Simba, Yanga yaitajirisha TFF

Muktasari:

  • Yanga ndiyo imeonekana kuumizwa zaidi na adhabu hizo na kujikuta ikilazimika kulipa fungu kubwa la fedha za faini ikifuatiwa na Azam na kisha Simba.

VITENDO vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na vigogo Simba, Yanga na Azam vikiwamo vya wachezaji wao, vimekuwa kama neema kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa namna inavyotajirika kiulaini kwa faini wazotoza kila mara kupitia Kamati zao za Saa 72 na ile ya Nidhamu.

Kamati hizo zimekuwa zikipiga rungu kwa haraka klabu hizo pindi zinapovunja kanuni ya ligi msimu huu hasa kanuni ya 14 inayotoa ufafanuzi wa Taratibu za Mchezo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/2019.

Kwa bahati mbaya, klabu hizo hasa Yanga licha ya kupigwa faini ya fedha, bado ni kama hazijifunzi kitu kwani zenyewe na wachezaji wameendelea kurudia makosa yaleyale.

Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti imebaini ndani ya kipindi cha miezi minne pekee tangu mwaka 2019 uliingie, Yanga, Azam na Simba zimeinufaisha TFF kwa kulipa faini ya Sh 17 milioni kutokana na imani za kishirikina pamoja na kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.

Yanga ndiyo imeonekana kuumizwa zaidi na adhabu hizo na kujikuta ikilazimika kulipa fungu kubwa la fedha za faini ikifuatiwa na Azam na kisha Simba.

Katika fungu hilo la Sh 17 milioni ambalo TFF imevuna kutoka kwa klabu hizo tangu mwaka huu uanze hadi sasa, Yanga imetozwa Sh 11 milioni, Azam Sh 3.5 milioni wakati Simba yenyewe imetozwa Sh 3 milioni.

Rungu la kwanza ambalo Yanga ilipigwa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi iliyokutana Machi 7 lilikuwa ni lile la faini ya Sh 1.5 milioni kwa kosa la kutoingia vyumbani wakati wa ukaguzi na wakati wa mapumziko katika mechi yake dhidi ya JKT Tanzania iliyochezwa Februari 10, 2019 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Kamati hiyo pia iliiadhibu Yanga kwa kuitoza faini ya Sh 6 milioni kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, kutoingia vyumbani na kusababisha wachezaji wakaguliwe kwenye korido, na pia kutotumia njia maalum iliyowekwa kwa ajili ya kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch) katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 16, 2019 katika Uwanja wa Taifa, Dares Salaam.

Lakini pia Yanga ilitozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la mashabiki wake kuingia uwanjani kushangilia baada ya kuibuka na ushindi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Februari 20.

Ikiwa ni baada ya mwezi mmoja tu baafa ya faini hizo, juzi Yanga ilijikuta ikipigwa rungu la faini ya Sh 3 milioni baada ya kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Ndanda iliyofanyika Aprili 4, 2019 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara ikiwa ni kinyume cha Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018.

Azam yenyewe ilianza kwa kutozwa faini ya Sh 3 milioni kwa kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi na kutoingia vyumbani hivyo kusababisha wachezaji wakaguliwe kwenye korido katika mechi yake dhidi ya Simba iliyochezwa Februari 22, 2019 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kama ilivyo kwa wenzake Yanga na Azam, Simba nao hawakuwa salama kwani nao walipigwa rungu na TFF kwa kutozwa faini ya Sh 3 milioni kwa kosa la kuingia uwanjani wakitumia mlango usio rasmi, lakini vilevile kutotumia njia maalum iliyowekwa kwaajili ya kuingia kwenye eneo la kuchezea.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Steven Mnguto alisema vitendo kama hivyo vinatia doa soka la Tanzania nchini na Bodi pamoja na TFF hawatovifumbia macho na wanaandaa mkakati kabambe wa kukomesha siku za usoni.

“Hebu fikiria ligi hii ina mdhamini wa televisheni na inaleta picha gani pale watu wanapoangalia runinga na kuona timu mara zinaruka ukuta au geti, kupita sehemu ambayo sio rasmi na mambo mengine ya kihuni?” Alihoji Mnguto na kuongeza;

“Inaleta picha mbaya. Nasi kama mamlaka inayosimamia ligi hatuwezi kufumbia macho.

Tutahakikisha msimu ujao tunakuwa na kanuni kali zaidi ambazo zitakomesha hayo matendo ili ligi yetu izidi kuwa na thamani na heshima stahiki.”