Simba, Gor Mahia zaubeba Ukanda wa CECAFA

Muktasari:


Mbali na Gor timu nyingine zilizofuzu RSB Berkane na Hassania Agadir kutoka Kundi A, kutoka Kundi B limeingiza timu za CS Sfaxien na Etoile du Sahel, Kundi C limeingiza timu za Al Hilal Omdurman na Nkana FC wakati kutoka Kundi D, Gor Mahia imevuka na Zamalek.

Miamba ya Tanzania, Simba na Kenya, Gor Mahia zimeubeba Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati chini ya Baraza la Vyama vya Soka (Cecafa) baada ya timu hizo kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Simba imekuwa ya kwanza kukata tiketi hiyo juzi baada ya kuibandua nje ya michuano, AS Vita ya DR Congo katika mchezo uliokuwa mkali na kusisimua kwenye Uwanja wa Taifa.
Wekundu hao wa Msimbazi wamefuzu robo fainali pamoja pamoja na miamba mingine ya Kundi D, Al Ahly ya Misri. Nyingine ni Wydad Casablanca (Morocco) na Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini zilizofuzu kutoka Kundi A.
Kundi B limetoa timu za Esperance ya Tunisia na Horoya ya Guinea wakati Kundi C ni TP Mazembe ya DR Congo na CS Costantine ya Algeria.
Bao la Simba lililowapa ushindi lilipatikana dakika ya 89 likiwekwa kimiani na Clatous Chama. Awali Simba ilikuwa nyuma kwa bao la Kasadi lililosawazishwa na Mohamed Hussein 'Tshabalala'.
Kwa upande wa Gor Mahia, iliyokuwa ikihitaji ushindi, ilitimiza hayo kwa bao la Jacques Tuyisenge lililowaangamiza Petro Atletico kutoka Angola. Miamba hiyo ya Angola ilishinda mabao 2-1 mchezo wa kwanza uliofanyika mjini Luanda.
Hata hivyo, katika mchezo huo, Gor Mahia ilicheza pungufu wakiwa tisa uwanjani, baada ya wachezaji wake wawili kulimwa kadi nyekundu pamoja na kocha, Hassan Oktay baada ya kuwajia juu waamuzi hao.
Wachezaji walioonyeshwa kadi nyekundu ni Ernest Wendo dakika ya 36 wakati Shafiq Batambuze alionyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 44. Wendo alilimwa kadi nyekundu baada ya kumkata kiungo wa Petro Atletico, Vladamir Eston.
Mbali na Gor timu nyingine zilizofuzu RSB Berkane na Hassania Agadir kutoka Kundi A, kutoka Kundi B limeingiza timu za CS Sfaxien na Etoile du Sahel, Kundi C limeingiza timu za Al Hilal Omdurman na Nkana FC wakati kutoka Kundi D, Gor Mahia imevuka na Zamalek.