania nafasi mbili za juu pamoja na kukwepa kushuka daraja.

Simba Queens wao wametwaa ubingwa wa ligi hiyo ambapo leo baada ya mchezo wao na TSC Queens watakabidhiwa kombe lao bila kujali matokeo watakayopata.

Iko hivi, vita ya kwanza itakuwa kwa timu za TSC Queens wenye alama 12 na Tanzanite pointi 13 ambapo timu moja itapaswa kuungana na Panama Girls ambao wameshuka daraja kutokana na alama nne walizokusanya.

Tanzanite wao watakuwa na kibarua dhidi ya vibonde Panama huku TSC wakiwa na shughuli pevu dhidi ya Simba Queens mchezo utakaopigwa dimba la Nyamagana jijini Mwanza.

Vita ya pili itazikumba timu za JKT Queens, Ruvuma Queens na Alliance Girls zinazowania nafasi ya pili baada ya mchezo ya leo ili kuhitimisha ligi hiyo kwa kishindo.

Hadi sasa JKT Queens ambao wako nafasi ya pili kwa alama 49 watakuwa wageni wa Marsh Queens, huku Ruvuma Queens wenye alama 47 watakuwa na kazi dhidi ya Baobab Queens na Alliance wenye pointi 47 watakipiga na Mlandizi Queens.