Sikia makocha Top Six wanachosema kuhusu Ole

Muktasari:

  • Baada ya Solskjaer kupewa kibarua cha kudumu Old Trafford, waliulizwa makocha wengine wa timu wapinzani hasa wale waliopo kwenye Top Six ambao wanauhakika mkubwa wa kuendelea kubaki kwa msimu ujao kutoa maoni yao kama Man United imefanya uchaguzi sahihi au imekosea kwa kumpa kazi hiyo nzito kocha Solskjaer.

MANCHESTER, ENGLAND.OLE Gunnar Solskjaer ndio kama ulivyosikia amebeba dili la kuwa kocha mkuu kwenye kikosi cha Manchester United.

Kocha huyo alianza kwa kuwa kocha wa muda huko Old Trafford na baada ya kushinda mechi 14 kati ya 19, basi mabosi wa Man United wakaamua kumsainisha mkataba wa miaka mitatu na kumtangaza rasmi kuwa kocha wao mpya.

Tangu wakati huo alipochaguliwa kuwa kocha mkuu, Solskjaer ameiongoza Man United katika mchezo mmoja na kushinda Jumamosi iliyopita alipowachapa Watford 2-1 na kuingiza timu kwenye Top Four kabla ya matokeo ya Arsenal katika mchezo wao wa usiku wa jana Jumatatu dhidi ya Newcastle United huko Emirates.

Baada ya Solskjaer kupewa kibarua cha kudumu Old Trafford, waliulizwa makocha wengine wa timu wapinzani hasa wale waliopo kwenye Top Six ambao wanauhakika mkubwa wa kuendelea kubaki kwa msimu ujao kutoa maoni yao kama Man United imefanya uchaguzi sahihi au imekosea kwa kumpa kazi hiyo nzito kocha Solskjaer.

Unai Emery – Arsenal

Licha ya kuingia Man United, Desemba tu hapo, lakini Solskjaer ameshakabiliana na Emery mara mbili kwenye Uwanja wa Emirates. Kwanza ilikuwa kwenye Kombe la FA na Man United ilishinda 3-1, kabla ya kukutana kwenye Ligi Kuu England na Arsenal kushinda 2-0.

Emery alisema hivi kuhusu Solskjaer: “Namkumbali sana Solskjaer kama mtu na kama kocha.” Hayo ndiyo yaliyokuwa maneno ya Mhispaniola huyo alipoulizwa kama Man United imefanya chaguo sahihi kwa kumteua Solskjaer kuwa kocha wao wa kudumu.

Jurgen Klopp – Liverpool

Kutokana na kufutwa kazi kwa Jose Mourinho huko Man United baada ya kichapo cha Anfield, Desemba mwaka jana, Solskjaer alikuwa kwenye mechi ya raundi ya pili kwenye Ligi Kuu England alipomenyana na Liverpool na kumalizika kwa sare ya 0-0 Uwanjani Old Trafford, Februari.

Bila shaka Klopp atakuwa mmoja wa makocha wanaofurahia kubaki kwa Solskjaer kwenye ligi, alisema:

”Nina imani amekuwa akiitaka nafasi hiyo kwa nguvu zote na huo ndio ulikuwa mpango wake. Ameshathibitisha hilo, hivyo atafanya kazi vizuri.”

Pep Guardiola – Man City

Kinachoelezwa mechi muhimu kabisa ya Manchester City kwenye mbio zao za ubingwa wa Ligi Kuu England itakuwa hapo watakapokwenda kumkabili Solskjaer uwanjani Old Trafford baadaye mwezi huu.

Kwa kipindi hicho pengine Man United itakuwa bado haijafahamu hatima yao kwenye Top Four huku Guardiola naye na Man City yake akiwa hana uhakika wa ubingwa kutokana na kuchuana na Liverpool.

Kuhusu uteuzi wa Solskjaer, Guardiola alisema: “Siku zote United ni wapinzani wazuri sana. Nampongeza, amefanya vizuri hasa kwenye upande wa matokeo hivyo namtakia kila la heri.”

Mauricio Pochettino – Tottenham

Wakati Tottenham Hotspur ilipoonyesha upinzani kwenye mbio za ubingwa miezi michache iliyopita, kocha Mauricio Pochettino alikuwa akitajwa kwamba huenda angeenda kuchukua mikoba ya kuinoa Manchester United.

Lakini, baada ya hapo mambo yamekuwa magumu na Spurs imekuwa ikipoteza tu pointi hivyo Pochettino kwenda Old Trafford likifutwa na Solskjaer akikabidhiwa timu rasmi. Kuhusu jambo hilo, Pochettino alisema: “Kamwe huwa sizungumzii mambo ya uvumi. Ninachotaka ni kumpongeza tu na kumtakia kila lenye heri baada ya sasa kuwa kocha mpya wa Manchester United.”