Siku za Sarri kubaki Chelsea zinahesabika

Muktasari:

Chelsea haichezi tena hadi Machi 31 ambapo itasafiri mpaka kusini mwa Wales kucheza na Cardiff inayohaha isishuke daraja na Abramovich ana wiki mbili za kuamua kama amfukuze kocha huyo wa zamani wa Napoli au amuache kibaruani.

LONDON, ENGLAND.HALI si shwari kwa Mzee wa sigara bwana Maurizio Sarri. Jahazi linazama, linaibuka, kisha linazama tena. Juzi Jumapili amechapwa ugenini dhidi ya Everton na inadaiwa Chelsea inaweza kumtimua wakati ligi ikiwa imesimama kupisha mechi za kimataifa.

Everton iliichapa Chelsea mabao 2-0 dimba la nyumbani Goodson Park na inadaiwa kocha huyo Muitaliano yuko katika presha ya kufukuzwa kufuatia matokeo mabovu na pia sakata lake na kipa, Kepa Arrizabalaga aliyegomea maamuzi yake pambano la fainali Kombe la Ligi dhidi ya Man City pia limemshushia hadhi.

Inasemekana tajiri wa Chelsea, Roman Abramovich ambaye kwa sasa haruhusiwi kuingia Uingereza, amechoshwa na mambo yanavyokwenda Stamford Bridge na anaweza kutumia kipindi hiki cha mapumziko wakati wachezaji wakienda kuchezea timu zao za taifa kumfukuza Sarri.

Chelsea haichezi tena hadi Machi 31 ambapo itasafiri mpaka kusini mwa Wales kucheza na Cardiff inayohaha isishuke daraja na Abramovich ana wiki mbili za kuamua kama amfukuze kocha huyo wa zamani wa Napoli au amuache kibaruani.

Mabao mawili ya Richarlison na Gylfi Sigurdsson yalitosha kuifanya Chelsea ipoteze mechi ya saba katika Ligi Kuu England msimu huu licha ya kuanza kwa mbwembwe huku ikitazamiwa kuwania ubingwa sambamba na Manchester City na Liverpool.

Kichapo cha juzi kinaifanya Chelsea iachwe nyuma kwa pointi tatu na Arsenal inayoshika nafasi ya nne na sasa kuna hatihati wababe hao wa London wakacheza michuano ya Europa kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kukosa Top Four mwaka jana.

Chelsea iliondolewa katika michuano ya FA na Manchester United ikiwa nyumbani Stamford Bridge na endapo itakosa Top Four basi nafasi yao kubwa ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao itabakia eneo moja tu kama wakichukua ubingwa wa Europa msimu huu.

Katika pambano la juzi, Sarri aliamua kuendelea kumuamini mshambuliaji wake wa kimataifa wa Argentina, Gonzalo Higuain aliyemchukua kutoka kwa mkopo kutoka Juventus dirisha la Januari na aliamua kumuweka benchi mshambuliaji wa Ufaransa, Olivier Giroud ambaye alipiga Hat trick Alhamisi iliyopita dhidi ya Dynamo Kiev ugenini katika michuano ya Europa League.

Katika pambano la juzi, Sarri ambaye alipewa kibarua hiki akichukua nafasi ya Muitaliano mwenzake, Antonio Conte, alidai hajui ambacho kiliwatokea wachezaji wake katika kipindi cha pili cha pambano hilo.

“Sijui na wachezaji hawajui kilichotokea katika kipindi cha pili. Siwezi kuelezea. Tulicheza vema katika kipindi cha kwanza na tungeweza kufunga mabao manne hadi matano lakini ghafla tukaacha kucheza. Ilishangaza sana. tulimiki mechi na kucheza vema lakini hatukujilinda vema katika kipindi cha pili,” alisema Sarri.

“Tulibadilisha mfumo lakini mambo yalikuwa yale yale. Tatizo lilikuwa akili zetu uwanjani kwahiyo mfumo au mbinu hazikuwa muhimu. Halikuwa suala la hamasa kwa sababu tulianza mechi vizuri. Inabidi tucheze mechi nane sasa na inabidi tupambane kwa ajili ya majukumu yetu,” alisema Sarri.