Simba haiachi kitu

Mshambuliaji wa Simba,Adam Salamba(kushoto) akichuana  na beki wa African Lyon wakati wa mchezo wa ligi kuu kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana,Simba ilishinda kwa 3-0.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Katika mchezo huo Aussems aliwapanga Nicholaus Gyan, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Adam Salamba na Rashid Juma ambao hawakucheza dhidi ya Yanga.

Arusha. Licha ya Kocha Patrick Aussems kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake kwa kuanzisha wachezaji wanane, Simba ilitoka uwanjani na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon.

Ushindi huo ni muendelezo wa Simba kupata matokeo mazuri katika mechi mbili zilizopita ambapo iliifunga Al Ahly ya Misri bao 1-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuilaza Yanga 1-0.

Simba imefikisha pointi 42 katika mechi 17 ilizocheza na ipo nafasi ya tatu nyuma ya Yanga (58) na Azam (50). African Lyon bado inaburuza mkia ikiwa na pointi 21 katika michezo 26 iliyocheza.

Simba na African Lyon zilivaana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Katika mchezo huo Aussems aliwapanga Nicholaus Gyan, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Adam Salamba na Rashid Juma ambao hawakucheza dhidi ya Yanga.

Kipa Aishi Manula, Pascal Wawa na John Bocco ambao walicheza jana, ndio wachezaji pekee waliokuwemo katika mchezo na Yanga uliochezwa Uwanja wa Taifa, Jumamosi iliyopita.

Simba inatarajiwa kucheza na Azam katika mchezo wa ligi uliopangwa kuchezwa keshokutwa, Dar es Salaam kabla ya kuivaa Lipuli Februari 26.

Mabadiliko hayo hayakuwa na athari kwa Simba kwa kuwa ilicheza soka kwa kiwango bora dakika zote 90 huku Niyonzima, Mzamiru na Dilunga wakionyesha uwezo mzuri katika eneo la katikati.

Licha ya viungo wa African Lyon Awadh Salum na Jabir Aziz kucheza kwa nguvu kwa lengo la kutibua mipango ya akina Niyonzima, lakini walikwaa kisiki baada ya kuzidiwa mbinu.

Ubora wa safu ya kiungo uliitikisa ngome ya African Lyon ambayo mara kwa mara ilikuwa katika wakati mgumu kuokoa mashambulizi ya Simba yaliyoongozwa na nahodha John Bocco.

Pacha ya Bocco na Salamba ilionekana kuwa na madhara langoni mwa African Lyon baada ya kufanya mashambulizi mara kwa mara.

Mashambulizi hayo yaliwashitua African Lyon ambayo ilianza kucheza soka ya kujilinda tofauti na awali ambapo dakika 15 za mwanzo ilicheza kwa kufunguka.

African Lyon ilitumia mbinu ya kumuacha mbele aliyekuwa beki wa zamani wa Yanga, Stephano Mwasika kwa kumpa mipira mirefu lakini haikuwa na madhara langoni mwa Simba.

Kocha wa timu hiyo Selemani Jabir aliingia kwa kutumia mfumo 4-5-1 ambao alijaza idadi kubwa ya viungo na kumuacha Mwasika mbele ambaye kiasili ni beki.

Bocco akionekana kuwa na kiu ya kufunga aliisumbua ngome ya African Lyon na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 27, baada ya kufunga bao kwa mkwaju wa penalti.

Nyota huyo alifunga bao hilo baada ya beki Roland Msonjo kushika mpira wa krosi uliopigwa na Pascal Wawa.

Dakika ya 44 Salamba alionyesha utulivu kwa kutuliza pasi ndefu kwa kifua iliyopigwa na Niyonzima kabla ya kumpa Bocco ambaye alipiga kiki kali na kipa wa African Lyon Douglas Kisembo alipangua vibaya.

Kosa la Kisembo kutema kiki hiyo lilitoa nafasi kwa Salamba kufunga bao la pili kabla ya Simba kuongeza bao la tatu dakika ya 47 lililofungwa na Bocco.

Nguli huyo alifunga bao hilo kutokana na juhudi binafsi za chipukizi Juma ambaye alikimbia kwa kasi na mpira pembeni kabla ya kupiga krosi nzuri iliyotua mguuni kwake.

African Lyon: Douglas Kisembo, Halfan Mbaruku, Omary Salum, Rolland Msonjo, Emmanuel Semwanza, Jabir Aziz, Pato Ngonyani, Awadhi Juma, Stephano Mwasika, Said Mtikila and Ramadhani Chombo.

Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Pascal Wawa, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Adam Salamba, John Bocco na Rashid Juma.

Katika mechi nyingine za Ligi Kuu Bara zilizochezwa jana, Azam ilitoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union, Mwadui iliichapa Biashara United mabao 2-1, Ruvu Shooting ilitoka suluhu na Kagera Sugar.