Simba ilizidiwa hapa tu

REKODI ya Simba ya kucheza kwa siku 98 bila kupoteza mchezo wowote kwenye mechi za mashindano imetibuliwa na maafande wa Tanzania Prisons. Kipigo cha bao 1-0 ambacho Simba imekipata kutoka kwa Prisons juzi mkoani Rukwa kimedhihirisha kuwa bado timu hiyo haipaswi kujivuna kuwa ina kikosi kipana kuliko nyingine hapa nchini kama ambavyo imekuwa ikifanya. Mara ya mwisho kwa Simba kufungwa katika mechi za mashindano ilikuwa dhidi ya Mbao FC katika ligi ya msimu uliopita. Baada ya hapo ilicheza mechi 10 zikiwamo mbili za Kombe la ASFC na Ngao ya Jamii pamoja na nane za Ligi Kuu bila kupoteza, lakini Prisons wakawatibulia juzi.

Kiwango kisichoridhisha cha idadi kubwa ya wachezaji wake ambao baadhi sio wa kikosi cha kwanza, kilidhihirisha kuwa bado Simba ina kazi kubwa ya kufanya ili kuthibitisha kuwa ina kikosi kipana.

Kukosekana kwa wachezaji sita tegemeo wa timu hiyo kulionekana kuwa na faida kubwa kwa Prisons ambayo wachezaji wake walionekana kucheza kwa uhuru na bila presha kubwa na kufanikiwa kuidhibiti Simba ambayo imekuwa ikitajwa kama timu tishio kwa sasa nchini.

Pengo la kuwakosa Gerson Fraga, Clatous Chama, Meddie Kagere, Chris Mugalu, John Bocco na Pascal Wawa lilionekana kutokana na makosa ya mara kwa mara yaliyofanywa na wachezaji wanaocheza nafasi zao na kuwapa mwanya Prisons kuwadhibiti kimbinu na kufanikiwa kuibuka na ushindi huo muhimu uliowafanya wafikishe jumla ya pointi tisa.

Prisons walionekana kujilinda vyema, wakishambulia kwa kushtukiza hasa kwa kutumia mbinu ya kupiga mipira mirefu na krosi za juu ambazo zilionekana kuisumbua safu ya ulinzi ya Simba.

Kiwango bora cha wachezaji Jumanne Elfadhil, Ezekiel Mwashilindi na Salum Kimenya ambao walicheza katika safu ya kiungo ya Prisons, kilitoa mchango mkubwa katika ushindi wa timu hiyo juzi.

Viungo hao waliziba vyema mianya na kuinyima fursa Simba kutengeneza nafasi kuingia katika eneo lao lakini pia waliweza kutengeneza balansi ya kitimu katika dakika 90 za mchezo huo.

Kiujumla ilikuwa ni siku nzuri kwa Prisons na kinyume chake ndio ilikuwa kwa Simba na ifuatayo ni mchezaji mmoja mmoja walivyojitoa.