Shoo ya Yanga yaingiliwa

KOCHA wa Mbeya City, Amri Said ambaye ni mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, amesisitiza shoo yao na Yanga Jumapili wataicheza kwa miguu yote miwili.

Amri ambaye pia ni mwanachama wa Simba, alisema kipigo cha mabao 4-0, hakina maana wala athari yoyote ya wao kuipiga Yanga Jumapili ya wiki hii kwenye Uwanja wa Mkapa.

Habari za ndani ya Mbeya City zinasema kipigo cha juzi kimewaamsha mpaka viongozi ambao wameamua kuingia kwa nguvu kwenye mchezo huo kuhakikisha hawapotezi tena.

Kama mechi dhidi ya KCM, timu hiyo haikuwa vizuri kuanzia kwenye safu ya ulinzi mpaka ushambuliaji, ambapo kocha naye alikiri kikosi chake kukosa muunganiko, pamoja na hilo halimtishi kuikabili Yanga, ambayo nayo haikuanza vyema dhidi ya Prisons, ikitoka sare ya bao 1-1, Uwanja wa Mkapa.

“Nikiri timu yangu haikuwa vizuri, mfano unaona kabisa safu ya ulinzi ilikosa umakini, kuna wakati kipa aliruhusu mabao mepesi ambayo angeweza kuokoa, lakini hayo yamepita tunaangalia yaliopo mbele yetu,” alisema kocha huyo.

“Pamoja na hilo, ifahamike KMC haiwezi kuwa Yanga, wala Yanga haiwezi kuwa KMC, nakwenda kurekebisha makosa ambayo yamefanywa na wachezaji wangu ili tujue tunarudi vipi kwenye mchezo uliopo mbele yetu,” alisema.

Alisema pamoja na kuwa timu ya kwanza kufungwa mabao mengi mpaka sasa, lakini hategemei wachezaji wake kuikabili Yanga kwa kiwango kile kile kama walichokionyesha dhidi ya KMC.

Hata hivyo, Mbeya City ina mlima mrefu wa kupanda dhidi ya Yanga kwani watoto hao wa jangwani watarejea katika mchezo huo wakiwa kama chui aliyejeruhiwa.

Lawama za mashabiki wa Yanga kwa kikosi chao zinaweza zisiwaache salama Mbeya City ingawa hata wao wanaweza wakashangaza katika mchezo huo.

Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic alisema timu yake inahitaji kupewa muda zaidi ili icheze kitimu kwani kwa sasa inakosa muunganiko lakini anamaini mchezo ujao timu hiyo itafanya vizuri.