Simba kupewa ‘ndoo’ ikiivaa Namungo leo

Wednesday July 8 2020

 

By Yohana Challe

Dar es Salaam. Mabingwa wa soka Tanzania, Simba watakabidhiwa kombe lao leo baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Simba imetwaa ubingwa huo ikiwa ni mara ya tatu mfululizo baada ya kufikisha pointi 80 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine 19 zinazoshiriki ligi hiyo.

Kwa ubingwa huo Simba itapokea Sh80 milioni za ubingwa na zawadi nyingine kutoka kwa wadhamini wakiwamo SportPesa ambao wiki iliyopita waliipa Sh100 milioni.

Mechi ya leo haitarajiwi kuwa ya mteremko kwani Simba itahitaji kupokea kombe kwa heshima ya ushindi tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambako ilipokea kombe kinyonge baada ya kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa mbele ya Rais John Magufuli.

Lakini kwa Namungo hiyo itakuwa mechi muhimu ya kupambana kushika nafasi mbili za juu kwani ikishinda itakuwa imefikisha pointi 62, sawa na Azam ambayo nayo itakuwa ikimenyana na Mwadui kwenye Uwanja wa Chamazi Complex.

Kabla ya mechi ya leo, timu hiyo ambayo hii ni mara yake ya kwanza kucheza Ligi Kuu, inashika nafasi ya tano ikizidiwa na Yanga kwa pointi mbili baada ya zote kucheza mechi 33.

Advertisement

Simba inaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa imepoteza mechi tatu tu za Ligi Kuu. Ililala 1-0 mbele ya Mwadui FC, ikapoteza tena kwa JKT Tanzania kwa kuchapwa 1-0 na ikafungwa 1-0 na Yanga kwa bao la Bernard Morrison.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Simba ilipokutana na Namungo, Januari 29, mabingwa hao waliibuka na ushindi wa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa yaliyofungwa na Francis Kahata, Hassain Dillunga na Meddie Kagere wakati yale ya Namungo FC yakifungwa na Bigirimana Balise na Lucas Kikoti.

Simba inaingia kwenye Uwanja wa Majaliwa kwa mara ya pili baada ya Agosti 11, 2018 kucheza na wenyeji hao na kutoa suluhu.

Mechi nyingine za leo

Katika michezo mingine leo, Mbeya City inayopambana kukwepa janga la kushuka daraja itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine kuchuana na Polisi Tanzania.

Biashara United baada ya kuilazimisha Yanga kutofungana katika mechi iliyopita, inachuana na Ruvu Shooting.

KMC ambayo inachungulia shimo la kuelekea Daraja la Kwanza, itakaribisha Singida United ambayo imekwisha shuka kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mbao FC ambayo tangu ilipomchukua kocha Fred Felix Minziro imekuwa na mwendelezo mzuri kwa kushinda mechi tatu mfululizo, itakuwa nyumbani ikicheza na Mtibwa Sugar.

Ndanda FC ambayo iliibana Simba na kutoka nayo suluhu katika mechi iliyopita itapambana na JKT Tanzania na Azam baada ya kuinyuka Singida United mabao 7-0 itakuwa tena nyumbani kucheza na Mwadui FC.

Kesho, Tanzania Prisons atacheza na Coastal Union wakati Alliance FC na Lipuli FC ambazo zote zipo katika hali tete zikichuana kuwania alama tatu.

 

Advertisement