Sibomana apiga tatu, Sadney mbili Yanga yapiga wiki Moro

Muktasari:

Wakati Sibomana akipiga hat trick, mshambuliaji wa kimataifa wa Namibia, Sadney Urikhob alipiga bao mbili huku mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Juma Balinya na wenzake wa Lamine Moro kutoka Ghana kila mmoja alifunga bao moja moja katika ushindi huo wa mabao 7-0

Morogoro. Mshambuliaji mpya wa Yanga, Mnyarwanda Patrick Sibomana ameanza kuonyesha makali baada ya kupiga bao tatu pekee yake (hat trick) wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 7-0 mbele ya Morogoro Athletics Soccer Academy katika mchezo wa kirafiki uliopigwa uwanja wa chuo cha biblia Bigwa mkoani Morogoro.

Wakati Sibomana akipiga hat trick, mshambuliaji wa kimataifa wa Namibia, Sadney Urikhob alipiga bao mbili huku mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Juma Balinya na wenzake wa Lamine Moro kutoka Ghana kila mmoja alifunga bao moja moja katika ushindi huo wa mabao 7-0.

Katika mchezo huo, Sibomana alianza kufungua kitabu cha mabao dakika ya 17 kwa shuti kali lililotokana na kona iliyochongwa na Sadney Urikhob wakati bao lake la pili akifunga dakika 40 kufuatia kazi nzuri ya kiungo, Papy Tshishimbi kabla ya dakika ya 59 kufunga la tatu kwa penati.

Mshambuliaji Urikhob alifunga mabao yake mawili katika dakika za 38 na 59 baada ya kazi nzuri ya Juma Balinya aliyetoa pasi za mabao hayo wakati washambuliaji, Juma Balinya alifunga bao moja katika mchezo huo dakika ya 33 na mlinzi, Lamine Moro alifunga bao lake kwa kichwa dakika ya 80.

Mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo walionekana kukikubali kikosi cha wanayanga hao kuanzia safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji kutokana na uwelewano nzuri katika mchezo huo huku wapinzani wao wakimiliki vyema mpira na kukosa mbinu za kuipenya ngome ya Yanga na kupata bao.