Simba ilijiamini, Azam ikaliamsha

Muktasari:

  • Mwanaspoti iliyopiga kambi visiwani humo tangu mwanzo wa mashindano hayo hadi mwisho ilipopigwa fainali kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba linakuletea mambo kadhaa kutoka Kombe la Mapinduzi 2019.

MSIMU wa 13 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi ilimalizika wikiendi iliyopita kwa Azam kutetea taji kwa mara ya tatu mfululizo na kulibeba jumla, huku kukiwa na rekodi kadhaa zilizowekwa kwenye michuano hiyo ya mwaka 2019.

Michuano hii iliasisiwa rasmi mwaka 2007 na msimu huu ilishirikisha klabu tisa, tatu kutoka Bara na sita za Zanzibar zilizogawanywa kwa nne za Unguja na mbili za Pemba.

Wawakilishi wa Tanzania Bara ni Azam, Simba na Yanga, huku Unguja zilikuwa KMKM, Malindi, KVZ na Mlandege, huku Chipukizi na Jamhuri kutoka Pemba.

Katika mashindano hayo Simba na Yanga hazikukutana kama ilivyokuwa ikitarajiwa kwa kuwa hazikupangwa kundi moja, lakini Yanga iliyopeleka kikosi cha pili na vijana iling’olewa mapema kama kuwakacha watani zao waliofuika fainali.

Mwanaspoti iliyopiga kambi visiwani humo tangu mwanzo wa mashindano hayo hadi mwisho ilipopigwa fainali kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba linakuletea mambo kadhaa kutoka Kombe la Mapinduzi 2019.

KILICHOANGUSHA BARA NA VISIWANI

Karibu timu zote zilizoshiriki zilikuwa na lengo la kutwaa ubingwa na hata hao Simba waliodai waliyatumia mashindano hayo kwa lengo la kujiandaa na mechi zao za kimataifa, lakini pia walikuwa wakiuota ubingwa wa michuano hiyo.

Simba iliyobeba taji hilo mara tatu, ilitamani kutwaa mara ya nne ili angalau kulingana na Azam ndio maana wakakomaa hadi fainali, japo walichemka pale Gombani mbele ya Jeshi la Hans Pluijm.

Kocha Patrick Aussems alikupeleka kikosi chake chote na kuweka wazi kutumia mashindano hayo kukiandaa kikosi kwa mechi ya Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya JS Sauora, ambapo walishinda bao 3-0 nyumbani.

Ni kweli lengo lake lilitimia kwani kwenye mashindano hayo aliwatuma nyota wake wote kucheza mechi za makundi na walionyesha kiwango kizuri na kutinga hatua ya nusu fainali kisha kuwaacha baadhi ya nyota wake ambao, hawakuwa kwenye mipango yake ya mechi ya kimataifa.

Aussems aliamua kuongeza nguvu kikosi hicho kwa kuwaleta wachezaji kutoka timu yake ya vijana chini ya kocha Nico Kiondo na walipoingia fainali aliwaongeza nyota wengine kama Shiza Kichuya, Haruna Niyonzima na Rashid Juma.

Hata hivyo, maelekezo yote ya mechi ya nusu fainali na fainali yalitokana na Aussems akishirikiana na Kiondo na lengo lilikuwa ubingwa huo.

Katika mechi zote za makundi ukiachana na mastaa waliocheza baadhi ya mechi kama Meddie Kagere aliyefunga bao mbili katika mechi moja pekee aliyocheza hadi kuondoka kwake, ila wachezaji kama Clatous Chama, Rashid Juma, Nicolaus Gyan walionyesha kiwango bora.

Simba mechi zote ilicheza kwa kujiamini na kuwa na uhakika wa kufanya vizuri zaidi, lakini siku ya fainali walikosa kucheza kwa kujiamini na kujikuta wakipigwa 2-1 na huenda presha ya mchezo pia ilichangia kwani wengi walikuwa ni vijana wa kikosi B.

YANGA

Yanga kwa asilimia kubwa kikosi chao kilikuwa vijana na wazoefu wachache japo waliondolewa hatua ya makundi. Kitu pekee kilichoonekana kwa Yanga ni wachezaji wengi kukosa uzoefu huku wale yao walishindwa kujituma zaidi.

Nyota wazoefu ndani ya Yanga waliongozwa na Deus Kaseke, Matheo Anthony, Said Juma ‘Makapu’ pamoja na Haji Mwinyi Mngwali.

AZAM FC

Hawa ndio mabingwa, tena mabingwa hasa kwani wamebeba kombe hilo jumla, mechi zao nyingi hasa za makundi walicheza chini ya kiwango, mpira haujifichi na ni mchezo wa wazi.

Ni wachezaji wachache ambao walijituma ukiachana na asilimia kubwa ya wale waliocheza chini ya kiwango.

Ilidaiwa, timu hiyo ilikuwa na zaidi ya nyota watatu majeruhi ila walichezeshwa hivyo hivyo akiwemo Tafadzwa Kutinyu raia wa Zimbabwe.

Nyota wa kigeni ndani ya Azam walipambana kwa kadri ya uwezo wao, lakini kama wachezaji wachache ndiyo hujituma timu haiwezi kupata matokeo mazuri ndicho kilichokuwa kinatokea kwa Azam.

Azam ilitinga fainali, ilicheza kwa kujituma na kama wangecheza hivyo tangu mwanzo basi ingekuwa inapata ushindi mnono wa mabao mengi.

Azam ilizinduka mwishoni ambapo mashabiki ndio walianza kuuona uwepo wa kila mmoja uwanjani, alionyesha nia na uchu wa kutetea ubingwa. Kati ya mechi zote walizocheza uhai ulianza kuonekana hatua ya nusu fainali.

KMKM, MLANDEGE, MALINDI

Hizi timu za Unguja ndizo angalau zilizoonyesha ushindani na kuwa na mashabiki kiasi. Lakini haikufanya vizuri, japo KMKM ndio pekee iliyofika nusu fainali na kuondolewa na Azam FC. Timu za Pemba, Jamhuri na Chipukizi hizi ziliondolewa hatua ya makundi. Tatizo kubwa kwa timu zote hizo ilielezwa ni wachezaji kukosa uzoefu wa mashindano makubwa kama ilivyo kwa Simba, Yanga na Azam.

MVUTO MDOGO

Mashindano ya msimu huu hayakuwa na mvuto, hayakusisimua wala hayakuwa na upinzani pengine kwa kitendo cha Yanga kutotuma mziki kamili uliokuwa unasubiriwa visiwani.

Pia, ilizoeleka kwa miaka nyuma kualikwa kwa timu za kigeni kutoka nchi za Afrika Mashariki kama Kenya na Uganda, lakini safari hii haikuwa hivyo na kupoteza ladha.

Mashindano yaliyopita kulikuwa na zawadi kwa mchezaji bora wa kila mechi lakini sasa ni Haruna Niyonzima pekee aliyepata zawadi ya mpira kwa kuwa mchezaji bora wa mechi moja ya makundi.

Maboresho yanapaswa kufanyika kwani mashindano haya ni muhimu. Waandaaji waongeze timu, mgawanyo wa pesa hata kama hautalingana na timu kama Simba, Yanga na Azam basi angalau timu zingine zinazotoka visiwani humo waboreshewe kwa kiasi fulani kutoka Sh 800,000 angalau hata Sh 2 milioni ikiwa ni nusu ya wanachopata Simba, Yanga.

Kilichoboreshwa kwa msimu huu ni zawadi ambapo awali bingwa alichukuwa Sh 10 milioni na sasa alikabidhiwa Sh 15 milioni huku mshindi wa pili akipewa Sh 10 milioni.

WALIOFUNIKA

Obrey Chirwa aliyefunga mabao matano katika mashindano hayo na Enock Atta wote wa Azam FC walitisha kama ilivyokuwa kwa Rashid Juma, Haruna Niyonzima, Meddie Kagere wa Simba, Gustafa Simon na Shaaban Mohammed wa Yanga.

Pia, kuna Abdulswamadu Ali ya Malindi hasa kwa kasi yake ya kufunga kwani, kama michuano ingeendelea huenda angetisha, huku mchezaji aliyekuwa gumzo ni kipa wa Yanga, Ibrahim Hamid kwa namna alivyokuwa akifungwa mabao ya kizembe. Hata hivyo, kipa huyo ndio anakaa langoni ikiwa ni mara ya kwanza tangu asajiliwe kutoka timu ya mpira ya ufulkweni.