Simba hii, acha kabisa watapata tabu sana

Muktasari:

  • Simba sasa imeingia robo fainali, na kuwa kati ya miamba nane ya soka ambayo sasa inasubiri droo itakayopangwa hivi karibuni na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Dar es Salaam. Ilitimu dakika ya 87, kila mmoja akili yake ilisema, aah! Simba basi tena...wengine walisema tusubiri mwakani wengine walikuwa wakishangilia kuwa Simba inarudi kumalizia viporo vyake vya Ligi Kuu.

Mchawi wa soka, King Pele, alisema mpira ni mabao na mpira ni dakika 90. Wakati mawazo ya mashabiki yakiwaza hivyo, wapo waliokuwa na imani kuwa dakika 90 hazijaisha.

Hawa waliokuwa na akili ya kusema tusubiri dakika 90, walikuwa na roho ngumu. Hawakukata tamaa, waliamini kama si Meddie Kagere atakuwa John Bocco kama si Bocco basi mwingine yeyote.

Dakika zikiwa zinasonga, Bocco alipiga mpira wa chini, ni kama anampa pasi Haruna Niyonzima aliyepiga mpira mwingi.  Niyonzima alishamwangalia Clatous Chama aliyekuwa kwenye nafasi nzuri.

Niyonzima alichokifanya, akaupitisha tobo mpira wa Bocco ukamfikia Chama, ambaye ni kama aliomba Miungu yote. Akatikisa nyavu za AS Vita na kuamsha shangwe, furaha, hoihoi na nderemo za kila aina ya mashabiki wa Simba dakika ya 88.

Waliokuwa na mawazo ya Simba ndio basi tena, yakafutika. Simba sasa imeingia robo fainali, na kuwa kati ya miamba nane ya soka ambayo sasa inasubiri droo itakayopangwa hivi karibuni na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Simba imeingia pamoja na miamba mingine ya Kundi D, Al Ahly ya Misri pamoja na Wydad Casablanca (Morocco) na Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini zilizofuzu kutoka Kundi A.

Kundi B limetoa timu za Esperance ya Tunisia na Horoya ya Guinea wakati Kundi C ni TP Mazembe ya DR Congo na CS Costantine ya Algeria.

Kati ya wachezaji waliokuwa kivutio alikuwa Clatous Chama ambaye alifanya kama alivyofanya kwa Nkana Red Devils alipiga bao la tatu kwenye goli lilelile alilowanyongea Wacongoman ambao hawakuamini kilichotokea.

Lakini shoo nzima alisimama nayo Bocco. Alicheza kwa nguvu akipanda na kushuka na alipoingia Niyonzima aliongeza kasi ya mchezo huku akionyesha udambwidambwi wa kutosha katikati.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Simba, Patrick Aussems aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi na kukiri hatua inayofuata ni ngumu zaidi n watakaa chini kuona nini cha kufanya kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zake.

Akizungumzia mchezo huo, mmoja wa wajumbe wa bosi ya wakurugenzi, Abdallah Salim ‘Try Again’, alisema wanachama, wapenzi na mashabiki wa Simba wamefurahi, furaha hii itaendelea kama kawaida.

Aliwataka mashabiki wa Simba kuiunga mkono timu kila mara kwani sapoti yao ndiyo inayowabeba.