Simba inawasha mitambo rasmi leo

Wednesday August 8 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN NA CHARLES ABEL

SIMBA ilitesti mitambo yake katika mechi ya SportPesa iliyofanyija Nakuru, Kenya. Kikosi kikafika fainali na kupoteza kwa Gor Mahia kwa mabao 2-0. Kuna watu wakacheka sana. Ikaja michuano ya Kombe la Kagame, wakaitesti tena mitambo yao kuona imekaaje. Kama zali wakafika fainali na kupoteza kwa Azam. Baada ya hapo mabosi wao wakaisafirisha timu masafar marefu hadi Ulaya na kuweka kambi nchini Uturuki. Kule wakajifua vya kutosha na leo Jumatano, Wekundu hao wataiwasha rasmi mitambo yao kwenye Uwanja wa Taifa.
Vijana hao wa Kocha Patrick Aussems itashusha nyota wake wote wa msimu uliopita wakiongozwa na Emmanuel Okwi hadi wapya chini ya Meddie Kagere.
Simba itatambulisha kikosi chake kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara 2018-2019 mapema tu uwanjani hapo kabla ya kuvaana na Asante Kotoko kutoka Ghana ambao mashabiki wa Msimbazi wanamini ndio kipimo kizuri kwa timu yao.
Baada ya mechi hiyo ya kuhitimisha Tamasha la Simba Day ikiwa ni msimu wake wa 10, Simba itajichimbia kambini kabla ya kuelekea Mwanza kuivaa Mtibwa Sugar katika mechi ya Ngao ya Hisani kujiweka tayari kuanza Ligi Kuu Bara.
Kocha Patrick Aussems ameweka wazi wachezaji wote wa Simba amewaona na amefurahishwa na viwango vyao na anaamini mashabiki watakaofika Taifa watashuhudia kile walichokifanya Uturuki.
Aussems alisema mipango yako ya kwanza kutafuta nyota 18 watakaokuwa fiti kuliko wengine katika kila nafasi atawapa kipaumbele cha kuwatumia katika mechi nyingi.
Mbelgiji huyo alisisitiza falsafa zake ni kushambulia kwa haraka na wakipoteza ni kukaba kuanzia mbele jambo ambalo mchezaji ambaye atakuwa hayupo fiti asilimia mia atashindwa kuwa chaguo lake la kwanza.
Alisema anaamini vijana wake wameiva na tayari kuwapa burudani mashabiki wa Simba wenye kiu ya kutaka kuiona baada ya kutoka kambini nchini Uturuki.
"Upana wa kikosi na wachezaji hainiumizi kichwa kwangu kwani huwa napenda ushindani na nimekuwa nikifanya hivyo katika timu zote nilizofundisha hivyo kila kitu naamini kitakuwa sawa," alisema.
"Timu niliyokuwa naipanga Uturuki hakuna kikosi cha kwanza, nilikuwa nawajaribu na katika mfumo wangu. Lakini naamini sasa ndio kazi inaanza," alisema Aussems.
"Mastraika, viungo, mabeki na makipa ambao wote niliokuwa nao sasa nina nafasi ya kuwatumia, ilai ambao watafanya au kuwa vile ambavyo Mimi nataka kwani watakuwa wakicheza katika malengo na falsafa zangu.
"Nafahamu kuwa na makipa watano lakini hawa watatu ambao nilikuwa nao katika kambi nchini Uturuki ndio nitawatumia msimu huu labda itokee sababu nyingine maalumu," aliongezea Aussems.
Kocha huyo alifichua kuwa, nahodha John Bocco atakosekana katika mechi ya leo dhidi ya Asante Kotoko kwa vile ni majeruhi ingawa atakuwa miongoni mwa nyota watakaotambulishwa pale Taifa.
"Bocco atakosekana katika mechi hii nimeona vyema kumpumzisha ili apate matibabu zaidi na kupona haraka, " alisema.
"Wachezaji wote wana nafasi ya kutumika katika mechi ya leo kwani nauchukulia kama mechi ya kirafiki na sitajali matokeo hivyo naomba mashabiki wa Simba wajitokeze kwa wingi kushuhudia timu yao," alisema Aussems.
Simba mbali na nyota wake wa msimu uliopita, itatambulisha wachezaji msimu huu ni saba, Deo Munishi, Pascal Wawa, Cletus Chama, Adama Salamba, Marcel Kaheza, Mohammed Rashid na Meddie Kagere.  
Naye Kocha Mkuu wa Asante Kotoko, Fabian Samuel akiizungumzia mechi hjiyo alisema "Nimeiona Simba katika runinga ni timu kubwa Afrika na wanacheza vizuri lakini tumejipanga kushindana nao na kupata ushindi katika mechi hii ndio maana tumekuja na kikosi chetu kamili."
Tamasha hilo litaanza saa 5 asubuhi, japo milango itakuwa wazi tangu saa 4 ili kyutoa fursa kwa mashabiki na wapenzi wa Simba kupata burudani mbalimbali za wasanii nyota wa muziki wa waigizaji kabla ya utambulisho na baadaye mechi.
Utambulisho huo ufanyika mara baada ya mechi ya Simba B dhidi ya Dodoma FC ya Kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadaye ndipo Simba na Asante Kotoko kuliamsha dude kuanzia saa 10 jioni.

Advertisement