Simba imenoga hatarii!

KWA mara ya kwanza msimu huu kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alianza na mastraika wawili katika kikosi cha kwanza dhidi ya JKT Tanzania ambao ni Meddie Kagere na Chris Mugalu.

Ndani ya dakika sita za mwanzo Simba walikuwa wanaongoza mabao mawili ambayo yalikuwa yamefungwa na Kagere na Mugalu.

Tathmini ya mechi tano za awali inaonyesha kwamba Joash Onyango ndiye mwenye uhakika wa kuanza miongoni mwa wachezaji saba wapya waliosajiliwa na Simba msimu huu wakati Larry Bwalya, Bernard Morrison na Mugalu wote wanapewa dakika chache.

Kwa mujibu wa wachambuzi, ingekuwa nadra kwa Bwalya, Morrison na Mugalu kuwekwa nje katika timu nyingine za hapa nchini kama ambavyo wanafanya mabingwa hao.

Kikosi hicho cha Simba sehemu nyingine ambayo imeimarika ni uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja kama ambavyo amekuwa akionyesha Clatous Chama, Bwalya, Luis Jose ambaye alifunga bao la kideoni dhidi ya JKT Tanzania.

Kocha wa wakilishi hao wa taifa kwenye Ligi ya Mabingwa, amekuwa na uwanja mpana wa kuchagua wachezaji watakaoanza katika kikosi cha kwanza na wale ambao watakuwa benchi.

Simba msimu huu wanaweza kuwakosa wachezaji kama John Bocco, Francis Kahata, Ibrahim Ajibu katika kikosi na ikashinda kwa idadi kubwa ya mabao.

Uwezo wa Ajibu, Hassan Dilunga, Said Ndemla na wengineo ambao wanaonekana wachezaji wa kawaida katika kikosi cha Simba kwenye timu nyingine wangeweza kuwa wachezaji wa kutegemewa katika kikosi cha kwanza.

Sven kulingana na ubora wa wachezaji aliokuwa nao anaweza kutumia mfumo wa 4-3-3 kama ambavyo alianza na JKT Tanzania na 4-4-2 au 3-5-2.

Mastraika wanne wa Simba, Bocco, Kagere, Mugalu na Charles Ilanfia wameongeza makali na ushindani katika kikosi hicho msimu huu kutokana na uwezo wao wa kufunga walioonyesha mpaka sasa.

Ubora wa mastraika hao ndio umeimarisha kikosi cha Simba kwani Kagere katika mechi tano za ligi amefunga mabao manne, Mugalu katika mechi 5 (zikiwamo za kirafiki) amefunga mabao matano.

Wakati Bocco katika mechi zake za ligi msimu huu alizocheza amefunga mabao mawili kama ilivyo kwa Ilanfia aliyefunga mawili katika michezo miwili.

Eneo jingine ambalo Simba wameonyesha kuwa wapo vizuri msimu huu ni katika masuala ya pesa, kwa mfano walikuwa wanaenda Dodoma kucheza na JKT Tanzania lakini hawakufika huko moja kwa moja walilala Morogoro.

Wachezaji na benchi la ufundi Simba ni ngumu kusikia wakilalamika katika masuala ya pesa kwani mambo yao yamekuwa yakinoga jambo linaloongezaka morali kikosini .

KOCHA SVEN

Kocha wa Simba, Sven alisema kati ya maeneo ambayo timu yake imeimarika ni hali ya ushindani kutokana na kila mchezaji kuonyesha uwezo wake ili kupata nafasi ya kucheza.

“Kuna wakati mpaka naumiza kichwa kuchagua wachezaji 18 wa kwenda kuwakilisha wenzao kwani wote waliokuwa ndani ya kikosi ni bora kutokana na viwango wanavyoonyesha mazoezini,” alisema.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema uimara wa kwanza ambao timu yake ya zamani umeonekana ni kwa kipa Aishi Manula ambaye msimu uliopita alikuwa ana makosa mengi.

Alisema: “Tangu miaka 25 iliyopita Simba lazima iwe na kipa mwenye uwezo, beki wa kati mwenye akili kama safu ya kiungo ilivyo na watu wa kuzalisha mabao ambayo yatakwenda kuwakuta mastraika wenye uwezo wa kufunga.

“Ukiangalia Simba ya sasa hivyo vyote vinapatikana na sioni kama watakuwa na ugumu katika mashindano ya ndani watafanya vizuri, ila wasi wasi wangu wataweza kuwa bora hivyo kimataifa.”