Simba, Yanga wanapiga pesa

Monday January 7 2019

 

By Mwanahiba Richard

KOMBE la Mapinduzi ndio kama mlivyosikia wenyewe, yaani linaendelea kukata mawimbi huo huko Zanzibar kwa timu tisa kutoka Bara na Visiwani zikichuana vikali kusaka ufalme.

Wababe wa Ligi Kuu Bara, Simba, Yanga na Azam FC wanachuana kuonyesha ubabe na wenzao wa Zanzibar ambao ni Chipukizi, KVz, KMKM, Malindi, Mlandege na Jamhuri.

Mashindano haya ambao ni maalumu kwa ajili ya kunogesha kilele cha Siku ya Mapinduzi hapa Januari 12, ingawa kwa msimu huu fainali zake zitapigwa visiwani Pemba.

Mwanaspoti ambalo limeweka kambi visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuhabarisha wasomaji wake kila kinachoendelea, kama kawaida limebaini mambo mbalimbali ikiwemo maisha ya kibabe ya timu za Bara.

 

Simba, Yanga maisha juu

Kwenye mashindano haya bila uwepo wa timu za Simba na Yanga mambo huwa hayajanoga kabisa na ndio sababu kila mwaka zimekuwa zikialikwa kushiriki, ambapo hukinukisha kinoma.

Lakini, kati ya timu ambazo zinatumia gharama kubwa ama kuchota mpunga wa maana kutoka kwa waandaaji basi ni Simba na Yanga.

Iko hivi. Waandaaji huzigharamia timu ambazo zinatoka nje ya visiwa vya Unguja, ambapo kwenye mashindano haya zipo tano.

Gharama ambazo hutolewa ni usafiri, malazi na chakula. Kwa Simba na Yanga kila siku hulipwa Sh 4 milioni kila timu ambapo, kwa siku 13 kila timu hukunja Sh 52 milioni huku jumla kuu kwa timu zote mbili ikiwa ni Sh 104 milioni.

Gharama hizo ni kubwa ukilinganisha na zawadi ya ubingwa inayotokewa ambayo ni Sh 15 milioni, ambayo ni ndogo ikilinganishwa na gharama inazolipwa klabu hizo.

Simba ambayo imekuja na kikosi kizima imefikia Zanzibar View Hoteli ambapo, kwa usiku mmoja gharama yake ni kati ya dola 80, 100 na 130 kwa chumba cha mtu mmoja.

Wakati Yanga wenyewe wamefikia Bububu ambako ni nje ya mji katika hoteli ya Ocean View ambayo mmiliki wake ni mmoja na ile waliyofikia Simba, ingawa Mwanaspoti limetonywa kuwa hoteli ya Yanga bei yake inaanzia dola 60, 80, 100 kwa chumba cha mtu mmoja kutokana na kuwa nje kidogo ya mji yaani mambo ni ‘fire’ kwa timu zilizotoka hasa bara. 

Azam FC wafikia nyumbani

Azam FC ambao wanaogelewa kwenye utajiri wa bilionea wao, Said Bakhresa wenyewe ni kama wamefikia nyumbani tu. Wapo kwenye hoteli ya kisasa ya Verde ambayo inamilikiwa na Bakhresa.

Gharama ya chumba kwa siku kwenye hoteli ni kuanzia dola 250, 300 hadi 700. Habari ambazo Mwanaspoti imeelezwa ni kwamba, matajiri hao wa ligi wao hawajachukuwa mgao kama Simba na Yanga kwani, wanahusika kwenye udhamini wa michuano hiyo ingawa wachezaji na benchi la ufundi imeelezwa wanapewa posho.

 

Chipukizi, Jamhuri

wapanga uswahili

Timu hizo mbili zinatoka Pemba ambapo kwa mujibu wa taratibu za mashindano haya nazo zinapaswa kugharamiwa kama ilivyo kwa Simba na Yanga, mambo ni tofauti kidogo.

Mwanaspoti limeelezwa kuwa gharama kwa timu hizo ni tofauti na zile za Simba na Yanga.

Chipukizi na Jamhuri zenyewe zinalipwa Sh 800,000 kwa kila timu kwa siku ambapo, kwa siku 13 kila mmoja itavuna zaidi ya sh 10 milioni.

Hata hivyo, timu hizo haziweka makazi kwenye hoteli kali kama Simba na Yanga, ambapo zimeibuka na mbinu mpya ya kukodisha nyuma za kawaida na kuzigeuza kuwa kambi kwa muda wanapokuwa kwenye mashindano hayo.

 

Timu za Unguja hamna kitu

Timu za visiwa vya Unguja ambazo ni KMKM, KVZ, Malindi, Mlandege. Hizi timu zipo hapa hapa visiwani Unguja ambapo kwenye mgao huo wa malazi hazimo kabisa.

Hizi timu zenyewe zinagharamiwa na waandaaji usafiri wa kwenda uwanjani na kuwarudisha walipowatoa pamoja na chakula, maji na posho.

Viongozi wa timu hizo wameelezea hisia zao kwamba, ni vigumu kwa timu za Unguja ambazo sio za majeshi kufanya vizuri kwani, hazina vyanzo vya mapato vya kutosha.

Rais wa Mlandege FC, Mbaraka Himid amesema kwamba: “Mashindano ni mazuri na yanasaidia katika kuibua vipaji, lakini kuna changamoto kubwa hasa kwenye malazi.

“Huwezi kufahamu mchezaji anaishi katika mazingira gani na anakula nini usiku baada ya mechi kwani, pesa tunayopewa ni kwa ajili ya chakula cha mchana, waandaaji wanapaswa kufikiria upya.”

000000

 

Advertisement