Simba VS Al Ahly mtu atateseka!

Tuesday February 12 2019

 

By Charles Abel

HAPANA shaka ubora na ufanisi wa wachezaji ndio una nafasi kubwa ya kuamua matokeo ya mchezo baina ya Simba na Al Ahly leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa.

Kiwango bora kilichoonyeshwa na wachezaji wa Ahly kwenye mchezo wa kwanza ambao Simba ilifungwa mabao 5-0 jijini Alexandria, Misri ilikuwa ni sababu tosha iliyowateketeza wawakilishi hao wa Tanzania.

Hata hivyo, baada ya kupoteza mechi ya kwanza, ni wazi kwamba nyota wa Simba wamefanyia kazi udhaifu wao wa mchezo uliopita ili wafanye vizuri leo ili wapate pointi tatu muhimu lakini pia kuwafuta machozi mashabiki wao na Watanzania kiujumla.

Pamoja na ubora na kiwango cha kitimu na mchezaji mmojammoja kwa wachezaji wa Al Ahly, Simba inayo nafasi ya kuwanyamazisha Waarabu hao ikiwa nyota wake watajituma na kufuata vyema maelekezo ya benchi la ufundi katika dakika zote tisini.

Kwa kulitambua hilo, gazeti hili linakuletea taswira ya vita ya ndani ya uwanja baina ya wachezaji wa Simba na Ahly ambayo yule atakayefanikiwa kushinda atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi.

Hata hivyo uchambuzi huu haumaaniishi vikosi vya timu zote mbili ndivyo vitakavyopangwa leo. Vinaweza kubadilika kulingana na matakwa ya benchi la ufundi

Advertisement

Meddie Kagere vs

Ayman Ashraf

Baada ya kucheza mechi mbili mfululizo za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika bila kufunga bao, mshambuliaji Meddie Kagere atakuwa na nafasi nyingine ya kuthibitisha ubora wake kwa kuifungia Simba bao.

Hata hivyo, Kagere mwenye mabao matano kwenye mashindano hayo, atakuwa na kibarua kizito mbele ya beki Ayman Ashraf ambaye alimficha kwenye mechi ya kwanza.

Emmanuel Okwi vs

Saad Samir

Emmanuel Okwi amekuwa aking’aa mara kwa mara pindi anapokutana na timu za Kaskazini mwa Afrika akiwa na timu yake ya Taifa, Uganda au ndani ya jezi za klabu yake.

Okwi licha ya kujaribu kuonyesha makeke kwenye mechi ya kwanza kule Misri, alijikuta akiondoka bila bao na hiyo ilitokana na upinzani kutoka kwa beki Saad Samir ambaye kuna uwezekano mkubwa akakutana naye leo tena.

Cletous Chama vs

Mohamed Hany

Mmoja wa wachezaji nyota kwenye kikosi cha Simba kwa sasa ni kiungo Mzambia Cletous Chama lakini katika mechi mbili zilizopita za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika alionekana kuchemsha.

Miongoni mwa wachezaji waliochangia kumficha Chama ni beki mwenye umri wa miaka 23 wa Al Ahly, Mohammed Hany ambaye leo ana nafasi kubwa ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza kutokana na kukosekana kwa nahodha Mohamed Fathi.

Rashid Juma/Dilunga vs

Al Maaloul

Mchezaji yeyote atakayepangwa upande wa kulia wa Simba kati ya Hassan, Dilunga, Rashid Juma na hata Haruna Niyonzima, ajiandae kukutana na shughuli pevu ya beki Mtunisia, Ali Maaloul ambaye ana kasi na uwezo mkubwa wa kufunga, kupiga pasi za mabao na kupandisha timu.

Jonas Mkude vs

Amr Hesham Mohamed

Mkude anaweza kuwa miongoni mwa viungo ambao kocha Patrick Aussems atawapanga kwenye mechi ya leo akitegemewa kuanza kuichezesha timu kuanzia nyuma lakini anapaswa kujiandaa kukutana na upinzani mkali kutoka kwa kiungo mgumu, Hesham Mohamed ambaye amekuwa akitumiwa na Ahly kutibua mipango ya wapinzani.

James Kotei vs

Hussein El-Shahat

Wahenga walisema ukitaka kuua mbu, anza kuua mazalia yake na ndivyo inavyotakiwa kufanywa na kiungo mkabaji wa Simba, James Kotei leo.

Kiungo huyo Mghana anapaswa kufanya kazi ya ziada kumficha El-Shahat ambaye ndiye mchezaji ghali anayecheza ndani ya Afrika kwa sasa akiwa amenunuliwa na Ahly kwa dau la zaidi ya Shilingi 17 bilioni kutoka Al Ain ya Falme za Kiarabu.

Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ vs Ramadan Sobhi

Miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao watakuwa na wakati mgumu kesho ni beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye atakabiliana na nyota wa Huddersfiled anayecheza kwa mkopo Al Ahly, Ramadan Sobhi.

Sobhi ni mchezaji mwenye kasi, uwezo wa kupiga chenga, kufunga na kupiga pasi za mwisho lakini pia ana stamina ya hali ya juu jambo ambalo Tshabalala anapaswa kujiandaa vilivyo kukabiliana naye.

Paschal Wawa vs Junior Ajayi

Kwenye mechi ya kwanza nchini Misri, beki Paschal Wawa alijikuta kwenye wakati mgumu wa kumdhibiti mshambuliaji kutoka Nigeria, Junior Ajayi anayecheza Al Ahly ambapo straika huyo alifunga na kupiga pasi moja ya bao. Wakati mwingine umefika kwa Wawa kujiuliza mbele ya Ajayi kwenye Uwanja wa Taifa leo.

Juuko Murushid vs Karim Nedved

Nidhamu, utulivu na umakini wa hali ya juu unatakiwa kuwepo kwa beki Juuko Murshid leo pindi atakapokuwa akikabiliana na kiungo mshambuliaji Karim Nedved ambaye Ahly humpanga nyuma ya mshambuliaji wa kati.

Katika mchezo uliopita, mabeki wa Simba walipata wakati mgumu mbele ya Nedved ambaye aliwafunga mabao mawili.

Nicholas Gyan vs

Nasser Maher

Kiasili, Nicholas Gyan sio beki wa pembeni lakini baada ya kufika Simba alibadilishwa na kuanza kuchezeshwa kama beki wa upande wa kulia.

Amekuwa akijitahidi kwenye baadhi ya mechi lakini nyingine amekuwa akichemka hasa akikumbana na timu zenye viungo na washambuliaji wazuri wa pembeni.

Leo atakuwa na kibarua mbele ya kiungo mshambuliaji Nasser Maher.

Advertisement