Simba Fantastic!

Muktasari:

Mashabiki wa Yanga waliojichanganya na wale wa wageni waliovalia uzi kama wao wa Jangwani, walijuta kuifahamu Simba, baada ya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere kufunga mabao hayo matamu katika mchezo huo.

OOH! Yes we can...! Simba ya Mo Dewji noma sana. Unajua nini? Jana ikiupiga mpira mwingi na kuwanyamazisha Waarabu na wapambe wao wa Yanga waliokuwa wakiishangilia JS Saoura ya Algeria na kupata ushindi wa mabao 3-0.

Simba ilipata ushindi huo katika mchezo mkali wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Wekundu hao wa Msimbazi wakaendeleza rekodi yao kuzitesa timu za Afrika Kaskazini zinapokanyaga tu nchini.

Mashabiki wa Yanga waliojichanganya na wale wa wageni waliovalia uzi kama wao wa Jangwani, walijuta kuifahamu Simba, baada ya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere kufunga mabao hayo matamu katika mchezo huo.

Alianza Emmanuel Okwi kufunga bao la kwanza dakika za jioni kabla ya mapumziko, ambapo mashabiki wachache wa Yanga waliokuwa wakiishangilia JSS waliamini lingerudi kipindi cha pili kwa kuwaamini Waalgeria hao walioibana Simba kwa muda mrefu kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, kabla ya bao hilo la Okwi ambaye katika mchezo wa jana aliupiga mpira mwingi, nahodha John Bocco aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Meddie Kagere aliyeanzia benchi katika pambano hilo kali lililohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliyekuwa mgeni rasmi. Mbali na viongozi hao wa kiserikali, pia Bilionea wa Simba Mohammed ‘Mo’ Dewji na viongozi mbalimbali wa Simba wakiwamo wale wa zamani, walikuwapo uwanjani hapo kuwashuhudia vijana wao wakithibitisha kauli mbiu yao ya ‘Yes We Can’.

Kuingia kwa Kagere kuliongeza kasi ya Simba na waliporudi kipindi cha pili alifunga mabao mawili na kuihakikisha timu yake ushindi huo, huku akifikisha mabao matano katika orodha ya wafungaji wa michuano hiyo.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Kocha wa Simba Patrick Aussems aliwaanzisha Pascal Wawa na Juuko Murshid waliotengeneza ukuta mgumu uliowanyima wageni hao wa michuano hiyo ya Afrika nafasi ya kuipenya kiasi cha kumfanya kipa Aishi Manula kuwa likizo muda mrefu.

Simba ilianza kwa mashambulizi ya haraka ndani ya dakika moja iliweza kupata kona mbili ambazo hazikuweza kuzaa bao.

Upande JSS wao walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza wakionekana kuwa na mipango ya polepole.

Viungo Hassan Dilunga, James Kotei na Jonas Mkude walielewana eneo katikati kiasi cha kuwapoteza waarabu ndani ya dakika 7 za mwanzo.

Dakika ya nane Cletous Chama na Emmanuel Okwi waligongeana pasi za haraka na Okwi kupiga pasi kwa Hassan Dilunga aliyepiga shuti lililopaa juu.

Waalgeria walitumia upande wa kulia wa Simba uliokuwa chini ya Nicholas Gyan kupitisha mashambulizi, huku winga Mohammed Boulaouidet akionekana kuwa kasi, licha ya kuwa hakuleta madhara langoni mwa Aishi Manula.

Simba ilikosa bao dakika ya 19 baada ya Okwi kuingia na mpira ndani ya dimba na kupiga shuti kali ambalo liligonga mwamba na kumfanya ashike kichwa.

Kabla ya mshambuliaji wa JSS, Ziri Hammar kumtesti Manula katika dakika ya 30 kwa shuti la mbali lililokuwa kama chakula tu.

Dakika ya 36, Bocco aliumia na kutolewa kwa machela na kuingia Kagere mabadiliko yaliyobadilisha kabisa kasi ya ushambuliaji ya Simba, ambapo sekunde chache kabla ya mapumziko pasi murua ya Chama ilimkuta Okwi katikati ya msitu wa mabeki wa JSS na kuwahadaa kabla ya kufunga kwa shuti kuitanguliza Simba.

KAGERE MOTO

Kipindi cha pili Simba ilionekana kutakata zaidi na hasa maelewano ya Dilunga, Chama, Mkude, Okwi na Kagere.

Safu hiyo ya ushambuliaji ya Simba iliisumbua sana ngome ya JS Saoura na dakika ya 51, Kagere aliiandikia Simba bao la pili baada ya Okwi kutegua mtego wakuotea wa Waalgeria na kumpenyezea straika huyo pasi aliyoiweka kimiani.

Dakika 63 Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Dilunga na kuingia Mzamiru Yassin ili kuweza kuimarisha safu ya kiungo.

Kagere kwa mara nyingine aliwanyamzisha waarabu baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 67 akipokea pasi akiwa peke yake na kueleka langoni, ambapo kipa wa JSS aliamua kutoka kumkabili na kupisha na shuti lake lililoenda wavuni.

JSS ilifanya shambulizi kali dakika ya 71 baada ya Ziri Hammar kugongeana na Lahmriaimen Lahmri na kupiga shuti la chini chini lililoishia mikononi mwa Manula.

Licha ya JSS kumuingiza Thomas Ulimwengu aliyeshangiliwa sana, bado hawakuweza kupata hata bao la kufutia machozi, huku wachezaji wa timu hiyo wakionekana mara nyingi wakimlalamikia mwamuzi wakihisi kama anawaonea.

Waalgeria pia walifanya mabadiliko dakika 75 kwa kumtoa Ibrahim Farhi na kuingia Mohammed Boulaouidet.

Dakika 87 Simba walifanya mabadiliko ya kumtoa Okwi na kuingia Shiza Kichuya na kuzidi kuwapa presha Waalgeria.

MO DEWJI GUMZO

Kabla ya pambano hilo Mo Dewji alikuwa kivutio uwanjani mara alipoingia na kuufanya uwanja mzima urindime kwa shangwe zilizokuwa zikielekezwa kwake, huku akiwapungia mkono kuonyesha furaha yake.

Hata mabao ya Simba yalipokuwa wakiingia wavuni, Mo Dewji alikuwa akishangilia sambamba na Dk Tulia na Waziri Mkuu sambamba na mabosi wengine wa Msimbazi waliokuwa jukwaani hapo.

MwanaFA, Zitto Kabwe na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe nao walikuwapo uwanjani hapo na Zitto alishindwa kujizuia baada ya Kagere kutupia kambani bao la tatu, kwa kuinuka na kulishangilia huku akiwa amezingirwa na walinzi wake.

MKUDE APEWA MIKOBA

Mfungaji wa bao la kusawazisha katika mchezo wa marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Afrika dhidi ya Nkana FC ya Zambia iliyokufa mabao 3-1, Jonas Mkude aliyekiongoza kikosi cha Simba kushuka katika basi mara walipofika uwanja wa Taifa saa 8:26 mchana.

Uwanjani mashabiki wengi walijitokeza kuiunga mkono timu yao, huku wakiwa na matumaini makubwa Simba kuchomoza na ushindi mnono, huku kukiwa na ulinzi mkali kutoka kwa askari polisi na wale wa Suma JKT.

Simba itaanza tena kujiwinda na mchezo mwingine, ambapo safari hii itasafiri kuifuata AS Vita ya DR Congo, ambapo mchezo huo utachezwa mjini Kinshasa.