Simba kujipima nguvu na African Lyon

Muktasari:

Simba imekuwa na kawaida ya kucheza mechi za kirafiki hata katikati ya Ligi kwaajili ya kuwapa utimamu wa mwili wachezaji wake ambao hawajacheza mechi za Ligi.

KLABU ya Simba kesho itakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya klabu ya African Lyon katika uwanja wa Chamazi Complex sa 10:00 jioni ikiwa ni sehemu ya kupasha misuli kwa wachezaji wa timu zote.

Licha ya Simba jana usiku kucheza mchezo wa Ligi Kuu na Biashara Utd na kupata ushindi wa mabao 4-0, kocha Sven Vandenbroeck ameona wapate mechi nyingine kabla ya kukutana na Gwambina kwenye Ligi Kuu, Jumamosi katika uwanja wa Benjamini Mkapa.

Kocha Sven amekuwa na kawaida ya kutumia wachezaji wake wa kikosi cha pili ambao wanakuwa hawajapata nafasi ya kucheza katika mchezo wa Ligi kucheza mechi za kirafiki ili wachezaji wake wote kuwa na utimamu wa mwili (Match Fitness).

Kupitia katika ukurasa wa Instagram ya Simba ulieleza"Kwa burudani ya jana ilivyokuwa nzuri tumeona ni vyema na kesho wanasimba tuipate tena, Simba wawili tunakutana,sisi wakubwa (Simba Sc) na Simba wadogo (African Lyon)" ilieleza taarifa hiyo.

Tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa kesho asubuhi Mbagala Rangi tatu na katika uwanja wa Azam Complex.