Sikia Staa Molinga anavyofanya huku!

Muktasari:

Alizungumzia mabao 15 na zaidi, ambayo Kocha Mwinyi Zahera aliweka wazi kuwa mchezaji huyo lazima ayafunge ndani ya msimu huu na ikishindikana akatwe mkono au atatoa dola 1,000 kwa waandishi wa habari.


STRAIKA anayeongoza kwa mabao ndani ya kikosi cha Yanga, David Molinga ‘Papaa Molinga’ ameamua kujifungia ndani nyumbani kwake na kukifanya mazoezi kwani corona imemfanya aogope hata kwenda Gym na akasisitiza mpango wake wa kufunga mabao 15 na zaidi atakaporudi kwenye kivumbi cha Ligi Kuu uko palepale.

“Hata gym mimi siendi kabisa, ngoja kutulie kwanza, mazoezi nafanya nyumbani kwangu binafsi asubuhi na jioni,” alisema Molinga ambaye kwa sasa anaishi mwenyewe Dar es Salam baada ya familia yake kuisafirisha Ufaransa wanakoishi.

Alizungumzia mabao 15 na zaidi, ambayo Kocha Mwinyi Zahera aliweka wazi kuwa mchezaji huyo lazima ayafunge ndani ya msimu huu na ikishindikana akatwe mkono au atatoa dola 1,000 kwa waandishi wa habari.

“Siku zote mpira hauchezwi mdomoni kwa watu, unachezwa uwanjani. Binafasi sina wasiwasi juu ya hilo nina uwezo wa kufunga lakini yote ni pale nitakapopata nafasi ya kucheza, Inshaallah Mungu mwema, tutafika,” alisema Molinga.

“Hamu yangu ni kufunga kila mechi na najua iko hivyo hata kwa mashabiki wa Yanga na benchi la ufundi, tuombe Mungu. “

Mpaka sasa Molinga ndiye kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga, licha ya kutocheza mechi nyingi kutokana na matatizo ya kifamilia, maumivu na uamuzi wa benchi lake la ufundi amepachika mabao manane kwenye ligi.

Molinga mwenye mwili mkubwa, amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga, katika kuwania ufungaji bora kinara wa mabao ni Mnyarwanda wa Simba, Meddie Kagere anaongoza baada ya kupachika mabao 19.

Ligi Kuu imesimama kupisha janga la ugonjwa wa Corona.