Simba katikati ya mtego mkali

Muktasari:

  • Timu zinazotumia viwanja hivyo KMC, Yanga, Simba na African Lyon zinaweza kujikuta zikipoteza fungu kubwa la fedha zitokanazo na viingilio kwani zitalazimika kuhamia kwenye viwanja ambavyo haviingizi idadi kubwa ya mashabiki kulinganisha na Uhuru na ule wa Taifa.

SIMBA imeanza kula viporo vyao kwa mbwembwe, lakini tamko na amri iliyotolewa na serikali hivi karibuni huenda ikatibua hesabu zao za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu iwapo tu itashindwa kuchanga vyema karata zao.

Kikwazo kipya kimeibuka katika mbio za Simba kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu baada ya serikali kutangaza uamuzi wa kuufunga Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa siku 30 kabla ya Fainali za Afrika kwa Vijana U17 zitakazofanyika kuanzia Aprili 14 hadi 28.

Uwanja huo pamoja na ule wa Uhuru, vitafungwa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati ili viweze kuwa na hadhi ya kutumika kwa mashindano hayo ya Afrika yatakayoshirikisha nchi nane ambazo ni wenyeji Tanzania, Uganda, Angola, Nigeria, Senegal, Guinea, Cameroon na Morocco.

“Tumepanga katika kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa mashindano ya Afrika kwa vijana, tutaufunga Uwanja wa Taifa kwa ajili ya marekebisho ya eneo la kuchezea ili mashindano yatakapoanza, uwe katika hadhi na ubora wa hali ya juu,” alisema Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Ingawa Waziri Mwakyembe hakuutaja ule wa Uhuru, taarifa ambazo gazeti hili limezinasa ni kuwa hadi ule wa Uhuru ulio jirani wa Taifa pia utafungwa kwa ajili ya ukarabati huo.

Kauli ya Mwakyembe inamaanisha, mechi zote za Ligi Kuu zilizopangwa kuchezwa viwanjani hapo katika kipindi hicho, zitalazimika kupangiwa viwanja vingine ili kutoathiri ratiba ya ligi.

Uamuzi huo wa kufunga Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru kwa siku 30, huenda ukaziathiri timu zinazoutumia hasa Simba kulingana na ratiba ya ligi ilivyo.

Timu zinazotumia viwanja hivyo KMC, Yanga, Simba na African Lyon zinaweza kujikuta zikipoteza fungu kubwa la fedha zitokanazo na viingilio kwani zitalazimika kuhamia kwenye viwanja ambavyo haviingizi idadi kubwa ya mashabiki kulinganisha na Uhuru na ule wa Taifa.

Lakini mbali na hilo la mapato, uamuzi huo huenda ukaiathiri zaidi Simba katika vita ya ubingwa kulinganisha na watani wao wa jadi, Yanga kwani katika kipindi hicho wana idadi kubwa ya mechi kama ratiba ya ligi inavyoonyesha.

Wakati Yanga wakiwa na mechi mbili tu wanazopaswa kucheza kwenye Uwanja wa Taifa ndani ya kipindi ambacho utapokuwa umefungwa, Simba kwenye muda huo watakuwa na mechi tano.

Timu hizo mbili kongwe huenda zikalazimishwa kuchagua viwanja vingine kwa ajili ya michezo hiyo katika kipindi hicho ambacho watakuwa wanapisha ukarabati kuelekea fainali za Afrika kwa vijana.

Ikiwa zitatumia Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Yanga na Simba zinaweza kujikuta zinapata changamoto ya kutouzoea uwanja wa nyasi bandia tofauti na ule wa Taifa ambao una nyasi za asili.

Lakini pia iwapo watachagua vile vya nje ya Dar es Salaam, changamoto ya ubovu wa eneo la kuchezea inaweza kuharibu mipango yao. Takwimu zinaonyesha Simba msimu huu wamekuwa wakifanya vizuri Taifa, katika mechi 10, wametoka sare mbili na kupata ushindi mara nane.

Hata hivyo, Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu, Boniface Wambura aliliambia gazeti hili kuwa bado hawajajulishwa rasmi juu.

Tulisikia hilo na tukafuatilia lakini hadi sasa hatujapokea barua kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupitia kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hata hivyo wenye mashindano ni CAF na ndio wanapanga ukarabati uanze lini na uishe lini. Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika likitoa taarifa rasmi za kufungwa kwa viwanja, tutaangalia nini cha kufanya,” alisema Wambura. Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema hawajapewa taarifa.