Shime anawaza kombe tu huko Cecafa

Muktasari:

Wakizungumzia timu hiyo, baadhi ya mashabiki wa soka nchini waliwataka wachezaji kuendelea kujituma ili waweze kulibakiza kombe hilo hapa nchini.

KAMA kuna kitu ambacho kocha wa timu ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’, Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ anakiwaza, basi litakuwa ni Kombe la Cecafa.

Kama Tanzania Bara itachukua ubingwa huo kipindi hiki itakuwa ni mara ya tatu baada ya awali kulitwaa kule Uganda mwaka 2016 na kisha ikalinyakua pale Burundi mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo iwapo watalinyakua mara hii wataendelea kuwa vinara wa makombe hayo wakifuatiwa na ndugu zao Zanzibar waliochukua mara moja mwaka 1986 na baada ya hapo mashindano hayo kwa akina mama yalisimama kwa muda wa miaka 30.

“Sina kitu kingine ninachokifikiria zaidi ya ubingwa. Siangalii idadi ya mabao, hata kama tumefunga mengi kiasi gani, ila tunachoangalia ni ushindi tu hadi ubingwa,” alisema Shime.

Hata hivyo, ameweka wazi kuwa mchanganyiko wa damu changa na wazoefu umekifanya kikosi chake kuwa imara zaidi.

Alisema wachezaji wake Stumai Abdallah na Opa Clement waliokuwa majeruhi pamoja na Julitha Singano aliyekuwa na kadi mbili za njano wataendelea na mechi zijazo.

Wakizungumzia timu hiyo, baadhi ya mashabiki wa soka nchini waliwataka wachezaji kuendelea kujituma ili waweze kulibakiza kombe hilo hapa nchini.

“Inaonekana kwamba kwa wanawake mambo yetu sio mabaya, nachowaomba dada zetu wakze kamba ili tubebe tena ubingwa,” alisema Josephine Onesmo.

Naye Ibra Simao aliwataka Watanzania kuiunga mkono timu hiyo kwa nguvu kutokana na kuendelea kuipeperusha bendera ya nchi kwa kufika nusu fainali.