TASWIRA YA MLANGABOY : Simba, Yanga usajili wa kutisha nje uwanja

Saturday July 27 2019

 

By Andrew Kingamkono

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza ratiba yake ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwa mtindo wa kipekee zaidi msimu huu na kuacha majanga kila kona Afrika.

CAF imetangaza ratiba yake Jumapili iliyopita tofauti na ilivyozoeleka na wengi msimu huu timu zote zitaanzia hatua ya awali isipokuwa kwa Wydad Casablanca, Esperance na TP Mazembe ambao wataanzia hatua ya pili.

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa, Simba ikianza ugenini dhidi UD Songo ya Msumbiji, huku Yanga ikirudishwa kwa Township Rollers ya Botswana kati ya Agosti 9-11 na marudiano itakuwa kati ya Agosti 23-25, 2019.

Kombe la Shirikisho mabingwa wa Kombe la FA, Azam itaanza ugenini dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia huku KMC watakuwa nyumbani kucheza na AS Kigali kati ya Agosti 9-11, 2019 na marudiano itakuwa kati ya Agosti 23-25, 2019.

Tuyaache hayo ya ratiba ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwa sababu bado naamini klabu za Tanzania zina nafasi ya kufanya vizuri katika hatua ya awali.

Wiki hii Taswira inajikita kuangalia ubora wa klabu zetu Simba na Yanga katika vyombo vya habari, lakini inapofika uwanjani mambo yanakuwa tofauti kabisa.

Advertisement

Napitia vichwa vya habari vya michezo tangu mwishoni mwa Mei hadi leo kila siku kumejaa habari njema za usajili na majina ya nyota wapya wa Simba, Yanga, Azam.

Yanga pamoja na kupitia katika ukata mkali msimu uliopita uongozi mpya chini ya Dk Mshindo Msolla ulifanya harambee ya Kubwa Kuliko na kupata fedha za kutoka kufanya usajili wa nyota 10.

Wachezaji waliosajili na Yanga ni pamoja na Issa Bigirimana (APR, Rwanda), Patrick Sibomana (Mukura Victory Rwanda), Mustapha Suleiman (Aigle Noir AC Haiti), Sadney Urikhob (Namibia), Lamine Moro (Ghana).

Wengine ni Ally Mtoni (Lipuli FC), Kassim Khamis Abdallah (Kagera Sugar), Abdulaziz Makame (mchezaji huru), Ally Ally (KMC).

Wakati Yanga ikifanya usajili huo, watani wao Simba wakijivunia jeuri ya fedha ya udhamini pamoja na kufanya vizuri katika mashindano ya CAF wamepata saini za nyota watatu kutoka Brazil, DR Congo, Sudan na Kenya.

Wachezaji waliotua Simba ni pamoja na Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Vieira, Wilker Da Silva, Sharaf Shiboub, Francis Kahata, Deo Kanda, Ibrahimu Ajibu, Gadiel Michael pia wapo Beno Kakolanya, Kennedy Wilson, Miraji Athuman.

Ukiangalia usajili wa klabu hizi mbili kongwe na kishindo za kambi zao huko Afrika Kusini pamoja na Morogoro kwa mpenda soka anajua kutakuwa na ushindani zaidi ndani ya uwanja. Hakuna anayewaza tofauti zaidi ya timu hizi kupata matokeo bora zitakapokuwa zinashuka dimbani kukabiliana na wapinzani.

Pamoja na usajili huu wa kelele nyingi kila kona bado Simba na Yanga zitalazimika kutumia mbinu chafu kusaka ushindi dhidi ya timu dhaifu kabisa katika Ligi Kuu.

Nakwambia usishange Yanga na Simba pamoja na kufanya usajili wa mamilioni bado zitahitaji mbeleko ya TFF na Bodi ya Ligi katika kupanga pangua ya ratiba ya Ligi Kuu ili kutegeneza mazingira ya kushinda mechi zao kiulaini.

Hivi karibuni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alieleza namna alivyochukizwa na viporo vya ligi ya msimu uliokwisha. Kulikuwa na viporo vingi kiasi cha kutibua kabisa ladha ya soka.

“Kwa namna viporo vilivyokuwa vingi, ligi yetu ingeingia hata kwenye kitabu cha maajabu ya dunia, tumelijadili hilo na TFF na Bodi ya Ligi ambao, wamenihakikishia kuwa hilo halitajirudia,” alisema Dk Mwakyembe.

Katika upangaji wa matokeo ya timu kigezo cha timu mmoja kupewa viporo vingi ni ishara ya kuibeba timu nakupanga matokeo. Japo kunakuwa na sababu mbalimbali ambazo zinatajwa kufikia uamuzi huo, lakini kiuhalisia timu husika ni lazima inufaike na ratiba hiyo.

Hiyo tisa kumi ni suala la rushwa katika ligi yetu, sitashanga klabu zetu kongwe Simba na Yanga zikipeana kashfa ya kuhonga wachezaji wa timu ndogo, waamuzi ili kununua ushindi katika mechi zao.

Mara kadhaa tumekuwa tukiona malalamiko hayo kuanzia kwa waamuzi, wachezaji kuhusishwa na upangaji wa matokeo. Kwa kawaida, mpira unaochezwa nje ya uwanja katika ligi yetu umechangia kwa sehemu kubwa klabu zetu kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Wachezaji wa klabu zetu wameshindwa kutegenezwa kwa ushindani kwa timu zote kwa sababu viongozi wamekuwa wakitumia njia za mkato kurahisisha matokeo ya uwanja.

Naamini Watanzania wanataka kupata bingwa wa kweli kwa kucheza uwanjani kwa sababu hiyo itasaidia kuwa na Taifa Stars bora itakayoweza kufanya vizuri katika mashindano ya Afcon.

Kama tutaendelea na ujanjaujanja wa kuucheza mpira nje ya uwanja badala ya uwanjani basi tunaweza kuendelea kuwa nyuma sana kupata timu bora yenye uwezo wa kupata matokeo kwenye anga za kimataifa.

Advertisement