Simba, Mtibwa ni mipango tu

Friday December 7 2018

 

By CHARLES ABEL

WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya Afrika, Simba na Mtibwa Sugar wamefuzu raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba ikishiriki kwa mara ya kwanza Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2013 waliposhiriki mara ya mwisho na kutolewa kwa aibu ya Recreativo do Libolo ya Angola ilifuzu kwa kuing'oa Mbabane Swallows kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1.
Ikiwa na ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa kwanza nyumbani, Simba ilienda kuwashindiliwa wapinzani wao kwao eSwatini kwa mabaoa 4-0 na kusonga mbele, wakati Mtibwa katika Kombe la Shirikisho waliing'oa Northen Dynamo ya Shelisheli.
Mtibwa walianza na ushindi wa mabao 4-0 nyumbani kabla ya Jumanne iliyopita kushinda tena ugenini baoa 1-0 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 5-0.
Ushindi huo umezifanya Simba sasa kuvaana na Nkana ya Zambia iliyoitoa UD Songo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-1, huku Mtibwa wakipangwa kupambana na KCCA ya Uganda ambayo ilipangwa kuanzia raundi hiyo bila kucheza raundi za awali.
Mwanaspoti linakuletea baadhi ya dondoo muhimu kuhusiana na timu pinzani ambazo Simba na Mtibwa wanakwenda kukutana nazo kwenye raundi inayofuata na jinsi wa wawakilishi wetu wanavyotakiwa kujipanga tu ili kila kitu kiwe freshi.
Simba kama itaing'oa Nkana itafuzu makundi moja kwa moja na kurejea rekodi yao ya mwaka 2003 walipoivua taji Zamalek na kutinga hatua hiyo ikifuata nyayo za Yanga waliokuwa wa kwanza kwa timu za Tanzania kucheza hatua hiyo ya makundi.
Mtibwa wao waliitoa KCCA watakuwa wamesaliwa na hatua moja ya kucheza playoff na timu zitakazotupwa kutoka Ligi ya Mabingwa ili kuwania kucheza makundi wakifuata ilichokifanya Yanga mwaka 2016 na mwaka huu katika michuano hiyo.

KCCA UGANDA
Thamani ya kikosi
Kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com, thamani ya kikosi cha KCCA ni Pauni 500,000 (zaidi ya Shilingi 1.5 bilioni)

Nyota wa kuchungwa
Ndani ya kikosi cha wababe haio wa Uganda nyota wa kuchungwa zaidi ni kiungo mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Uganda ya Vijana U23, Allan Okello.
Okello mwenye umri wa miaka 19, ndiye mpishi mkuu wa mabao ya KCCA ambayo ilimpandisha akitokea kikosi chao cha vijana mwaka jana.
Nyota huyo anayetumia hasa mguu wa kushoto ni mzuri katika kupasua ukuta wa timu pinzani, kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao na kiwango chake bora kimemfanya atajwe katika orodha ya wachezaji watatu wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa Uganda mwaka 2018.
Katika Ligi Kuu ya Uganda msimu huu, Okello amefunga mabao matatu huku pia akifunga moja kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Mbali na Okello, wachezaji wengine wa kuchungwa ni mshambuliaji Patrick Kaddu, kiungo mshambuliaji Jackson Nunda na beki wa kati na nahodha wa timu hiyo, Timothy Awany ambao wamekuwa wakifunga mabao muhimu ya KCCA.

Uimara wao
KCCA ni timu inayojua vyema kutumia vizuri mipira ya adhabu ndogo, krosi na kona katika kufunga mabao.
Ikiwa safu ya ulinzi ya Mtibwa itafanya makosa yatakayopelekea KCCA ipate aina hiyo ya mipira basi watajiweka matatizoni.
Lakini pia KCCA wana safu imara ya ulinzi ambayo imekuwa hairuhusu sana mabao hasa inapokuwa nyumbani.
Katika mechi 10 za mwisho za kimataifa walizocheza Uwanja wa nyumbani, KCCA wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne tu huku wakifunga mabao 14. Wameibuka na ushindi mara nane, kutoka sare moja na kupoteza mmoja.

Udhaifu
KCCA wamekuwa na udhaifu wa kucheza soka la kufunguka pindi wanapokuwa ugenini jambo ambalo limepelekea wawe wanapoteza idadi kubwa ya mechi za ugenini.
Katika mechi 10 za mwisho ugenini za kimataifa, timu hiyo imefungwa mechi tisa, imeibuka na ushindi mara moja huku ikiwa haijawahi kushinda. Imefunga mabao nane na nyavu zake kutikiswa mara 22.

Uwanja- StarTimes Lugogo
Timu hiyo inautumia Uwanja wa StarTimes uliopo Lugogo kwa ajili ya mechi zake inazocheza ikiwa nyumbani. Uwanja huo ni wa nyasi bandia na ulijengwa mwaka 1957.

Kocha-Mike Mutebi
KCCA wanaongozwa na Mike Mutebi, muumini wa soka la kuvutia na kushambulia na miongoni mwa walimu ambao wanapendelea kutoa nafasi kwa vijana wadogo.

Kikosi kilivyo
Makipa:
Tom Ikara, Charles Lukwago na Jamil Malyamungu
Mabeki
Bernard Muwanga, Timothy Awany, Mustafa Kizza Peter Magambo, Herbert Achai, Walter Ochora, Filbert Obenchan, Eric Ssenjobe, Hassan Musana, Muwadda Mawejje na Lawrence Bukenya.
Viungo
Nicholas Kasozi,Jackson Nunda, Steven Sserwadda, Mike Mutyaba, Muzamiru Mutyaba, Ibrahim Sadam Juma, Isaac Kirabira, Julius Poloto, Gift Ali na Allan Okello
Washambuliaji
Patrick Kaddu, Musa Esenu, Allan Kyambadde

NKANA FC ZAMBIA
Thamani ya kikosi
Kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com, thamani ya kikosi cha Nkana ni Pauni 725,000 (Zaidi ya Shilingi 2.1 bilioni)

Kikosi chake
Makipa
Allan Chibwe, Kelvin Malunga, Moses na Mapulanga
Mabeki
Ben Adama Banh, Hassan Kessy, Musa Mohammed, Richard Ocran, Gift Zulu, Laison Thole, Given Sinyangwe na Joseph Musonda.
Viungo
Duncan Otieno, Shadrick Malambo, Kelvin Kampamba, Harrison Musonda Chisala, Jacob Ngulube, Shadrick Musonda, Freddy Tshimenga, Yannick Kalenga, Bwalya Kasonde na Simon Bwalya.
Washambuliaji
Walter Bwalya, Ronald Kampamba na Festus Mbewe.
Katika kikosi chao, wana nyota watano wa kigeni ambao ni mabeki Hassan Kessy (Tanzania), Richard Ocran (Ghana), Ben Adama (Ivory Coast), Musa Mohammed (Kenya) pamoja na viungo Duncan Otieno (Kenya) na Yannick Kalenga (DRC).

Nyota wa kuchungwa
Hapana shaka mshambuliaji Walter Bwalya aliye nahodha wa wa timu hiyo ndiye mkali zaidi katika mwaka 2018, mchezaji huyo mwenye uraia wa Zambia na DRC ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 11 katika mechi 27 za Ligi Kuu nchini humo.
Bwalya anayecheza kama mshambuliaji wa kati ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya vichwa na pia anatumia miguu yote vizuri huku akiwa na sifa ya ziada ya uwezo wa kuwatoka walinzi wa timu pinzani.

Uimara
Nkana kama ilivyo kwa timu nyingine za Zambia au Kusini mwa Afrika, inacheza soka la pasi fupifupi ambalo limekuwa likiisaidia ikae na mpira kwa muda mrefu ambalo limekuwa likizifanya timu pinzani ikose nafasi ya kumiliki mpira na kuwashambulia mara kwa mara.

Udhaifu
Soka la kasi inaweza kuwa silaha kubwa kwa Simba kuwamaliza Nkana Red Devils kutokana na timu hiyo kuwa na safu ya ulinzi inayoundwa na wachezaji ambao mara kwa mara hushindwa kuhimili vishindo vya timu zenye washambuliaji wenye spidi.

Uzoefu
Kama ilivyo kwa Simba, Nkana nao walipita kipindi kirefu bila kushiriki mashindano ya kimataifa ambapo walirudi rasmi mwaka huu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miaka minne tangu waliposhiriki mara ya mwisho mwaka 2014.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliyomalizika, walitolewa kwenye hatua ya awali na CR Belouizdad ya Algeria kwa kipigo cha jumla cha mabao 3-1.
Mafanikio yao makubwa ni kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2014 waliposhika nafasi ya tatu.
Uwanja unaotumiwa na timu hiyo ni  Nkana Stadium unaoingiza mashabiki wanaokadiriwa kutozidi 10,000 na timu hiyo kwa sasa inadhaminiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya  Mopani Copper Mines

Rekodi yao na Simba
Timu hizo zitakutana kwa mara ya tano na ya sita katika mashindano ya kimataifa baada ya kufanya hivyo mwaka 1994 na 2002.
Mwaka 1994 walikutana mara mbili kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika ambapo Nkana aliibuka na ushindi wa jumla wa mabao 4-3 ambapo mechi iliyochezwa Zambia walishinda mabao 4-1 na walipokuja nchini Simba walishinda 2-0.
Mwaka 2002, walikutana kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mchezo wa kwanza Nkana walishinda kwao mabao 4-0 na walipokuja Tanzania, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 ingawa hayakutosha kuwavusha.
Ikumbukwe walipokutana mwaka 1994, Simba ilikuwa inadhaminiwa na Azim Dewji na walipokutana mwaka 2002, Simba ilikuwa chini ya udhamini wa Mohammed Dewji ambaye ana undugu na Azim
Safari hii tena wanakutana huku Simba ikiwa chini ya mwekezaji ambaye ni Mohammed Dewji aliyeonjeshwa shubiri na Zanaco mwaka 2002.

Advertisement