Simba, Mtibwa hesabu ugenini

Muktasari:

Mtibwa inayoshiriki Kombe la Shirikisho na Simba Ligi ya Mabingwa Afrika, zipo kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele zikihitaji sare au ushindi wa namna yoyote ili kuingia raundi ya kwanza ya mashindano hayo ya Afrika.

Manzini, Swaziland. Hesabu na maandalizi mazuri nje na ndani ya uwanja huenda zikawa sababu kuu ya kuzipatia matokeo mazuri Simba na Mtibwa Sugar ugenini leo ili zivuke hatua inayofuata ya mashindano ya kimataifa.

Mtibwa inayoshiriki Kombe la Shirikisho na Simba Ligi ya Mabingwa Afrika, zipo kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele zikihitaji sare au ushindi wa namna yoyote ili kuingia raundi ya kwanza ya mashindano hayo ya Afrika.

Ushindi wa mabao 4-0 iliyopata Mtibwa dhidi ya Northern Dynamo ya Shelisheli na mabao 4-1 iliyovuna Simba ilipovaana na Mbabane Swallows ya Eswatin (zamani Swaziland), unaziweka timu hizo katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Matokeo hayo yameziweka kwenye wakati mgumu timu pinzani ambazo wanakutana nazo leo kwa kuwa zinahitaji kupata ushindi mnono ili kuwatupa nje wapinzani wao.

Hata hivyo pamoja na kuwa katika mazingira mazuri ya kufanya vyema, wawakilishi hao wa Tanzania Bara wanapaswa kuingia uwanjani kwa tahadhali na umakini wa hali ya juu ili kutimiza malengo yao.

Katika michezo hiyo miwili ambayo timu hizo zinacheza, Simba ndiyo inapaswa kujipanganga na kuingia kwa tahadhari ya hali ya juu zaidi kulinganisha na Mtibwa.

Simba kama ilivyo kwa timu nyingine za Tanzania, haifanyi vizuri inapocheza ugenini, hivyo inapaswa kuingia katika mchezo wa leo ikiwa na umakini mkubwa kutokana na ubora wa Mbabane.

Kukosa umakini na makosa binafsi ya safu ya ulinzi, mara kwa mara ndiyo huwa sababu kuu kwa Simba kushindwa kuonyesha makucha inapocheza ugenini na kujikuta ikichezea vichapo mara kwa mara.

Simba imeruhusu mabao 18 ya kufungwa katika mechi 10 za mwisho za kimataifa ilizocheza ugenini, matokeo ambayo kwa makadirio yanaifanya timu hiyo kuruhusu mabao mawili katika kila mchezo.

Katika mechi 10 ugenini ilizocheza miaka ya hivi karibuni, Simba imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Gendarmarie Nationale ya Djibout kwa bao 1-0 huku ikitoka sare ya bila kufungana mara mbili na Elan Club (Comoro) pia Al-Masry (Misri) na iliyobaki yote walipoteza.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems aliliambia gazeti hili jana kuwa matokeo ya ushindi katika mchezo wa kwanza hayawezi kutoa fursa kwao kubweteke.

“Angalia tuna timu imara ambayo inajua inachokifanya. Tuko hapa kutafuta matokeo bora ili tusonge mbele, tumekubaliana timu nzima tusahau matokeo yaliyopita.

“Hakuna majeruhi kwa wachezaji wote waliopo hapa nafurahi kuona maandalizi ya timu tangu tumefika hapa yako sawa. Kiufundi hatuwezi kupunguza washambuliaji tujaze mabeki, tukifanya hivyo itakuwa ni sawa na kuwaambia wapinzani wetu waje watushambulie,” alisema Aussems.

Hata hivyo, Aussems hakusita kueleza hofu yake katika nafasi ya beki ya kulia ambako atamkosa mchezaji wake nyota Shomari Kapombe.

“Tunatarajia mashabiki watakuja ingawa siyo kwa idadi kubwa kutokana na mchezo kuchezwa siku ya kazi, hata mashabiki wa Mbabane hatudhani kama watakuja wengi kutokana na matokeo yaliyopita,” alisema Meneja wa Uwanja wa Mavuso Mkhantjwa.

Kwenye Uwanja wa Stade Linite Shelisheli, Mtibwa itakuwa na kazi nyepesi mbele ya Northern Dynamo ya Shelisheli, baada ya kuibuka na ushindi mnono.

Mtibwa kazi kubwa iliyonayo ni kuongeza umakini katika safu ya ya ushambuliaji ili kupata ushindi wa ugenini utakaofanya iandike rekodi kwa kuwa tayari ni kama imejihakikishia kucheza hatua inayofuata.

Rekodi inaonyesha Mtibwa imefunga mabao sita katika mechi sita ilizocheza ugenini ikiwa na wastani wa bao moja kwenye kila mchezo jambo linalowaweka sawa wachezaji kisaikolojia.