Simba hii imebamba hadi huku unaambiwa

Muktasari:

  • Bondia bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka alisema kwenye mechi za uwanja wa Taifa anaamini Simba haifanyi makosa.

KAMA si Simba nani mwingine? Ndivyo unaweza kutamka wakati mashabiki wa klabu hiyo wakihesabu saa tu kushuhudia timu yao ikitoana jasho na JS Saoura ya Algeria Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo ya kwanza kwa Simba ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika imewabamba hadi wadau wa michezo mingine nje ya Soka ambao ni wanazi wa kubwa wa Simba.

Jamaa wanakwambia, wanachosubiri ni muda tu ufike washuhudie Simba ikiwapa raha wakiamini timu hiyo itapata ushindi mnono Jumamosi.

“Sina presha na Simba, ushindi mbona upo pale Taifa,” alijinasibu bondia Mada Maugo ambaye ni shabiki wa kulia lia wa Simba na kuitabiria Simba ushindi wa mabao 3-0.

Nyota wa riadha nchini ambaye pia ni shabiki kindakindaki wa Simba, Alphonce Simbu alisema kwa kikosi cha Simba wala hana presha ya kuangalia laivu mechi ya kesho kutwa Jumamosi.

“Kikosi kimekamilika, tunaowachezaji wanaojitosheleza kwenye kila safu, waarabu mapema tu wanakalishwa,” alisema Simbu.

Bondia bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka alisema kwenye mechi za uwanja wa Taifa anaamini Simba haifanyi makosa.

“Hata Jumamosi naamini watatutoa kimasomaso Watanzania, timu iko vizuri na hakuna shaka Watanzania wote tutawaunga mkono wawakilishi wetu hao wa Taifa, “ alisema Cheka ambaye ni shabiki wa Simba.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday anakwambia kati ya timu bora nchini hivi sasa ni Simba ambayo inaliwakilisha Taifa.

“Kama Sio Simba nani mwingine, timu imejipanga, haina ‘njaa’ ina wachezaji wa kiwango cha kimataifa, hapo tunakosaje ubingwa, “ alisema.

Kocha wa Tenisi nchini, Riziki Salum ameitakia Simba kila la heri kuelekea katika mchezo huo wa Jumamosi akisisitiza kwamba kwa namna kikosi cha Simba kilivyo, hamasa ya uongozi wake na uchu wa mafanikio wanaamini watafanya vizuri na kushinda Jumamosi.

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Anna Kibira licha ya kuwa shabiki kindaki ndaki wa Yanga, amesema anatamani Simba ishinde kwani ushindi wao utakuwa wa Watanzania wote bila kujali ni Yanga au Simba. Hivi Karibuni Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo iliwaomba mashabiki wote nchini watakaokwenda uwanjani Jumamosi kuiunga mkono Simba kwa kuishangilia.

“Mashabiki watangulize utaifa kwanza, zile itikadi za Yanga kushangilia wageni tuziweke pembeni, bora kukaa kimya kuliko kuwashangilia wageni,” alisema Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo.