Simba, Yanga Moro walilia MO

Muktasari:

  • Dewji 'Mo Dewji' yupo mbioni kununua asilimia 49 za hisa za ummiliki wa klabu ya Simba alitekwa Alhamisi asubuhi na watu wasiojulikana wakati akienda kufanya mazoezi kwenye gym iliyopo katika hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam

Morogoro. Kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini na mfadhili mkuu wa klabu ya Simba SC, jijini Dar es Salaam, Mohamed Dewji (Mo) kumeibua sintofahamu kwa viongozi na wapenzi wa soka mkoani Morogoro.
Wakizungumza MCL Digitalli mkoani hapa, Mwenyekiti wa tawi la Simba SC Mjimpya, Saidi Mkwinda alisema baada ya kupokea taarifa za kutekwa kwa Mohamed Dewji, wanachama na viongozi wa klabu hiyo walishikwa na butwaa na simanzi.
Mkwinda alisema amekuwa akipokea simu zaidi ya 30 kutoka kwa wanachama, mashabiki na wanaoitakia mema Simba wakiuliza juu ya taarifa za kutekwa kwa Dewji, lakini kama uongozi umekuwa hana jibu sahihi juu la tukio hilo.
“Dewji ni mfadhili wa Simba SC na kila mpenzi wa soka anamfahamu na watani zetu (Yanga), lakini tangu taarifa za kutekwa kwake nimekuwa nikipigiwa simu na wanachama, mashabiki kila kona ya mkoa wa Morogoro wakitaka kujua taarifa za mfadhili wetu.”alisema Mkwinda.
Mkwinda alisema wanafikilia kuomba dua ya kumuombea mfadhili wao aweze kupatikana akiwa hai na salama na maadui wasiweze kumdhuru kwa namna yoyote ile ili kuendeleza soka na uchumi wa Tanzania kijumla.
Kwa upande wa Katibu wa Yanga SC tawi la Mjipya, Karimu Omari alisema ni jambo lililowastua wanamichezo kutekwa wa Dewji.
“Hakuna mwanamichezo au raia wa Tanzania anayerufahia jambo la kutekwa kwa Dewji ni tukio ambalo limetustua watu wengi isipokuwa watanzania tuungane na kuomba dua ili aachiwe akiwa hai.”alisema Omari.
Naye shabiki wa soka, Richard Mkude alisema kwa sasa viongozi, mashabiki na wachezaji wanapaswa kutulia ili kuviachia kazi vyombo vya dola kuona wanafanya kazi ya kumsaka Mohamed Dewji na kupatikana akiwa hai na salama.
Mkude alisema kuwa wachezaji bila shaka hawana furaha na hilo sio kwao tu bali kwa wapenda soka na watanzania wengine, lakini niwaombe wasielekeza akili zao moja kwa moja katika tukio la kutekwa Dewji isipokuwa waelekeze akili kwenye mazoezi kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania bara kwani vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi yake.