Simba, Yanga zakabidhiwa jeshini

Muktasari:

Ratiba inaonyesha JKT Tanzania ndio wenyeji wa mchezo huo na watacheza na Simba Agosti 23 Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, huku Yanga itawakaribisha Ruvu Agosti 28 (Uhuru).

RATIBA ya Ligi Kuu Bara, inaonyesha JKT Tanzani itafungua pazia la msimu ujao na Simba, jambo hilo haliwapi shida badala yake wanaona linapunguza mzigo mzito mbeleni.

Mwanaspoti limezungumza na makocha mbalimbali kuhusu mtazamo wao juu ya ratiba ya msimu ujao, hawajaonyesha kushangazwa na badala yake jambo kuu kwao ni maandalizi.

Kocha wa JKT Tanzania, Mohamed Abdallah ‘Bares’ alisema watafungua dimba na Simba, jambo alilodai halimpi shida kwa madai bora wamalizane nao mapema.

Bares alisema hata wangeikwepa Simba kuanza nao mechi ya kwanza bado wangekumbana nao mbele ya safari, jambo alilodai wanaona watatua mzigo wa kelele mapema. “Ujue timu zenye kelele nyingi bora kumalizana nazo mapema kwani kadri mechi inavyokuwa inaendelea ugumu unaongezeaka zaidi, sisi tumejipanga kufunga kila mechi bila kujali Simba au Yanga,” alisema.

Ratiba inaonyesha JKT Tanzania ndio wenyeji wa mchezo huo na watacheza na Simba Agosti 23 Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, huku Yanga itawakaribisha Ruvu Agosti 28 (Uhuru).

Kwa upande wa Azam FC, wao wataanza na KMC ambao wanatajwa kama daby mpya ya Dar es Salaam, mchezo huo utapigwa Agosti 29 Uwanja wa Uhuru.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila alisema yeye sio muumini wa kulalamikia ratiba anachoamini atacheza na kila timu ambayo ipo ligi kuu na jambo la msingi kwake ni kufanya maandalizi ya msingi. “Kuhusu ratiba siku zote nasema hainisumbui ili mladi mechi zinazotakiwa zimalizike kwa msimu zichezwe na mimi nakuwa tayari kukabiliana na timu inayokuwa mbele yetu.

“Kazi ya kocha nikuandaa timu ya ushindani na sio kuhangaika na ratiba, ingawa kikwazo kitakuja pale mechi zinapokuwa zinasimama simama hiyo ndio kero lakini sio naanza na nani ama namaliza na nani,” alisema.

Naye katibu wa Prisons, Ajabu Kifukwe alisema anaona ratiba ni ya kawaida akidai kama haitakuwa na mabadiliko ya msimu uliopita

“Ingawa bado sijaisoma vizuri, sijaona shida kikubwa waangalie yasije yakatokea ya msimu ulioisha ambao mechi ilipooza na kutokuwa na ladha, hapo ndipo shida inapoweza kutokea na sio vinginevyo,” alisema.