Simba SC yasubiri kombe lake, Azam, Yanga wakabana koo, Singida United maji shingoni

Wednesday March 25 2020

Simba SC yasubiri kombe lake, Azam, Yanga wakabana koo,Singida United maji shingoni,Ligi Kuu Tanzania Bara ,

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam.Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imesimama kwa muda, baadhi ya klabu zinazoshiriki mashindano hayo zimepitia katika kipindi kigumu na nyingine neema kutokana na matokeo waliyopata.

Serikali imesimamisha michezo yote kwa siku 30 kutokana na janga la ugonjwa wa corona ambalo limetikisa sekta hiyo ukiwemo mchezo wa soka.

Janga la corona limesababisha idadi kubwa ya ligi UIaya kusimama hadi Aprili 3 kabla ya mashindano kuanza endapo hali ya utulivu itarejea.

Janga hilo pia limeleta mtikisiko katika Ligi Kuu Bara ambapo hadi inasimama Simba ilikuwa inaongoza katika msimamo.

Simba inaongoza ikiwa na pointi 71 ikifuatiwa na Azam (54), Yanga (51) na Namungo (50) ambayo imekuwa tishio licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza.

Wakati idadi kubwa ya timu zikiwa zimebakiza mechi 10 kumalizika ligi, kimahesabu Simba ina nafasi ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya tatu mfululizo.

Advertisement

 

Simba moto

Achana na kuongoza ligi kwa pointi nyingi na kuwaacha mbali watani wake wa jadi Yanga, Simba imeonekana ni moto mkali wa kufunga mabao msimu huu.

Hadi sasa Simba ndio timu iliyofunga mabao mengi ikiwa imepachika 63 ikifuatiwa na Azam 37 na Kagera Sugar 36 huku Yanga ikiwa imefunga mabao 31.

Pia Simba iko vizuri katika safu yake ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao machache mpaka sasa kwenye ligi ikiwa imefungwa 15 kulinganisha na timu nyingine.

 

Wazawa wafunika

Ingawa Meddie Kagere ndiye anaongoza kwa kufunga mabao 19 lakini kasi ya kufunga kwa wachezaji wazawa msimu huu imeonekana iko juu.

Kwa misimu takribani mitatu iliyopita, wageni walionekana kutawala kwa kufunga mabao huku wachezaji wazawa wakipotezwa katika eneo hilo.

Msimu huu mambo yameonekana kuwa tofauti kwani mpaka ligi hiyo inasimama idadi kubwa ya wazawa walicheza kwa kiwango bora katika safu ya ushambuliaji kwa timu zao.

Washambuliaji wazawa Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar, Paul Nonga (Lipuli), Reliants Lusajo (Namungo) kila mmoja amefunga mabao 11.

Mhilu anasema anashindwa kujiaminisha kama anaweza akamfukuzia Kagere ambaye amemzidi mabao manane, ingawa soka ni mchezo wa maajabu lolote linaweza kutokea.

“Ujue soka ina maajabu yake, angalia mfano Kagere hakufunga muda mrefu akaja akaibukia kwa Singida na  kufunga mabao manne, hilo ndilo linanifanya nisikate tamaa kwamba ninaweza nikafanya maajabu katika mechi zilizobaki licha ya kwamba yeye ana nafasi kubwa ya kuwa mfungaji bora.

“Kuna changamoto nyingi ikiowemo kukosa motisha kwa wachezaji hasa wa timu ndogo, pia mechi zenyewe zinaoonyesha huku Bukoba ni timu tatu. Simba, Yanga na Azam ukiona kuna mchezaji anafunga mabao mengi nje ya hizo klabu ujue anajituma.

Lusajo anasema bado kuna mechi nyingi hivyo hawezi kukata tamaa kwa kumuachia Kagere awanie kiatu cha dhahabu katika ligi hiyo msimu huu.

“Ni changamoto kuzidiwa na wageni ingawa kuna wakati hata sisi wazawa tunafanya vyema. Sijakata tamaa nitapambana mpaka mwisho wa msimu  na hapo ndio itajulikana nani ni mfungaji bora,”anasema.

Maajabu ya Namungo

Moja ya klabu ambayo ina mashabiki wengi kutokana na kiwango ilichokionyesha mpaka sasa kwenye ligi ni Namungo FC.

Namungo yenye maskani yake Ruangwa, Lindi imeweza kuonyesha soka safi iliyochangia kukaa nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 50, ikizidiwa moja tu na Yanga.

Kitu kinachowashangaza wengi ni kwamba timu hiyo   imepanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu huu lakini soka  la kitabuni  inalopiga hata Yanga na Simba wakati mwingine zinasubiri

Biashara United usipime

Timu nyingine ambayo imenekana kutikisa kwenye Ligi Kuu ni Biashara United ya Mara.

Licha ya timu hiyo kuwa  ndogo lakini imekuwa na kiwango bora  kwa  kiasi cha kuwashtua wadau wengi wa soka hapa nchini huku ikibebwa na wachezaji wake kama  Innocent Edwin mwenye mabao matano, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, James Mwasote, Bright Obina, Atupele Green na nahodha Abdulmajid Mangalo.

 Biashara United imeshaanza kujiondoa na presha ya kushuka daraja kwani kwa sasa iko nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi, ikiwa imecheza michezo 28, imeshinda 10, imetoka sare tisa, imepoteza tisa na ina pointi 39.

Timu hiyo inayonolewa na kocha Mkenya Francis Baraza, katika michezo 12 ya hivi karibuni, imeshinda sita, sare nne na kupoteza mechi mbili dhidi ya Simba na Lipuli ya Iringa.

Kocha huyo alitua ndani ya timu hiyo mapema Novemba, mwaka jana na ameonekana kuisadia Biashara United kuwa katika kiwango bora kwani tangu aanze kuinoa ameiongoza katika michezo 18, imeshinda minane, imetoka sare  michezo saba na imepoteza mitatu dhidi ya Yanga, Simba na Lipuli.

Singida United maji shingoni

Singida United ambayo huu ni msimu wake wa tatu kushiriki Ligi Kuu Bara tayari imeonekana kuchungulia kaburi la kushuka daraja kwani inashika mkia kwenye msimamo wa ligi na haina uhakika  wa kupona kutokana na msimu huu timu zinazotakiwa kushuka sita.

Timu hiyo si tu inashika mkia lakini pia ndiyo timu iliyoruhusu mabao mengi kwenye ligi ikiwa imefungwa mabao 49  huku pia ikiwa ndio timu pekee iliyofunga mabao machache ikiwa imefunga 16.

Akizungumzia mashindano hayo kocha Kennedy  Mwaisabula anasema  ligi ya msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa lakini jambo linalomfurahisha zaidi ni jinsi wachezaji wazawa walivyoamka na kupigania timu zao.

Janga la corona   limekuja katika muda ambao ligi ndio ilikuwa imepamba moto kwani timu nyingi zilikuwa zinaonyesha ushindani mkubwa hasa hizi zinazopambana na janga la kushuka daraja. Hivyo hali hii ikipita  ligi ikirejea  timu nyingi zitakuwa zimeathirika kwani  sidhani kama wachezaji wataweza  kutunza viwango vyao

“Kitu kilichonifurahisha katika ligi hii ni jinsi washambuliaji wazawa wanavyotikisa kwa ufungaji, mfano  yule Lusajo na Kikoti wa Namungo, Mhilu (Kagera), Paul Nonga (Lipuli) na Peter Mapunda wa Mbeya City wameonyesha thamani  ya wazawa. Kila mara wageni ndio walikuwa wakitamba kwenye ufungaji lakini safari hii wanakwenda nao sambamba nawapongeza sana,”anasema Mwaisabula ambaye amewahi kuzinoa timu za Cargo, Bandari na Yanga kwa nyakati tofauti.

Mtazamo kocha wa AFC ya Arusha inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Ulimboma Mwakingwe kwa upande wake ametoa pongezi kwa washambuliaji wazawa kuonyesha kiwango bora msimu huu.

“Ligi inakwenda vizuri na baadhi ya  timu zimeshangaza kama, Namungo, Biashara United, Coastal Union, Polisi Tanzania na hata Ndanda  zinacheza soka safi lakini kitu kizuri washambuliaji wazawa hivi sasa wanachuana na wageni,”anasema kocha huyo.

Ulimboka ni miongoni mwa mawinga waliocheza kwa mafanikio Simba na Taifa Stars akiwa mmoja wa wafungaji bora katika mechi za mashindano mbalimbali kabla ya kustaafu.

Advertisement