Simba, Azam zaujaza Gombani

Muktasari:

Kocha wa Azam Hans Pluijm alilazimika kufanya mabadiliko ya kwanza kwa kumtoa Tafadzwa Kutinyu aliyeonekana kutokuwa fiti ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Ramadhan Sindano mabadiliko hayo aliyafanya dakika ya 24.

Fainali za kombe la mapinduzi kati ya Simba na Azam zimeujaza uwanja wa Gombani, Pemba baada ya mashabiki kujitokeza kwa wingi huku ikielezwa tiketi zimemalizika kabla hata hata ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo kumalizika huku Azam ikiongoza kwa bao 1-0.
Azam ilipata bao hilo kupitia kiungo wao Mudathir Yahya dakika 44 baada ya kupiga shuti lililokwenda mavuno moja kwa moja, shuti hilo lilitokana na krosi iliyopigwa na Enock Atta.
Mchezo huo wa fainali umeonekana kuwa na upinzani mkubwa kwa timu zote mbili ambapo kipindi cha kwanza zimecheza kwa kushambuliana ingawa Simba nafasi walizopata walishindwa kuwa makini katika ufungaji.
Atta ndiye aliyeonekana mwiba katika dakika 45 za kwanza kwa kuisumbua ngome ya Simba iliyoongozwa na Yusuph Mlipili na Paul Bukaba.
Kocha wa Azam Hans Pluijm alilazimika kufanya mabadiliko ya kwanza kwa kumtoa Tafadzwa Kutinyu aliyeonekana kutokuwa fiti ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Ramadhan Sindano mabadiliko hayo aliyafanya dakika ya 24.
Kipa wa Simba,  Ally Salim alilazimika kupangua mashuti ya Obrey Chirwa mara mbili ambayo yalitokana na krosi ya Atta.
Simba ambao pia walifika Langoni mwa wapinzani wao mara kwa mara walikosa mabao kupitia wachezaji wao Abdul Seleman na Shiza Kichuya ambapo mashiti yao yalitoka nje ya lango huku kipa wa Azam, Razak Abalora akionyesha umaridadi wa kupanga hatari zote.
Mwamuzi wa mchezo huo Mfaume Ali, alilazimika kutoa kadi ya njano kwa Atta baada ya kuonyesha kucheza rafu.