Simba, Yanga washusha presha ya Kocha Bizimungu

Muktasari:

  • Mwadui ilipata ushindi mfululizo katika uwanja wa nyumbani, ikiishindilia Mtibwa Sugar bao 1-0, Coastal Union mabao 2-1, Biashara United mabao 2-1.

Mwanza. Ushindi katika mechi tatu mfululizo kwa Mwadui FC umempa mzuka kocha wake, Ally Bushiri na kutamba kuwa mechi zilizobaki ni kujipigia tu kwani ameshamalizana na Simba na Yanga.

Timu hiyo ilianza vibaya msimu, lakini sasa imebadilika ikishinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Mtibwa Sugar bao 1-0, Coastal Union mabao 2-1 kisha kushinda mbele ya Biashara United mabao 2-1.

Mwadui imekusanya pointi 33 na kupanda hadi nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu baada ya kucheza mechi 28, huku Yanga wakiongoza kwa alama 61 baada ya kushuka uwanjani mara 25.

Kocha Bizimungu alisema anavutiwa na mwenendo wa kikosi chake kwa jinsi kinavyopambana kila mechi kutokana na kwamba hawana presha baada ya kumalizana na timu kubwa za Simba na Yanga.

Alisema mchezaji ametambua majukumu yao ndio maana wanapokuwa uwanjani ni kushambulia mwanzo mwisho kuhakikisha wanapata mabao mengi ambayo kimsingi ndio yanawapa ushindi.

“Tunashukuru kwa matokeo tunayopata na hii ni kutokana na dhamira yetu ya kufanya vizuri kwa sababu hatuna wasiwasi baada ya kumalizana na timu kubwa zinazowania ubingwa Simba na Yanga, lakini vijana wanajitambua na wanapokuwa uwanjani nawaelekeza kushambulia zaidi kusaka mabao,”alisema Bizimungu.

Aliongeza licha ya kazi nzuri vijana wake wanayoifanya, lakini bado kuna mapungufu madogo madogo yanamuumiza kichwa haswa washambuliaji wake kwa kushindwa kufunga mabao na kwamba anaendelea kuyafanyia kazi.

“Kuna mechi ambayo unaona kabisa lazima tushinde kwa mabao mengi lakini washambuliaji wanakosa kufunga, kwahiyo naendelea kulifanyia kazi suala hilo ili tunapopata nafasi lazima tuitumie vizuri hata kwa kufunga mabao saba,”alisema kocha huyo.