Simba Queens yakabidhiwa kombe lao, TSC Queens na Panama Girls zashuka Daraja

Muktasari:

Simba Queens wamekabidhiwa kombe lao baada ya kuongoza Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2019/2020 kwa pointi 52, huku timu za TSC na Panama Girls zikishuka daraja.

Mwanza. Achana na ishu ya kukabidhiwa kombe Simba Queens, leo Wekundu hao wameifanyia TSC Queens kitu mbaya kufuatia kichapo cha mabao 9-0 na kuwafanya wapinzani hao kushuka rasmi Daraja.

Katika mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Nyamagana jijini hapa, Simba Queens ambao walikuwa tayari wametangazwa bingwa mpya, walihitaji ushindi ili kusherehekea vyema na mashabiki wao, huku TSC wakisaka ushindi ili kujinusuru na janga la kushuka Daraja.

Mabao ya Opa Clement na Mwanahamis Omary ambao wote wamefunga matatu kila mmoja 'Hatitriki' pamoja na ya Joelly Bukuru aliyefunga mawili na Asha Jafari moja, yalitosha kuwashusha wapinzani wao TSC ambao walikuwa wenyeji wa michezo huo.

Hata hivyo licha ya kukubali kipondo hicho kikali, TSC walionesha ushindani licha ya kwamba Simba Queens walikuwa bora kwa kuwazidi kila kitu ndani ya uwanja na kusababisha matokeo hayo.

Katika michezo mingine ambayo ilichezwa mapema katika viwanja viwili tofauti jijini Mwanza, Alliance Girls wameikandika Mlandizi Queens mabao 2-0, mchezo uliochezwa uwanja wa Nyamagana majira ya saa 8 mchana.

Katika mechi nyingine ya kuhitimisha Ligi hiyo ambayo ilichezwa dimba la CCM Kirumba, Marsh Queens wamekubali kuloa kwa kichapo cha mabao 6-0 dhidi ya Jkt Queens na maafande hao kujihakikishia kumaliza mashindano hayo nafasi ya pili kwa alama 52.

Katika hafra hiyo ya kukabidhi kombe kwa bingwa, viongozi wa shirikisho la soka nchini (TFF) waliwakilishwa na Rais wake, Walles Karia pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya Ufundi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati tendaji, Vedatus Luphano ambao waligawa zawadi kwa washindi hao.