Simba itapenya hivi kwa Songo

Tuesday July 23 2019

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Umakini na ubora wa washambuliaji wa Simba katika kutumia nafasi inaweza kuwa silaha ya kuibuka na ushindi dhidi ya UD Songo ya Msumbiji.

Simba itaanzia ugenini kati ya Agosti 9 na 11 kabla ya kurudiana Dar es Salaam kati ya Agosti 25 na 28 katika mchezo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

UD Songo imeonekana kutokuwa na safu imara ya ulinzi miaka ya hivi karibuni, jambo ambalo linaweza kuibeba Simba.

Matokeo ya mechi 10 za mwisho za kimataifa na Ligi ya Msumbiji, yanatoa ishara iwapo safu ya ushambuliaji ya Simba itajipanga vyema, UD Songo haitakuwa kikwazo kwao kupata ushindi.

Katika mechi 10 za mwisho ilizocheza katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, UD Songo imefungwa mara 16 katika mechi hizo iwe nyumbani au ugenini. UD Songo imefunga mabao 10 ikiwa ni wastani wa bao moja katika kila mchezo na imeibuka na ushindi mara moja, imetoka sare tatu na kupoteza michezo sita.

Katika idadi ya mechi 10 za kimataifa ilizocheza hivi karibuni, tano kati ya hizo ilikuwa uwanja wa nyumbani ambako Simba itaanzia kucheza dhidi ya timu hiyo na kwenye idadi hiyo ya michezo, iliibuka na ushindi mara moja, ilipata sare mbili na kupoteza mara mbili, jambo linaloashiria ni timu inayoweza kufungika hata ikiwa nyumbani.

Advertisement

Katika Ligi ya Msumbiji msimu huu, UD Songo ilicheza jumla ya michezo 12, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10, imepata mabao 14. Timu hiyo imeshinda mechi sita, imetoka sare mara tatu na kupoteza mechi tatu.

Pamoja na kasoro hizo, Simba inapaswa kuingia na tahadhari dhidi ya UD Songo kwani timu hiyo mwaka 2018 nusura iwatupe nje vigogo vya soka Afrika, TP Mazembe ya DR Congo katika mashindano ya hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa kwanza ambao ilicheza ugenini, UD Songo ilichapwa mabao 4-0 lakini katika mechi ya marudiano nyumbani, iliichapa TP Mazembe mabao 3-0.

Hata hivyo, Simba inatakiwa kufanyia kazi udhaifu kwenye safu ya ulinzi hasa inapokuwa ugenini ambako haijapata ushindi katika mechi sita mfululizo katika mashindano ya kimataifa.

Katika mechi 10 za kimataifa za mwisho ilizocheza imefungwa mara 20 na yenyewe ikifunga mabao 11 tu. Hata hivyo, Simba imeibuka na ushindi mara nne, kutoka sare moja na kupoteza tano.

Mafanikio makubwa ya UD Songo ilipata mwaka 2018 ilipotinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikimaliza nafasi ya tatu kwa pointi tatu.

Nyota tegemeo ni mshambuliaji Helder Pelembe na kipa Leonel ambaye ni chaguo la kwanza la timu ya taifa ya Msumbiji.

Advertisement