Simba, Mazembe shoo ya kibabe

Muktasari:

Wakati timu hizo zikipambana leo, Simba inaonekana hatari zaidi mwishoni mwa kipindi cha kwanza, na katikati ya kipindi cha pili.

Dar es Salaam. Wakati Simba ikicheza na Tout Puisant Mazembe leo, bilionea wa Wekundu wa Msimbazi, Mohammed Dewji amewatoa hofu mashabiki kwa kuwaambia waujaze uwanja kwani ushindi upo.

Simba inaikabili TP Mazembe ya DR Congo leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaonza saa 10:00 jioni.

Zilivyo Simba na Mazembe

Wakati timu hizo zikipambana leo, Simba inaonekana hatari zaidi mwishoni mwa kipindi cha kwanza, na katikati ya kipindi cha pili.

Katika michezo yao mitatu waliyocheza nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi, Simba ilishinda mechi zote lakini katika mabao sita waliyofunga mawili waliyafunga mwishoni mwa kipindi cha kwanza na mengine mawili katikati ya kipindi cha pili.

Mabao hayo ambayo waliyafunga mwishoni mwa kipindi cha kwanza ni kuanzia dakika ya 30 hadi 45 na yalikuwa mabao ya Emmanuel Okwi dakika tatu za nyongeza baada ya 45 dhidi ya JS Saoura na lingine lilifungwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyefunga kwenye mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya AS Vita dakika ya 36.

Mabao mawili waliyofunga Simba katikati ya kipindi cha pili ni kati ya dakika 60 hadi 75 yalifungwa yote na Meddie Kagere, moja ni kwenye mchezo dhidi ya Al-Ahly na lingine lilikuwa bao la tatu dhidi ya JS Saoura.

Mabao mengine mawili ya Simba yalifungwa dakika ya 52 na Kagere katika mchezo dhidi ya JS Saoura wakati lingine lilifungwa dakika ya 90 na Clatous Chama katika mchezo na AS Vita.

Wapinzani wao TP Mazembe wameonekana ni hatari zaidi dakika 15 za mwisho za kila kipindi.

Mazembe wamefunga mabao yao kati ya dakika ya 30 hadi 45 na 75 – 90 yakiwemo mabao matano kati 13 waliyopachika kwenye hatua ya makundi.

Idadi ya mabao 13 waliyofunga TP Mazembe ambao waliruhusu pia nyavu zao kuguswa mara nne, inaendana na mabao ambayo Simba iliruhusu katika hatua ya makundi.

TP Mazembe ambao ni mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo zamani lilikuwa ikiitwa Kombe la Washindi wamekuwa wakimtegemea zaidi straika wao, Trésor Mputu ambaye hadi sasa ana mabao manne sawa Jackson Muleka.

Simba wao wanamtegemea Meddie Kagere mwenye mabao sita na Mzambia Clatous Chama (5) kwenye orodha ya wafungaji kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu wa 2011, Simba iliondolewa na TP Mazembe kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 6-3.

Katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, Simba iliyokuwa na Mbwana Samatta ambaye baadaye alijiunga TP Mazembe walilazwa Taifa kwa mabao 3-2 na katika mchezo wa marudiano walichapwa tena Lubumbashi mabao 3-1.

Simba inatakiwa kujichunga katika eneo lao la ulinzi linaloongozwa na kipa, Aishi Manula, mabeki Pascal Wawa na Erasto Nyoni ili wasiruhusu mabao ya kizembe kwenye mchezo huo.

Hatua ya makundi

Katika hatua hiyo ambayo Simba wametokea Kundi D na TP Mazembe (C) hazijapoteza mchezo hata mmoja kati ya mitatu ambayo kila mmoja alikuwa akicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Simba walianza kampeni zao za kushinda michezo ya nyumbani katika hatua hiyo ya makundi kwa kuilaza, JS Saoura mabao 3-0, Al-Ahly bao 1-0 na AS Vita mabao 2-1.

TP Mazembe waliifunga Ismaily mabao 2-0 iliyokuwa dhaifu kwenye kundi hilo, wakaichapa Club Africain kwa mabao 8-0 kabla ya kuichapa CS Constantine mabao 2-0.

Upande wa michezo yao ya ugenini sio Simba wala TP Mazembe ambao waliibuka na ushindi hivyo hii inaonyesha jinsi gani timu hizo mbili zilivyo na nafasi kila mmoja kumuadhibu mwenzake nyumbani.

Kocha wa zamani wa Yanga na Azam, Hans van der Pluijm ambaye yupo Ghana, amedai kuifahamu vizuri TP Mazembe hivyo Simba wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwenye ukabaji.

“Kukiwa na uzembe kwenye ukabaji wanaweza kutoa nafasi kwa Mazembe kuweza kuwaletea madhara kwani wana timu nzuri na yenye wachezaji wenye uzoefu kama Simba wakifanikiwa kwenye hilo basi wanaweza kushinda mchezo huo,” alisema Pluijm.

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema kwa ugumu wa mchezo huo ulivyo washambuliaji wa Simba wanatakiwa kuwa makini mno na kila nafasi ambayo watakuwa wanatengenezewa.

“Kama mnauwezo wa kufunga hata mabao matano ni vema yafungwe kwa sababu mchezo wa ugenini huwa tofauti na nyumbani hasa kwenye mashindano makubwa kama haya, wakizichezea nafasi inaweza kuwaweka kwenye mazingira mabaya katika marudiano, DR Congo,” alisema Chambua.

MO aita mashabiki Taifa

Bilionea wa Simba Mo ametaja siri ya mashabiki kuujaza uwanja kuwa ni kuwapa hofu wapinzani wao na hivyo kuimaliza TP Mazembe kutoka DR Congo mapema tu.

Dewji ametamba kuwa ikiwa mashabiki wa klabu hiyo na Watanzania wataujaza Uwanja wa Taifa kuna uwezekano mkubwa TP Mazembe wakapokea kichapo kama ilivyokuwa wa JS Saoura, Al Ahly na AS Vita.

Hawaachi Kagere, Chama

MO alisema klabu hiyo haina mpango wa kuwaacha mastaa wake, Meddie Kagere na Clatous Chama hata zikija ofa za namna gani mezani.

Dewji alisema Simba inataka kushindana kimataifa hivyo kupoteza wachezaji wazuri na muhimu ni hasara kwao huku akisisitiza kuwa wachezaji hao wawili bado wana mikataba na klabu hiyo.

Ujenzi wa Uwanja

Dewji alisema hatua ya mwanzo ya ujenzi wa uwanja huo itakamilika Mei mwaka huu.

Alisema kuchelewa kukamilika kwa zoezi la uwekaji nyasi kwenye uwanja huo ambalo ilikuwa likamilike Februari kulitokana na klabu hiyo kutozipata nyasi zake bandia kwa wakati kwa sababu ya masuala ya kisheria.

“ Mungu amesaidia nyasi zetu zimeshatoka na tumeshamalizana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) waliokuwa wanazishikilia.