Silaha sita Yanga ikivaana na KMC

Sunday October 25 2020
kmc yanga pic

Siku chache baada ya watani zao wa jadi, Simba kufungwa na Tanzania Prisons bao 1-0, Yanga inashuka uwanjani ugenini leo kucheza na KMC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Simba ilipoteza mchezo wake wa sita kwa bao la Samson Mbangula ambalo lilihitimisha rekodi ya mabingwa hao watetezi kutofungwa tangu Ligi Kuu msimu huu ilipoanza.

Hata hivyo, kwa upande wa Yanga katika mchezo wa leo nyota sita wanaounda safu ya ulinzi ndio watakaokuwa silaha muhimu ambayo itaitegemea. Wachezaji hao ni kipa Metacha Mnata, mabeki Shomary Kibwana, Yassin Mustafa, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto na kiungo Mukoko Tonombe.

Kiwango bora na uimara ulioonyeshwa na wachezaji hao katika mechi tano zilizopita za ligi hapana shaka vinalipunguzia mzigo benchi la ufundi la Yanga katika maandalizi ya kimbinu kwa ajili ya kuwakabili KMC.

Mawasiliano mazuri baina yao, uwezo wa kutibua mashambulizi ya timu pinzani na ushiriki wa kupanga mashambulizi ya timu yao bila shaka vitamsukuma Kocha Cedrick Kaze kutumia muda mwingi katika mchezo kushughulika na safu ya ushambuliaji ambayo imeonekana haijakaa sawa kabla na baada ya ujio wake.

Ukuta wa Yanga umecheza mechi tano mfululizo za ligi bila kuruhusu bao na safu ya ushambuliaji ya KMC ambayo inaonekana kuyumba katika siku za karibuni itakuwa na kazi ya kufanya kuupenya ili kufunga mabao.

Advertisement

Mbinu ya kupiga pasi nyingi za haraka kuelekea langoni mwa adui ambayo inapendelewa na Kaze itakutana na kipimo kutoka kwa KMC ambayo silaha yake tegemeo katika mechi dhidi ya timu kubwa ni kujaza idadi kubwa ya wachezaji katika safu ya kiungo ambao huwa na hulka ya kukabia katika robo ya mwisho ambalo ni eneo la hatari la adui.

Hakuonekani kutakuwa na mabadiliko makubwa katika kikosi cha Yanga na kile kilichoshinda kwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania juzi kinaweza kuanzishwa tena kinachoundwa na Metacha, Kibwana, Mustafa, Moro, Mwamnyeto, Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Songne Yacouba, Haruna Niyonzima na Farid Musa.

Historia ya mechi nne zilizopita za Ligi Kuu baina ya timu hizo inaonyesha Yanga imeibuka na ushindi mara mbili na kupoteza moja, huku mara moja zikitoka sare.

Kwa upande wa KMC inaweza kuwa na kikosi chenye wachezaji Juma Kaseja, Israel Patrick, David Bryson, Andrew Vincent, Lusajo Mwaikenda, Hassan Kapalata, Hassan Kabunda, Abdul Hillary, Reliants Lusajo, Emmanuel Mvuyekure na Kenny Ally.

Makocha wanasemaje?

Kocha wa Yanga, Cedrick Kaze alisema ana imani upungufu waliouonyesha katika mechi iliyopita wataurekebisha na kufanya vizuri.

“Hatukuwa wazuri katika kufanya maamuzi pindi tulipokuwa katika lango la timu pinzani, lakini tunaendelea kurekebisha. Mchezo wa KMC najua utakuwa mgumu lakini tunahitaji kushinda na kupata pointi tatu,” alisema Kaze.

Kocha wa KMC, Habibu Kondo alisema anaamani ataibuka na ushindi mnono.

“Tumekuja Mwanza kutafuta alama tisa katika michezo mitatu, kesho (leo) tunachukua alama tatu kwa Yanga, halafu tunaenda kuchukua kwa Gwambina, Biashara na hivyo tukirejea jijini Dar es Salaam tunarudi kwa kishindo kutokana na ushindi tutakaokuwa tumeupata,” alisema.

Ukiondoa mchezo huo kutakuwa na mechi nyingine mbili ambapo ya kwanza ni Polisi Tanzania dhidi ya Biashara United katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid - Arusha utakaochezwa kuanzia saa 8.00 mchana.

Advertisement