Siku ya Solskjaer kufutwa kazi Man United yatajwa

Muktasari:

Ghafla kila kitu kilibadilika. Hata miezi miwili haijapita, tayari Solskjaer ameanza kukalia kuti kavu kwenye kikosi hicho akipambana kuweka salama kibarua chake.

MANCHESTER, ENGLAND.HABARI ndio hiyo. Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ameshaanza kuwa na presha kuhusu usalama wa kibarua chake huko Old Trafford, ikiwa hata miezi miwili haijapita tangu alipopewa kibarua cha kudumu na bosi Ed Woodward.

Wachambuzi wa mambo wameshapanga siku za Solskjaer kufutwa kazi kwenye kikosi hicho cha Man United. Bosi huyo wa Man United, Solskjaer alipewa kibarua cha kudumu Machi mwaka huu. Kwa wakati anapewa kibarua hicho, hakuna aliyekuwa akimhoji Woodward kwa uamuzi huo.

Man United ilikuwa imeshinda mechi 14 kati ya 17 ilizokuwa imecheza chini ya kocha huyo, huku ikigawa vipigo kwa vigogo kama PSG, Chelsea, Arsenal na Tottenham. Kasi hiyo ilirudisha matumaini kwamba moto wa Man United umerudi. Walikuwa bora kwenye beki na mbele, Paul Pogba, Marcus Rashford, Jesse Lingard na hata Romelu Lukaku waliuwasha moto.

Ghafla kila kitu kilibadilika. Hata miezi miwili haijapita, tayari Solskjaer ameanza kukalia kuti kavu kwenye kikosi hicho akipambana kuweka salama kibarua chake.

Man United imeshinda mechi mbili tu kati ya 12 za mwisho. Kipigo cha kutoka kwa Cardiff kwenye mchezo wa mwisho Old Trafford msimu huu kimefichua rasmi tarehe ambayo Solskjaer atafunguliwa geti la kutokea huko Manchester.

Suala la kufuta kazi makocha wake Man United imekuwa ikilifanya sana kwa miaka ya karibuni, ambapo ilianza na David Moyes, ikaja kwa Louis van Gaal na hivi karibuni Jose Mourinho. Wadau wanaamini hivi, kama Solskjaer atashindwa kuiweka Man United ndani ya Top Four hadi kufika Desemba, basi hakuna namna atafutwa tu kazi. Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kitu muhimu katika timu hiyo, hasa ukizingatia kwamba msimu ujao hawatakuwapo na hawatahitaji kuendelea kuwa nje ya michuano hiyo kwa misimu mingine zaidi.

Man United imekuwa na msimu wa hovyo kwelikweli, ambapo pointi 66 ilizovuna kwenye ligi, imedaiwa kwamba imelipa Pauni 100,000 kwa kila pointi moja.

Rekodi ziko hivi, Man United inalipa mshahara wa Pauni 6,534,654, ikiwa ni nyingi zaidi kwenye ligi hiyo kuliko timu yoyote, hivyo kwa pointi 66 walizopata hiyo ni sawa na kulipa Pauni 99,010 kwa kila pointi.

Alexis Sanchez, ambaye hajafunga bao lolote kwenye Ligi Kuu England tangu Oktoba mwaka jana, anavuna Pauni 505,000 kwa wiki, wakati Paul Pogba anapokea Pauni 290,000 kwa wiki, huku kwenye timu hiyo kukiwa na wachezaji kama Jesse Lingard ambao nao wanalipwa pesa nyingi, lakini hakuna cha maana wanachofanya uwanjani. Man City, ambao ni mabingwa na wameiacha Man United kwa pointi 32, wenyewe wametumia Pauni 61,513 kwa pointi kutokana na bili yao ya mishahara wanayolipa kwenye kikosi hicho, Pauni 5,993,000.