Simba, Yanga, Azam ni kicheko FA

Muktasari:

  • Mwanaspoti lilizungumza na mabosi wa klabu hizo kupata maoni yao kuelekea mechi hizo ambapo Kaimu Katibu Mkuu wa Simba, Hamis Kisiwa alisema kwamba klabu yao imejidhatiti msimu huu ili wafike mbali tofauti na msimu uliopita.

DROO ya mechi za Kombe la Azam Federation (ASFC) raundi ya tatu imefanyika jana Jumatano, huku vigogo Simba, Azam na Yanga wakipangwa kuanzia nyumbani katika mechi zao zote.

Mabingwa wa kwanza wa taji hilo msimu wa 2015/2016, Yanga imepangwa kuvaana na mshindi kati ya Ihefu au Tukuyu Stars zote za Mbeya katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa.

Ikumbukwe msimu uliopita, Yanga ilikutana na Ihefu FC katika hatua ya 16 Bora na kuing’oa kwa mikwaju ya penalti 4-3 jijini Mbeya.

Simba iliyobeba taji la msimu wa pili yaani 2016/2017 na kutolewa msimu uliopita kwenye hatua kama hii ya 32 na Green Warriors iliyokuwa Ligi Daraja la Pili imepangwa kuanzia nyumbani dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma.

Wakati watetezi Mtibwa Sugar wenyewe nao watakuwa nyumbani Manungu Complex dhidi ya Kiluvya United, huku Azam waliofika nusu fainali msimu uliopita wakipangwa kuvaana na Madini ama Stend ya Babati, kwenye uwanja wa nyumbani wa Azam Complex.

Mwanaspoti lilizungumza na mabosi wa klabu hizo kupata maoni yao kuelekea mechi hizo ambapo Kaimu Katibu Mkuu wa Simba, Hamis Kisiwa alisema kwamba klabu yao imejidhatiti msimu huu ili wafike mbali tofauti na msimu uliopita.

“Tunataka tufanye kweli katika michuano hii, hivyo baada ya ratiba hii tutajipanga na kujua namna tutakavyojiandaa ili kufanya vizuri kwenye mashindano haya kwa mwaka huu,” alisema.

Mratibu wa Azam FC, Philip Alando, alisema kwa upande wao mashindano hayo yana umuhimu mkubwa hivyo hawataki kuitumia nafasi yao vibaya. “Tuna kikosi kizuri, inatulazimu kushinda katika kila mechi ili kujiweka kwenye sehemu nzuri ya mashindano haya, lengo letu ni kuleta upinzani na kuwa mabingwa,” alisema.

Naye Msemaji wa Yanga, Dismas Ten, alisema licha ya kwamba ratiba imetaka kufanana na msimu uliopita, wapo vizuri zaidi.

“Ihefu tulicheza nao msimu uliopita, ila kwa sasa kuna mechi wanacheza kisha ndio anapatikana mshindi.” Mechi za raundi ya tatu zitaanza kuchezwa kati ya Desemba 21-24.