Simba, Nkana ni hesabu tu

Muktasari:

Timu ya Simba inatarajiwa kukutana uso kwa uso na mabingwa wa Ligi Kuu Zambia Nkana Red Devils, katika mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Manzini. Ushindi mnono iliyopata Simba juzi jioni dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland, umeacha maumivu nchini humo na sasa wawakilishi hao wa Tanzania watakutana uso kwa uso na Nkana Red Davils ya Zambia.

Nkana jana ilishinda bao 1-0 mjini Kitwe na katika mchezo wa kwanza iliichapa UD Songo 2-1 ya Msumbiji katika mchezo wa awali mjini Maputo.

Mchezo baina ya miamba hiyo, utamrudisha nyumbani aliyekuwa beki wa Yanga Hassani Kessy anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Nkana.

Simba imefuzu raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1 iliyopata katika mechi mbili za nyumbani na ugenini.

Timu hiyo ilishinda mabao 4-1 katika mechi ya kwanza Dar es Salaam kabla ya juzi kuirarua Mbabane 4-0. Mabao ya Cletous Chama (mawili), Emmanuel Okwi na Meddie Kagere yalinogesha ushindi wa Simba.

Simba na Nkana zinakutana zikiwa ni klabu kongwe katika soka, Simba ilianzishwa mwaka 1936 wakati Nkana 1935 na jambo la kufurahisha timu zote mbili zinavaa jezi nyekundu.

Mchezo huo utakuwa wa kulipa kisasi kwa Simba ambayo ilinyukwa na Nkana mwaka 2002 walipokutana kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa mjini Kitwe, Nkana ilishinda mabao 4-0 na ziliporudiana Dar es Salaam, Simba ilishinda 3-0. Nkana ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.

Lakini Simba ya sasa ni ya kuotea mbali kwa kuwa inajivunia ubora wa safu ya kiungo ikiungozwa na Mzambia Chama na ushambuliaji John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Nayo Nkana inatambia nyota watatu tegemeo ambao ni mhimili wa matokeo mazuri inayopata akina Walter Bwalya, Kelvin Mubanga na Chisamba Lungu.

Tangu mwaka 1974, Simba imeshinda mara tatu kati ya michezo mitano iliyocheza dhidi ya timu za Zambia katika mashindano ya Afrika.

Mwaka 1974, Simba ilitoa Green Buffaloes kwa jumla ya mabao 3-1 katika Kombe la Mabingwa Afrika. Awali, ilishinda 2-1 dhidi Buffaloes kabla ya kuilaza bao 1-0.

Mwaka 1976, Buffaloes iliing’oa Simba kwa jumla ya mabao 4-2, mchezo wa kwanza Simba ilichapwa 3-2 na ziliporudiana ilifungwa bao 1-0.

Simba ilirudi Zambia mwaka 1995 na kufanikiwa kuitoa Power Dynamos kwa penalti 3-4 baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini kutoka sare ya bao 1-1 hivyo matokeo ya jumla kuwa 2-2 kabla ya kutumika kikwaju ya penalti.

Mwaka 2004, Simba ilitolewa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Zanaco baada ya kuchapwa jumla ya mabao 3-2. Mchezo wa kwanza  Simba ilishinda 1-0, lakini mechi ya marudiano Zanaco ilishinda 3-1 na kusonga mbele.

Ushindi wa kishindo iliyopata Simba unaweza kuwa kichocheo cha Simba kupata matokeo mazuri katika mchezo wake na Nkana hasa ubora wa kikosi cha Kocha Patrick Aussems.

Hakuna aliyetarajia kama Simba ingepata ushindi huo kutokana na rekodi na ubora wa kikosi cha Mbabane katika mashindano ya kimataifa.

Uimara wa kikosi kipana unaweza kuwa chachu ya Simba kuanza vyema mchezo wa kwanza ambao utapigwa Desemba 14, 15 na 16 nchini Zambia kabla ya kurudiana Desemba 21 jijini Dar es Salaam.

Aussems anaweza kuendeleza mbinu aliyotumia kuing’oa Mbabane kwa ushindi bila shaka ataitumia katika mchezo dhidi ya Nkana.

Akizungumza na gazeti hili jana, Aussems alisema mbinu pekee aliyotumia kuizima Mbabane ni kucheza soka ya kufunguka licha ya kutangulia kupata ushindi mzuri nyumbani.

Aussems alisema Mbabane ilitarajia Simba itacheza mchezo wa kujilinda kwa kuwa ilikuwa na mtaji wa idadi kubwa ya mabao iliyopata katika mchezo wa kwanza.

“Nilijua nina timu imara yenye wachezaji wenye uwezo mzuri wa kucheza soka ya kufunguka. Pia nina vijana wanaojitambua wanaoweza kumiliki mpira, hivyo sikuwa na wasiwasi na mbinu niliyokuwa nimeandaa katika programu yangu,” alisema Aussems.

Kocha huyo alisema Mbabane ilipoteza mwelekeo katika mechi zote mbili kwa kuwa haikuwa na wachezaji wenye viwango bora vya kushindana na mastaa wake.

"Tulidhibiti eneo la kiungo tukatengeneza nafasi. Unapokuwa na timu kama Simba kitu pekee unachotakiwa kukifanya ni kuwa mbunifu na kujua kutumia ubora wa wachezaji ulionao,” aliongeza Aussems.

Ubora wa viungo James Kotei, Jonas Mkude na Cletous Chama ulikuwa mwiba kwa Mbabane ambayo ilishindwa kufurukuta na kutoa fursa kwa Simba kutawala mchezo.