Simba, Yanga rekodi tofauti Ligi Kuu Bara

Wakati Ligi Kuu Bara ikisimama katika mzunguko wa tano, timu nne zinashikilia rekodi tofauti zikiwamo vigogo Simba na Yanga ambazo zitakutana Novemba 7 badala ya Oktoba 18 iliyopangwa awali.

 Mpaka sasa timu zote zimecheza mechi tano, huku Azam FC ikiwa timu pekee ambayo haijafungwa wala kutoka sare ambapo inaongoza msimamo kwa kuwa na pointi 15.

Mbali na Azam FC, Simba na Yanga kila moja imeandika rekodi katika mechi hizo, Simba ikiwa timu pekee iliyofunga mabao mengi tangu kuanza msimu huu kulinganisha na timu nyingine 17 zinazoshiriki ligi hiyo.

Simba, mabingwa watetezi imefunga mabao 14, imefungwa mawili na kujikusanyia pointi 13 baada ya kushinda mechi nne na kutoka sare moja ikifuatiwa na Azam FC yenye mabao tisa.

Kwa upande wake, Yanga imeweka rekodi ya kuwa timu pekee iliyofungwa bao moja tangu kuanza kwa msimu.

Yanga yenye pointi 13 sawa na Simba pia imefunga mabao saba katika mechi hizo, rekodi ambayo mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay anasema ina maana kubwa kuelekea kwenye mechi ya Novemba 7 ya watani hao wa jadi.

“Itakuwa ni vita ya mabeki wa Yanga na washambuliaji wa Simba,” alisema Mayay alipozungumza na Mwananchi, jana.

Alisema pamoja na kwamba kikosi cha Yanga hakijapata muunganiko mzuri kama ilivyo kile cha Simba, lakini uwezo wa mchezaji mmojammoja na mbinu za makocha ndivyo vitaamua mshindi wa mechi.

Safu ya ulinzi ya Yanga imeruhusu bao moja mpaka sasa huku Simba, Azam na Polisi Tanzania zikifuatia kwa kufungwa mabao machache kila moja ikifungwa mabao mawili.

“Mechi ya Simba na Yanga haitabiriki kwani siku zote huwa na uwiano wa 50/50, lakini ukiachana na mechi ya mwisho ambayo Yanga ilifungwa mabao 4-1, msimu huu ina kikosi tofauti hivyo kitakachoamua matokeo siku hiyo ni mbinu za makocha na uimara wa beki ya Yanga na washambuliaji wa Simba,” alisema mchambuzi huyo.

Mbali na rekodi hizo, nayo Mbeya City imejitengenezea rekodi yake ya kuwa timu pekee ya kutoshinda mechi hata moja hadi sasa.

Timu hiyo ya Manispaa ya Mbeya ni ya mwisho katika msimamo ikiwa na pointi moja katika mechi tano ilizocheza ikifuatiwa na Ihefu SC iliyopanda daraja msimu huu ambayo imefungwa mechi tano na kushinda moja huku JKT Tanzania, Coastal Union, Gwambina na Kagera Sugar kila moja imeshinda mechi moja na kutoka sare moja.

“Bado ligi ni mbichi, hivyo tuna nafasi ya kujipanga na kurekebisha makosa,” alisema Juma Mgunda, kocha wa Coastal Union.