Simba, Big Bullets zatunziana heshima Dar

Muktasari:

Mechi hiyo ilikuwa sehemu ya maandalizi ya Simba na Big Bullets zinazojiandaa na mashindano ya Afrika yatakayoanza mwisho wa mwezi huu.

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wamemalimishwa suluhu na Big Bullets katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa imecheza mechi hiyo ya kirafiki bila ya uwepo wa nyota wake wanatumia timu za taifa ilishindwa kufanya kile kilichotegemewa na mashabiki wao.

Simba ilionekana kuanza kipindi cha kwanza kwa kupasiana pasi nyingi, lakini hawaku tengeneza nafasi yoyote ya wazi.

Safu ya kiungo iliyoundwa na Hassan Dilunga, Said Ndemla, Mzamiru Yassin, Mohammed Ibrahim na Haruna Niyonzima ilishindwa kabisa kupitisha pasi nzuri za mwisho kwa mshambuliaji Mohamed Rashid ‘MO’.

Mshambuliaji Mo Rashid alipata nafasi mmoja ya wazi katika kipindi cha kwanza, lakini shuti lake lidakwa na kipa.

Wageni Big Bullets ilikuwa imara katika safu yake ya ulinzi huku wakionekana wakicheza kwa kujiamini zaidi kila muda ulivyokuwa unakwenda.

Bullets ilitegeneza nafasi kadhaa wakitumia mashambulizi ya kushtukiza, lakini walilkosa umakini katika umaliziaji.