Siku 481 TFF bila kufanya mkutano mkuu

Muktasari:

  • Tangu uongozi mpya wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) uingie madarakani ni zaidi ya mwaka sasa bila kufanya mkutano mkuu na walipanga kuufanya mwishoni mwa mwezi huu lakini umesogezwa mbele hadi Februari sambamba na uchaguzi mdogo wa shirikisho.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) lilipanga kuitisha Mkutano Mkuu wa mwaka Desemba 29, lakini ghafla mkutano huo umeyeyuka hadi Februari 2 mwakani ili kwenda sambamba na uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizo wazi.

Huo ungekuwa mkutano wa kwanza wa TFF iliyopo chini ya Rais Wallace Karia aliyeingia madarakani na wenzake Agosti 12, mwaka jana, ambao ungetumika kujadili bajeti mpya ya mwaka, mapato na matumizi ya mwaka uliopita na mambo mengine, lakini kuahirishwa kwao umefanya leo Alhamisi kutimiza siku 481 bila mkutano mkuu.

Siku hizo 481 ni sawa na mwaka mmoja na miezi mitatu na siku 24 bila TFF kuitisha mkutano mkuu, huku lenyewe likiwa mbele kuzikomalia klabu kutekeleza mwongozo wa katiba zao.

Mkutano huo upo kwenye Katiba ya TFF inayoelekeza Kamati ya Utendaji inapaswa kuitishwa mkutano mkuu unaohudhuriwa na klabu wanachama pamoja na vyama vingine ambavyo ni wanachama wa shirikisho hilo.

Mapema wiki hii Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho hilo chini ya Mwenyekiti wake, Ally Mchungahela alitangaza uchaguzi mdogo wa shirikisho ambao ni kujaza nafasi za wajumbe walioenguliwa kwenye nafasi hizo ama kujiuzulu kwa nafasi mbalimbali kutoka mikoani na Kamati ya Utendaji.

Katika ratiba ya uchaguzi huo inaonyesha kuanzia Desemba 4-9 itakuwa mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu za wagombea.

Imeelezwa kwa kawaida mkutano mkuu kikatiba ni lazima uendane na uchaguzi mdogo na hiyo ndiyo sababu ya kusogeza mbele mkutano huo uliopangwa kufanyika jijini Arusha.

TFF wenyewe bado haijatangaza kusogeza mbele mkutano huo, ila Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Mchungahela aliliambia Mwanaspoti kwamba mabadiliko hayo yapo kwani ni maelekezo ya kikatiba.