Shukrani kocha Amunike, naona ameanza kutuelewa

Monday September 10 2018

 

By EDO KUMWEMBE

DAKIKA 90 za kwanza za Emmanuel Amunike kama kocha wa Taifa Stars zilimalizika Kampala Uganda juzi Jumamosi jioni na kuwaacha wenyeji wasijue kilichowapata. Walitarajia ushindi wakaishia kupata suluhu wasiyoitarajia. Ni kwa sababu ya Amunike.

Anaonekana kuwa kocha kwelikweli. Siku chache alizowasoma wachezaji wa Tanzania, kisha wapinzani wake Uganda, alijua namna ya kutuchezesha. Alifanya kile ambacho Marcio Maximo alikuwa anakifanya alipowasili mwaka 2006.

Baada ya kugundua Waganda wametuzidi uwezo, karibu timu yote ikiwa na wachezaji wanaocheza nje ya nchi yao na wanajitambua, Amunike alitutengenezea nidhamu nzuri katika eneo la ulinzi. Aliweka watu watatu katika eneo la katikati. Agrey Morris, David Mwantika na Abdi Banda. Kushoto alicheza Gadiel Michael na kulia akacheza Hassan Kessy.

Hawa Kessy na Gadiel walikuwa wanacheza kama mabeki mawinga. Katikati wakacheza Frank Domayo na Mudathir Yahaya ambaye alikuwa katika kiwango bora. Kutokana na nidhamu nzuri ambayo aliwatengenezea, Domayo na Mudathiri walicheza zaidi chini.

Kwa Domayo na Mudathir kucheza chini kulimaanisha Saimon Msuva, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu walikuwa na kazi ya kurudi chini kukusanya mipira na kujitengenezea mashambulizi wenyewe.

Sawa, mashambulizi hayakuwa mengi lakini ni wazi tusingeweza kupishana na Uganda kirahisi. Miaka ya karibuni wamekuwa wakitutambia kiurahisi zaidi. Tulihitaji kubuni kuwazuia kwanza kabla hatujatafakari kuwafuata katika eneo lao.

Advertisement

Katika kuwafuata eneo lao tulihitaji kasi. Sikushangazwa kuona mshambuliaji wetu mpya staa, Shaban Chilunda akikaa benchi. Licha ya tiketi ya ndege kumshusha Dar es salaam kwa ajili ya mechi hii lakini aina yake ya soka ni tofauti na kile ambacho Amunike alihitaji.

Chilunda ni mmaliziaji mzuri sana hata hivyo, hana kasi kama ya Msuva na Ulimwengu. Hawezi pia kumfikia kasi Samatta. Amunike alihitaji watu wenye kasi kwa ajili ya kurudi nyuma na kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Chilunda atatufaa sana katika aina ya mechi ambazo tunalivamia lango la adui.

Haikushangaza kuona Msuva, Samatta na Ulimwengu walitengeneza mashambulizi hasa katika kipindi cha pili kutokana na kasi yao. Tulipata kona, mipira ya adhabu na pia kufanya kosa kosa nyingine.

Hii ndio namna ya kucheza na timu ambayo unaiheshimu na unajua imekuzidi uwezo. Kwa baadhi ya makocha wazawa wangeingiwa na tamaa ya kuwapanga Msuva, Chilunda, Samatta, Ulimwengu na Farid Mussa kwa pamoja. Iliwahi kutokea kitu kama hiki wakati tulipofungwa mabao 7-0 na Algeria ugenini.

Shukrani nyingine kwa Amunike zinakwenda kwa namna ambavyo alimtumia Mwantika.

Huyu aliitwa baada ya Erasto Nyoni kushindwa kwenda kambini. Nilipenda kombinesheni ya Mwantika na Aggrey lakini hapa Amunike anatuonyesha jinsi alivyotambua ubora wa Mwantika ndani ya siku chache alizokaa naye mazoezini.

Mwantika ana mwili mkubwa, anajua kuruka juu vizuri na ana kasi. Ni aina ya beki ambaye utamuhitaji pindi utakapocheza na wachezaji wenye maumbo makubwa kama Waganda. Baada ya mechi ya juzi sioni namna ambavyo Amunike anaweza kumuacha kiurahisi.

Wachezaji wetu wa kulipwa wanaocheza nje ya Tanzania walitubeba. Zaidi ya kutubeba lakini waliipigania bendera yao. Ungeweza kutazama nyuso zao na kugundua walikuwa wameipania mechi. Ni tofauti na mechi kadhaa zilizopita.

Ni rahisi kumlaumu Samatta pindi anaposhindwa kufunga kwa sababu Watanzania wamekariri kuwa Samatta ni mtambo wa mabao, lakini mwisho wa siku kama uliichunguza mechi ungeweza kuona juzi Jumamosi alikuwa na kazi ya kurudi kukaba kama wachezaji wengine.

Banda alikuwa bora sana. mtulivu, makini na hakubutua ovyo. Alipenda kuichezesha timu kuanzia nyuma. Alionekana ameiva hasa na alicheza vizuri eneo la katikati na upande wa kushoto ambako alipaswa kuvutika kama Gadiel angekuwa ameondoka.

Kessy ni mchezaji anayekupa asilimia mia ya alichonacho mwilini. Ndicho alichofanya juzi. Anachopaswa kufundishwa, hasa na manahodha wa timu zake anazochezea ni kuacha kumlalamikia mwamuzi mara kwa mara na kwa sauti kali. Waamuzi wa Kiafrika waliojipanga kumpendelea adui ni rahisi kumuona na kumtoa nje kwa kisingizio cha kutoa lugha chafu.

Tukizichanga karata vema tunaweza kwenda Cameroon katika Afcon 2019. Tumepunguza mechi moja ngumu sana. Dhidi ya Uganda ugenini, ilikuwa ni mechi ngumu kama ilivyo dhidi ya Cape Verde ugenini. Kama umeambulia kupata suluhu Kampala kisha ukapata suluhu nyingine Cape Verde kisha kushinda mechi mbili Uwanja wa Taifa na kushinda moja ugenini dhidi ya Lesotho tunaweza kwenda Cameroon.

Kinachotakiwa kwa sasa ni kurudisha hamasa kwa mashabiki ili Uwanja wa Taifa uwe mgumu kama ilivyokuwa katika zama za Maximo. Dalili za mwanzo zinaonyesha Amunike ni kocha unayeweza kwenda naye vitani katika mechi ngumu. Hasa ukijikumbusha jinsi alivyowatuliza Waganda kwa nidhamu nzuri ya ulinzi.

Advertisement