Simba hii mbona kazi itakuwepo

Muktasari:

Makala haya yanakuletea maeneo mbalimbali ambayo huenda katika kikosi hicho kukawa na ushindani ili kuweza kufikia yale mafanikio ya msimu uliopita katika mashindano yote ambayo walishiriki lakini hata yale ambayo walishindwa kufanya vizuri.

MSIMU huu Ligi Kuu Bara itakuwa na ushindani wa aina yake kwani timu nyingi zimeonekana kufanya usajili wa maana katika vikosi vyao kwa kuongeza nyota wapya kutokana na mapungufu waliyokuwa nayo, pia waliachana na wale ambao walionekana kushindwa kufanya vizuri.

Simba iliachana na nyota wake saba wa kigeni huku kuna wengine haikutarajiwa kuachwa kama kiungo fundi Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, James Kotei kutokana na viwango vyao walivyoonyesha, huku pia ikiwaacha Asante Kwasi, Nicholas Gyan, Juuko Murshid na Zana Coulibaly.

Makala haya yanakuletea maeneo mbalimbali ambayo huenda katika kikosi hicho kukawa na ushindani ili kuweza kufikia yale mafanikio ya msimu uliopita katika mashindano yote ambayo walishiriki lakini hata yale ambayo walishindwa kufanya vizuri.

USAJILI

Kabla ya kuanza kwa msimu huu, Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara ni miongoni mwa timu zilizofanya usajili wa maana na walisajili nyota wapya 12, ili kuongeza nguvu katika kikosi chao kulingana na mapungufu ambayo waliyaona msimu uliopita.

Wachezaji wapya ambao walisajiliwa msimu huu kwa upande wa wazawa ni Benno Kakolanya, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Miraji Athumani na Ibrahim Ajibu wakati wa kigeni wakiwa Tairone Zagueiro, Gerson Fraga, Wilker da Silva, Sharafeldin Shiboub, Deo Kanda na Francis Kahata.

Simba baada ya kufanya usajili huo wanaonekana kuwa na kikosi kipana ambacho kinasubiriwa na mashabiki wengi wa soka hapa nchini kuona wanatetea ubingwa wa ligi, kufika mbali katika mashindano ya kimataifa zaidi ya msimu uliopita na hata kuwa bora kwenye mashindano ambayo walishindwa kufanya vizuri kama Kombe la Shirikisho (FA), walipoondolewa kwenye hatua ya awali.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori anasema walifanya usajili kwa kuzingatia mahitaji ya benchi la ufundi kutokana na ripoti yao ilivyokuwa inataka wachezaji wa aina gani kutokana na kile ambacho msimu uliopita walikuwa wanakosa.

“Kwetu uongozi tumefanya kila ambalo benchi la ufundi lilikuwa linataka kutokana na wachezaji ambao wanawahitaji tukiamini tumefanya usajili bora ambao utakuja kuzaa matunda na tukawa na msimu bora kuliko uliomalizika katika mashindano yote,” anasema Magori.

KAMBI

Baada ya kufanya usajili wa nguvu, Simba katika kuhakikisha wanapata mazingira sahihi ya kwenda kufanya maandalizi ya msimu, walikwenda Afrika Kusini kuweka kambi na walifanya mazoezi huko kwa muda wa wiki mbili ya mbinu na yale ya nguvu.

Msimu uliopita Simba ilikwenda kuweka kambi Uturuki, lakini walishindwa kufanya baadhi ya mazoezi ambayo walipanga kutokana na mazingira na hali ya hewa na kulikuwa na mvua kubwa katika nyakati tofauti.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems anasema sehemu ambayo walikwenda kuweka kambi msimu huu ni bora kuliko msimu uliopita kwani walipata kila kitu ambacho walikuwa wanahitaji kwa wakati na waliweza kutumia ili kufikia malengo ambayo walijipangia.

“Kambi ya mwaka jana tulikuwa tunakosa baadhi ya mahitaji ya msingi na hata tulishindwa kucheza mechi za kirafiki na kufanya mazoezi kutokana na hali ya hewa, mvua ilinyesha tena kubwa kwa nyakati tofauti lakini msimu huu tumefanikiwa kufanya kila ambalo tulikuwa tunahitaji,” anasema.

WABRAZILI

Msimu huu Simba imeongezwa nguvu kwa kusajiliwa Wabrazili watatu Wilker ambaye kwa sasa ni majeruhi, Fraga na Zaguiero ambao wote wapo kwenye kikosi na walicheza mechi na Power Dynamos siku ya Simba Day.

Kabla ya kwenda katika kambi ya maandalizi Kocha Aussems, aliliambia Mwanaspoti anataka muda zaidi wa kuwaona Wabrazili hao kutokana na aina ya uchezaji wao walikotoka ambao ni tofauti na la hapa Afrika hasa Tanzania.

Aussems anasema amepata muda wa kuwaona baada ya kambi kumalizika na amefahamu zaidi namna gani ya kuweza kuwatumia kulingana na mechi ambazo wanakwenda kukutana nazo msimu huu katika mashindano yote ili kuhakikisha wanafikia malengo ya timu.

“Wabrazili wote ni wachezaji wazuri ndio maana unawaona hapa na hata kucheza baadhi ya mechi za kirafiki jambo ambalo limenipa mwanga kuweza kuwatumia katika mechi za kimashindano ambazo muda si mrefu tunaanza,” anasema Aussems.

WANATAZAMWA

Simba imeongeza nyota wapya 12, ambao kati ya hao kuna wachezaji wanatazamwa watakwenda kuibeba timu msimu huu kulingana na viwango vyao ambavyo wamekuwa wakionyesha huko walipotoka kabla ya kujiunga na mabingwa hao watetezi wa ligi.

Baadhi ya nyota wapya ambao wanatazamwa ni Ajibu na Kakolanya ambao wamesajiwa wakitokea Yanga, wengine Kahata, Kanda, Shiboub na Wabrazili wote watatu kwani katika Ligi Kuu Bara rekodi zinaonyesha hakuna mchezaji Mbrazili aliyeweza kung’ara.

Sio waliosajiliwa tu, hata wale waliokuwa na timu msimu uliopita kama Meddie Kagere ambaye aliibuka mfungaji bora msimu uliopita akifunga mabao 22, John Bocco na wengineo.

USHINDANI

Kutokana na usajili wa nguvu ambao Simba walmefanya msimu huu na uwepo wa kikosi kipana, kunaweza kumfanya Kocha Aussems kuumiza kichwa katika kupanga kikosi cha kwanza kwani kutakuwa na ushindani wa namba wa kutosha.

Nafasi ambazo zinatazamwa kuwa na mchuano wa kuwania namba ni kipa na kwa sasa chaguo la kwanza Aishi Manula atakutana na mchuano wa kutosha kutoka kwa Kakolanya, nahodha msaidizi Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ nae atakuwa na changamoto ya kuwania nafasi dhidi ya Gadiel Michael aliyetokea Yanga.

Katika beki wa kulia Shomary Kapombe atachuana na Haruna Shamte, mabeki wa kati waliokuwepo msimu uliopita Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili nao watakutana na mchuano mkali dhidi ya mabeki wa kati wapya Zagueiro, Juma na Fraga ambaye muda mwingine anacheza nafasi ya kiungo mkabaji.

Katika eneo la ushambuliaji hasa mawinga kutakuwa na mchuano kutokana na usajili mpya wa Ajibu, Kahata, Kanda na Athumani ambao watakwenda kuchuano na Cletous Chama na Rashid Juma ambao wanacheza katika eneo hilo.

MAJERUHI

Kabla ya kuanza kwa msimu Simba imekutana na changamoto ya kuwa na majeruhi ya wachezaji watatu Wilker aliyeumia akiwa Afrika Kusini, Ajibu na Manula walioumia wakiwa na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wakiwa na kibarua cha kupambana na Kenya.

Wachezaji hao watatu majeruhi wameshindwa kucheza mechi ya Power Dynamos siku ya Simba Day na mchezo wa kwanza wa kimashindano Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini Msumbiji dhidi ya UD Songo ambao ulimalizika kwa suluhu lakini kuna uwezekano mkubwa wa kukosa pia mchezo wa Ngao ya hisani dhidi ya Azam.

Aussems anasema kufanya maandalizi ya timu kukosa zaidi ya wachezaji watatu muhimu si suala zuri katika maendeleo ya timu lakini anaendelea kuwafatilia kwa karibu ili waweze kupana haraka na kujiunga na wenzao ili kutoa mchango wao.

“Naimani katika mechi ya marudiano dhidi ya UD Songo hapa nyumbani wanaweza kuwa katika sehemu ya timu kwani mpaka wapo katika timu basi ni sehemu ya mipango ya kikosi changu na mchango wao unahitajika ili kuweza kufanikisha malengo,” anasema Aussems.

BAJETI YA MSIMU

Katika msimu uliopita uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ walikubaliana kuweka bajeti ya Sh6 bilioni ambayo itatumika katika timu hiyo kwa mwaka mzima ili kufanya vizuri.

Mo Dewji katika mkutano wake na waandishi wa habari za michezo Mei 22, mwaka huu aliweka wazi msimu huu bajeti ya klabu itazidi kwani hata katika soko la usajili walipanga kuongeza nguvu kwa maana ya kutumia pesa zaidi ya ile ambayo walitumia msimu uliopita.

“Bejeti yetu itakuwa nzuri kwa mwaka mzima tukianzia katika usajili, posho na mahitaji mengine yote ya msingi kwa wachezaji ili waweze kufikiria kazi yao ambayo itakuwa faida kwa timu kama wataweza kwani tutakuwa tumefikia yale malengo yetu,” anasema Mo Dewji.

NAHODHA

Nahodha wa kikosi cha Simba, Bocco anasema katika usajili, wachezaji wengi wapya waliongezwa wana uwezo mzuri na wote wakicheza kwa kushirikiana watakuwa na matokeo mazuri katika mechi nyingi ambazo watacheza msimu huu.

Bocco nasema katika masuala ya kambi uongozi waliwatafutia mahala sahihi kabisa zaidi ya pale walikuwa msimu uliopita, kwani mbali ya kufanya mazoezi ya aina yote kama benchi la ufundi ambavyo walipanga walikuwa katika mazingira tulivu na sahihi ya kuandaa miili yao.

“Kikubwa kuhusu ushindani wa nafasi ya kucheza baada ya usajili huu uliofanyika au wachezaji waliokoseana nafasi zao zitazibwa vipi hilo ni jukumu la makocha na si langu lakini naimani tutafanya vizuri tena zaidi ya ambavyo tulionekana msimu uliopita,” anasema Bocco.

UONGOZI

Magori anasema katika usajili wanaimani wamefanya usajili ulikuwa bora ambao ulizingatia mahitaji ya benchi la ufundi na matarajio yao ni kuona timu hiyo inakuwa bora zaidi ya msimu uliopita ili kufanya vizuri katika mashindano yote ambayo watashiriki.

“Kuhusu masuala ya uwanjani hayo ni wachezaji na benchi la ufundi lakini kwetu uongozi kwa timu ambavyo tumeiona tuna kila sababu ya kuona tunaweza kufanikiwa na kufikia yale malengo ambayo tulikubaliana kuyaweka na kuona timu inafikia hapo,” anasema Magori.