Simba SC yanasa siri nzito AS vita

Muktasari:

  • Kila mchezaji wa Simba atakayepata nafasi ya kucheza mechi hiyo, anapaswa kuhakikisha hafanyi makosa ya utovu wa nidhamu hasa kucheza rafu zinazoweza kuwapatia wapinzani faulo zitakazotumiwa na wenyeji kufunga mabao.

UNAAMBIWA hata kabla msafara wa Simba haujaondoka mapema asubuhi ya leo kwenda DR Congo, klabu hiyo tayari imenasa siri nzito ambazo zitawafanya nyota wake wakiwamo Emmanuel Okwi na Meddie Kagere kuwa na kazi nyepesi ugenini.

Simba ilitarajiwa kupaa saa 2:30 asubuhi ya leo Alhamisi kuifuata AS Vita itakaovaana nayo keshokutwa Jumamosi katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikisaka ushindi wa pili kundini utaoaisaidia kujikita zaidi kileleni.

Sasa kabla msafara wa Simba haujaondoka, inaelezwa wamenasa taarifa muhimu za ndani na nje ya uwanja ambazo zikifanyiwa kazi zinaweza kuwabeba katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu kwani wenyeji walipoteza mechi yao awali ugenini.

Simba inayoondoka na usafiri wa ndege ya Shirika la Kenya ‘Kenya Airways’ itatua jijini Kinshasa ambako itachezwa mechi hiyo ikiwa na ripoti kamili mkononi ya mbinu za kufundi na mikakati ya nje ya uwanja ambayo Vita imekuwa ikiitumia kupata matokeo pindi inapokuwa nyumbani.

Vita iliyolala kwa Al Ahly imekuwa ikifunga mara kwa mara mabao ya vichwa kutokana na uwezo na maumbo ya nyota wanaounda kikosi chake, kazi inayowapa kibarua mabeki Pascal Wawa na Juuko Murshid kujipanga mapema kabla ya mechi.

Kina Juuko wanapaswa kuwa makini na mipira ya krosi, kona na ile ya adhabu ndogo ambayo ndio huwa chanzo cha mabao ya vichwa ya nyota wa Vita hasa wanapocheza mechi za nyumbani.

Kila mchezaji wa Simba atakayepata nafasi ya kucheza mechi hiyo, anapaswa kuhakikisha hafanyi makosa ya utovu wa nidhamu hasa kucheza rafu zinazoweza kuwapatia wapinzani faulo zitakazotumiwa na wenyeji kufunga mabao.

Lakini Vita pia imekuwa ikitumia mbinu ya kupiga mipira mirefu na kushambulia kwa kasi lango la adui ili kulazimisha mabeki wa timu pinzani wafanye makosa ambayo huyatumia kufunga mabao.

Safu ya ulinzi ya Simba inapaswa kucheza kwa nidhamu na kuepuka kutengeneza mitego ya kuotea ambayo inaweza kuwagharimu mbele ya washambuliaji wa AS Vita.

Katika mbinu hiyo ya kutumia mipira mirefu, silaha kubwa ya Vita ambayo huangamiza timu pinzani, ni mshambuliaji wake tishio na tegemeo, Jean Marc Makusu Mundele ambaye ana ujanja, kasi mbinu na uwezo wa hali ya juu wa kuichezesha timu, kupiga pasi za mwisho, kufunga mabao na kusumbua mabeki.

Makusu aliyeshika nafasi ya pili katika ufungaji kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, anaweza kufunga mabao kwa kichwa, mashuti na pia ni mfungaji mzuri wa mabao ya faulo.

Sehemu nyingine ambayo inawapa jeuri Vita ni safu yao ya ulinzi ambayo hucheza kwa nidhamu ya hali ya juu na imekuwa haifanyi makosa ya mara kwa mara lakini ni imara katika kudhibiti mashambulizi ya mipira ya juu, ingawa sio wazuri sana pindi wanapokabiliana na timu zinazopiga pasi za chinichini na za haraka.

“Nimebahatika kuiona Vita kwenye mechi yake dhidi ya Al Ahly. Ukiachana na mafanikio yake ya msimu uliopita, jamaa wana timu nzuri na inayocheza soka la mbinu na ina wachezaji wenye ubora wa hali ya juu, hivyo ni lazima tujipange vizuri kukabiliana nao.

“Ni timu yenye wachezaji ambao wanaweza kukuadhibu pindi unapofanya makosa, hivyo ni lazima tucheze kwa nidhamu ya hali ya juu na tunatakiwa kuwa na mpango unaoeleweka. Kama kocha anaingia na mbinu ya kujilinda, basi tujilinde hasa na kama tunashambulia, basi tuhakikishe kila nafasi tunayoipata tunaitumia,” alisema beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa.

Nje ya uwanja, nyota wa zamani wa Tanzania waliowahi kucheza soka la kulipwa huko DRC, Musa Hassan ‘Mgosi’ na Ngawina Ngawina, wameipa tahadhari Simba kujipanga na mbinu chafu za AS Vita kuwavuruga wachezaji kisaikolojia.

“Timu za DRC kiukweli zipo vizuri ndani ya uwanja na hata ukiangalia ushiriki wao kwenye mashindano ya kimataifa utalithibitisha hilo lakini pamoja na hilo zimekuwa zikitumia sana mbinu za ovyo za nje ya uwanja kuwavuruga wapinzani pindi zinapokuwa nyumbani.

Simba wanapaswa kuwa makini na wawaandae wachezaji kisaikolojia kwani timu za kule zimekuwa na vitimbi, fitina na vurugu kubwa kwa wapinzani pindi wanapocheza nao. Kuanzia Simba watakapoingia Congo, wakati wa mazoezi, barabarani, hoteli na hadi siku ya mchezo watakutana na vitisho vya hali ya juu ambavyo vyote lengo ni kuwavuruga tu,” alisema Ngawina aliyewahi kucheza TP Mazembe.

Kwa upande wake Mgosi aliunga mkono kauli ya Ngawina ingawa alisema Simba wanaweza kukutana na unafuu kutokana na ugomvi wa AS Vita na DC Motema Pembe.

“Mashabiki wa DRC huwa hawana utimu pindi timu mojawapo inapowakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa lakini afadhali ya Simba ni kwamba kwa sasa Vita haina uhusiano mzuri na Motema Pembe ambayo mimi ndio nilikuwa nachezea.

Lakini pia wachezaji wanapaswa kuiwaza zaidi mechi na wasitishwe na vurugu za nje ya uwanja kwa sababu pale Kinshasa ndipo huwa kuna vurugu zaidi kuliko mechi inayochezwa Lubumbashi.

Vita ni timu kubwa tunayopaswa kuiheshimu lakini hatutakiwi kuingia na akili ya kujilinda. Tushambulie huku tukichukua tahadhari kubwa kwa sababu hii ni hatua ya makundi na kinachohitajika ni pointi,” alisema Mgosi.

Tayari Simba imeshatanguliza baadhi ya viongozi wake huko DRC, umeliambia gazeti hili kuwa kila kitu kinakwenda sawa.

“Kuhusu masuala ya usalama hakuna tatizo kwani tumeshahakikishiwa ulinzi wa kutosha kule lakini pia tumegundua changamoto mbili ambazo tumeanza kuzishughulikia ambazo ni foleni ya barabarani pamoja na gharama za hoteli kuwa juu lakini zote tutazitatua vizuri tu watu wasiwe na wasiwasi wowote,” alisema mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya Simba, Mulamu Nghambi.