Simba: Kwani sisi na wao bado ngapi!

Muktasari:

  • Mibao ya Chama, mipasi ya Luis balaa tupu
  • Luis huu ni msimu wake wa pili akiwa na Simba baada ya kusajiliwa na mabingwa hao katika dirisha dogo la Januari mwaka huu. Alitengeneza asisti tatu katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Biashara

DAKIKA 90 za mchezo dhidi ya Biashara United juzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini, zilitosha kudhihirisha kwa nini Simba inapaswa kufanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha inaendelea kubakia na kiungo wake mshambuliaji Clatous Chama kutoka nchini Zambia.

Lakini mashabiki wao wakawakejeli wenzao wa Yanga wakihoji; “Kwani sisi na nyie bado ngapi? Tukutane hapa hapa kwa Mkapa.” Walikuwa wakimaanisha zimebaki mechi ngapi kabla ya mechi ya watani kutokana na kiwango cha mechi ya juzi na ubora wa mastaa wao haswa Chama.

Kitendo cha kiungo huyo kushiriki moja kwa moja katika mabao matatu kati ya manne ambayo Simba ilipachika katika mchezo huo yakichagizwa na kiwango bora kilichoonyeshwa na Chama mwenye umri wa miaka 29 ni uthibitisho tosha wa umuhimu na mchango mkubwa ambao nyota huyo amekuwa akiutoa tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2018.

Katika mchezo huo ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0, Chama alipachika mabao mawili na kupiga pasi ya mwisho kwa bao la nne lililopachikwa na Chris Mugalu raia wa DR Congo.

Haikuishia katika kuhusika na mabao hayo matatu tu bali pia Chama alionyesha uwezo mkubwa wa kuvunja ukuta wa Biashara, kutengeneza nafasi na pia kuichezesha timu na hilo kwa kiasi kikubwa lilichangiwa na mambo manne ambayo yamekuwa yakimtofautisha na wengine nayo ni utulivu, maamuzi sahihi na ya haraka, mikimbio sahihi na pia muono wa wapi apeleke mpira katika muda gani.

Muunganiko wa utulivu, maamuzi sahihi na ya haraka pamoja na mikimbio sahihi ndivyo vilimfanya Chama aweze kufunga mabao mawili katika mchezo huo ambayo yote yalitokana na pasi za Luis Miquissone.

Katika bao la kwanza, wakati Miqussone akiingia na mpira kuelekea lango la Biashara United pembeni kulia, Chama alikimbia kwa haraka ndani ya boksi la Biashara na kusimama katika eneo ambalo hakuwa amedhibitiwa na mchezaji yeyote wa timu hiyo ya Mara na bila kutuliza aliiunganisha mpira kwa mguu wake wa kulia kwenda upande wa kulia wa kipa wa Biashara, Daniel Mgore ambaye angeweza kuwa na nafasi kubwa ya kuuokoa ikiwa ungepigwa upande wake wa kushoto.

Mikimbio na uwezo wa Chama kusimama kwenye nafasi sahihi vilionekana tena kwenye bao lake la pili ambalo safari hii lilipikwa kupitia katikati ambapo alipenyezewa pasi na Miquissone na kutokana na utulivu wake, badala ya kuunganisha moja kwa moja alimhadaa beki mmoja wa Biashara pamoja na kipa wao na kuupitisha mpira kushoto kwa kipa Mgore ambaye wakati huo alidhania Chama ataupitisha kulia kwake kama ilivyokuwa kwa bao la mwanzo.

Lakini pia muono wa kujua wapi apeleke mpira na katika nyakati gani pamoja na uamuzi wa haraka ndivyo vilichangia apike bao la tatu kwa kupiga kwa kisigino mpira ambao aliupokea kutoka kwa Bernard Morrison, ambapo ulifika vyema mguuni kwa Chris Mugalu aliyeujaza wavuni.

UIMARA, UBORA WA SIMBA

Tofauti na timu nyingi za Ligi Kuu, Simba inaonekana kuwa na muunganiko mzuri wa kitimu na hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na kuwa na kundi kubwa la wachezaji ambao wamekaa pamoja ingawa pia wapya waliosajiliwa wameonyesha ubora wao kwa kuzoea mapema mazingira mapya ndani ya timu hiyo.

Timu nzima imekuwa ikishiriki katika kujenga mashambulizi lakini pale mpira unapopotea, kila mchezaji amekuwa akisaidia kuhakikisha unarudi katika umiliki wao.

Pasi zimekuwa zikifika katika mahali sahihi kwa wakati na pindi mchezaji mmoja anapokuwa na mpira, anakuwa na machaguo mengi ya sehemu sahihi pa kuupeleka kutokana na kuzungukwa na wenzake jambo linalowarahishia kazi pindi wanapojenga mashambulizi ama wanapojilinda.

Namna walivyofunga mabao yao manne ambayo yote yalitokana na pasi zilizopigwa na zaidi ya wachezaji wawili, ni ishara tosha ya muunganiko wa kitimu ambao Simba wamekuwa nao ukichagizwa na ubora wa mchezaji mmojammoja.

Na hilo halijaja kwa bahati mbaya bali ni jambo amalo wamekuwa wakilifanyia kazi mazoezini. Ikumbukwe siku mbili kabla ya mechi ya juzi, Simba ilikuwa ikifanyia kazi mbinu ya kushambulia kupitia katikati kwa kupiga pasi za kupenyeza ambayo ndio iliwapa mabao matatu kati ya manne waliyofunga.

MUGALU AKOLEZA VITA

Ndani ya 13 tu alizocheza, Chris Mugalu alipachika bao moja kati ya nafasi mbili nzuri alizopata akiwa ndani ya eneo la hatari la timu pinzani.

Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na Simba kutoka Lusaka Dynamos ya Zambia, hakucheza mechi mbili za mwanzo dhidi ya Mtibwa Sugar na Ihefu na juzi aliingia kuchukua nafasi ya Medie Kagere ambaye alipachika bao pia.

Kitendo cha nyota hao kufunga kila mmoja, ni wazi kwamba kinazidi kuliweka katika presha kubwa benchi la ufundi la Simba chini ya kocha, Sven Vandenbroeck ambalo limekuwa likipendelea kumtumia zaidi John Bocco katika mfumo wa 4-2-3-1 ambao huwa wanaanza na mshambuliaji mmoja.

Uwezo wa wawili hao kufunga mabao pengine unaweza kumlazimisha Sven abadili mfumo na kujaribu kuwaanzisha washambuliaji wawili au wote watatu kwani kila mmoja ameonyesha uwezo wa kufunga.

ASISTI ZA LUIS

Luis Jose alihusika kwenye kutengeneza mabao matatu ya Simba. Alikuwa kwenye fomu yake na alifanya kile alichotakiwa kukifanya kuipa ushindi Simba na kuongeza thamani yake mbele ya mashabiki.

Mchezaji huyo ambaye ambaye maranyingi hupenda kupiga misele kwa kutumia baiskeli yake Jijini Dar es Salaam,aliwalaza Biashara na viatu.

SVEN AFUNGUKA

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema; “Nimeridhishwa na kiwango na kila kitu cha mechi tulichoonyesha katika mchezo.Nadhani hiyo ndio nguvu ya timu yetu. Kila mmoja anaweza kufunga na anaweza kuzuia na inadhihirisha.

Hatuna mtu mmoja lakini yeyote anaweza kufunga na yeyote anaweza kupiga pasi ya mwisho. Mwisho wa siku tunafanya chaguo kwa kile tunachokiona mazoezini kwa kuangalia nani atatengeneza balansi katika kuzuia na kushambulia. Inawezekana nikapanga mshambuliaji mmoja, wawili, watatu au hata nisipange kabisa,” alisema Vandenbroeck.

“Chama kama ataendelea kuonesha uwezo kama aliokuwa nao sasa katika mashindano ya kimataifa ambayo tunakwenda kushiriki tutakutana na ushindani mkubwa wa timu nyingine nyingi ambazo zitakuwa zikimuhitaji,” alisema.

“Kwangu natamani kumuona Chama akiendelea kubaki hapa Simba lakini mwenye maamuzi ya mwisho ni yeye mwenyewe pamoja na Bodi ya Wakurugenzi pale watakapokuwa wamekubaliana katika masuala yao ya kimaslahi na mkataba,”aliongeza na kufafanua maingizo mapya manne kwenye kikosi cha juzi.

Wachezaji hao walioanza ni, Pascal Wawa aliyechukua nafasi ya Kennedy Juma, Gerson Fraga aliyeanza kabla ya kutolewa baada ya kuumia na kuingia, Said Ndemla walichukua nafasi ya Jonas Mkude.

Mfungaji wa bao la tatu, Meddie Kagere alichukua nafasi ya nahodha John Bocco na kiungo fundi, Larry Bwalya alichukua nafasi ya Bernard Morrison aliyekuja kuingia kipindi cha pili.

Sven alisema; “Katika timu yangu nina machaguo ya wachezaji 28, ambao wote wanafanya vizuri inafikia wakati natamani kuwatumia kama walivyo ila sheria za soka zinanibana natakiwa kuwa na wachezaji 11, uwanjani na wengine saba katika benchi.”

“Ubora wa wachezaji hao imenilazimu kufanya mabadiliko ya wachezaji hao wanne ambao wote wamefanya vizuri na unakosa sababu hata ya kushindwa kuwapa nafasi katika mechi ijayo.

“Ukiangalia na wale ambao hawakuvaa walikuwa jukwaani na wengine walikuwa katika benchi la akiba wote wanaviwango bora ambavyo nitajitahidi kufanya mabadiliko mengine na kuwapa nafasi katika michezo ijayo.

“Nimefurahishwa na kiwango cha kila mchezaji ambaye amecheza katika mechi na Biashara United, jambo ambalo linaendelea kunitoa wasi wasi na kuwa na machaguo mengi ya wachezaji kuwatumia kutokana na wapinzani walivyo,” alisema Sven.

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema malengo ambayo waliingia nayo katika mechi dhidi ya Simba ya kupata suluhu yalifeli kutokana na ubora ambao walionesha wapinzani wao.

“Ukiangalia tumekuwa tukipata matokeo mabaya ugenini kama ambavyo tumeanza msimu huu tumeshinda mbili nyumbani na kupoteza moja ugenini jambo ambalo msimu huu natakiwa kulifanyia kazi,” alisema.

“Wachezaji wangu wanapocheza mechi za ugenini wanaonekana kukosa hali ya kujiamini kama inavyokuwa mechi za nyumbani, nimeliona hilo na katika kulifanyia kazi kila tutakapokuwa ugenini tutacheza pia mechi ya kirafiki,” alisema.

“Sababu nyingine iliyopelekea kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao timu yangu kutokupata muda wa kutosha kucheza mechi za kirafiki kwani mchezo wa kwanza wa kujiandaa ulikuwa dhidi ya Gwambina ambao ulikuwa pia wa ligi,” aliongeza Baraza.

52

Straika nyota Simba, Meddie Kagere alipachika bao lake la kwanza la msimu huu dakika hiyo kwenye mechi ya juzi dhidi ya Biashara

03

Luis Jose ambaye ni raia wa Msumbiji alitengeneza asisti tatu katika ushindi wa mabao 4-0 iliopata Simba dhidi ya Biashara

MECHI 4 ZIJAZO

SIMBA vs GWAMBINA-Dar

JKT TANZANIA-Dom

PRISONS-Mbeya

YANGA-Dar

 

YANGA vs MTIBWA-Moro

COASTAL-Dar

POLISI-Dar

SIMBA-Dar