Simba SC jipangeni upya, TPLB ipangeni vyema ratiba ya viporo

Muktasari:

  • Inawezekana nyota wa Simba roho zikawauma kwa kushindwa kutimiza ahadi yao ya kupata ushindi wa kwanza ugenini katika hatua ya juu ya michuano hiyo, lakini kwa kazi waliyoifanya hawapaswi kujilaumu sana. Simba ilicheza na timu kubwa na yenye rekodi katika michuano ya Afrika, hivyo ni wajibu wao kurejea nyumbani na kujipanga upya kwa msimu ujao.

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Simba imeyaaga Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 4-1 na TP Mazembe ya DR Congo.

Licha ya kutolewa, lakini hatu waliyofikia Simba haikuwa mbaya ikiziangatiwa kuwa, yenyewe mipango yao ya awali ilikuwa ni kufuzu hatua ya makundi, jambo ambalo ilifanikiwa kulitimiza kwa kuing’oa Nkana FC ya Zambia katika mechi za raundi ya kwanza.

Inawezekana nyota wa Simba roho zikawauma kwa kushindwa kutimiza ahadi yao ya kupata ushindi wa kwanza ugenini katika hatua ya juu ya michuano hiyo, lakini kwa kazi waliyoifanya hawapaswi kujilaumu sana. Simba ilicheza na timu kubwa na yenye rekodi katika michuano ya Afrika, hivyo ni wajibu wao kurejea nyumbani na kujipanga upya kwa msimu ujao.

Kwa sasa Simba itulize akili na kupambana kwenye Ligi Kuu Bara kwa kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kupata matokeo mazuri mbele ya wapinzani wao hasa kwenye michezo yao ya viporo kusudi watetee taji lao walilotwaa msimu uliopita. Wekundu wa Msimbazi hao, hawana nafasi nyingine yoyote ya kupata tiketi ya ushiriki wa mechi za kimataifa msimu ujao isipokuwa kwa kunyakua taji la Ligi Kuu ambalo pia linatolewa macho na klabu za Azam na Yanga zilizopo nafasi mbili za juu kwenye msimamo.

Mwanaspoti tunawapa pole na pia kuwapongeza Simba kwa uwakilishi mzuri wa michuano hiyo ya Afrika kwani ni muda mrefu, timu za Tanzania zilikuwa hazijawahi kufikia hatua ya juu ya mashindano kama walivyofanya wawakilishi wao msimu huu.

Mara nne ambazo timu za Tanzania kucheza makundi, mbili katika Ligi ya Mabingwa na mbili za Kombe la Shirikisho, Simba na Yanga zilikuwa kama washiriki tu na kusindikiza wapinzani wao, lakini mara hii ya tano ambayo Simba ilipata nafsi ya kucheza imeitoa kimasomazo nchi. Wanastahili pongezi hata kama tayari Simba imeshayaaga mashindano.

Pamoja na kuipongeza Simba kwa mafanikio iliyopata msimu huu katika michuano hiyo ya CAF, pia kama wadau wa michezo tulikuwa tunaikumbusha Bodi ya Ligi (TPLB) kwamba huu ni wakati wa kutengeneza ratiba ya kuhakikisha mechi za viporo zinachezwa kwa uwiano sawa.

Awali TFF na TPLB walikuwa wakitoa visingizio vya kuahirishwa mechi ovyo kwa madai ya ratiba yao kuingiliana na mechi za kimataifa za Simba, kwa sasa Simba imeshatoka ni wajibu wao kuipanga vyema ratiba hiyo ili timu zicheze kwa uwiano sawa na kuzipunguzia mzigo wa gharama. Hata Simba ambao wanarudi wakiwa na uchovu wa kibarua cha kimataifa watambue kuwa, kazi kwao ndio kwanza zinaanza kwa vile watalazimika kula viporo vyao ndani ya muda ili kuifanya Ligi Kuu iwe na uwiano kwa klabu zote 20 zinazoshiriki.

Ukiangalia msimama wa ligi hiyo, Simba ina mechi 22 tu wakati klabu nyingine zimecheza mechi 33 kwa maana hiyo ni kwamba watetezi hao wana michezo 11 mkononi kabla ya kulingana na wenzao.

Maana yake ni kwamba itapaswa icheze mechi zake za viporo kabla ya kwenda sambamba na wenzao ambao wamesaliwa na idadi ndogo kabla ya kufungia msimu. Hatutarajii kusikia tena ratiba ikipangwa kisha ikapanguliwa kwa kisingizio hiki na kile labda itokee janga la kiasili ambalo halikwepeki.

Kadhalika hata hivyo ratiba ya viporo ipangwe kwa kuangalia jiografia ya nchi ilivyo kwa nia ya kuepuka kuwachosha wachezaji wa Simba kwa maana mechi ziwe zinapisha kwa muda utakaowapa nafasi wachezaji kupumua na kupata mapumziko.

Pia ni vyema TPLB ikahakikisha ratiba ya mechi hizo zinatoa nafasi kwa timu pinzani zitakazocheza na Simba nazo zinapata wasaa wa kupumzika, lakini pia wasimamizi wahakikishe haki inatendekea kwenye mechi hizo ili kutoa matokeo yasiyoleta mashaka.

Hizi ni mechi za lala salama, kuna timu zitakazocheza na Simba hazina cha kupoteza na zipo nyingine zipo kwenye mapambano la kuepuka kushuka daraja na hata matokeo yao wakati mwingine yanaweza kuleta athari kwa klabu nyingine ambazo tayari zilishacheza na Simba ila hazipo eneo lililo salama.

Kwa kuwa tunapenda kuona ligi inamalizika bila mizengwe wala malalamiko, basi ni wazi hata waamuzi watakaopangwa kuchezesha watazingatia sheria za soka.