Simba Queens yachimbwa mkwara

Muktasari:

  • Chobanka aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi katika dimba la Nyamagana kushuhudia Simba anavyopokea kichapo, kwani uwepo wao huongeza nguvu ya kupambana.

MWANZA.KESHO Jumatano, Alliance Girls itawavaa Simba Queens katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake lakini Kocha wao, Ezekiel Chobanka ametamba Wekundu wa Msimbazi lazima wakae.

Kikosi hicho chenye maskani yake Mahina jijini hapa, kinashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo kikiwa na pointi 26 walizozipata katika michezo 13 waliyocheza.

Alisema wamefanya maandalizi ya kutosha, kilichobaki ni kuifunga Simba licha ya mchezo wa kwanza kutoka sare ya bao moja katika dimba la Karume.

“Tumefanya maandalizi ya kutosha, mechi ya kwanza walisawazisha bao dakika za lala salama kutokana na mfumo tunaotumia ugenini ila kwa mfumo wa nyumbani, Simba watakubali mziki wetu,” alisema Chobanka.

Chobanka alisema anafahamu wapinzani wake wameboresha kikosi chao lakini nyota wao wote waliowasajili dirisha dogo anawafahamu vyema, hivyo hawampi tabu ya kuwadhibiti.

Alisema katika mchezo huo watamkosa winga wao Elizabeth Edward ambaye anasumbuliwa na malaria lakini ametamba pengo lake halitaonekana kwani ana wachezaji wengi wanaocheza nafasi yake.

Chobanka aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi katika dimba la Nyamagana kushuhudia Simba anavyopokea kichapo, kwani uwepo wao huongeza nguvu ya kupambana.

“Shabiki ni mchezaji wa 12, nashukuru huwa wanajitokeza kwa wingi kutupa sapoti, niwaombe wajitokeze kwa wingi na watashuhudia soka safi na matokeo mazuri,” alisema.